Jumapili, 20 Agosti 2017

NAFASI YA KWAYA KATIKA IBADA



Ni muhimu kila mwamini ajue kuimba nakumsifu Mungu kwa midomo yake, kusifu na kuabudu si kwa watu fulani au kundi maalumu tu. Bali uimbaji ni wajibu wa kila mtu ndani ya ibada. Ni muhimu iwepo tahadhari kwa kanisa kutojisahau jukumu la kuimba kuiachia kwaya na wengine wakawa wasikilizaji na watazamaji, hilo ni jambo la hatari na ni anguko mbele za Mungu. Kanisa lidumu katika sifa daima kwa ujumla.

KWAYA: Ni chombo chema sana ndani ya ushirika. Kama tunavyoona katika neno la Mungu INyak 16:4 INyak 23:30, IINyak 5:12-14 Haya ni maandiko yanayoelezea huduma ya kwaya katika ibada ilivyo muhimu.
(INyak 16:4-7)
Walawi walitengwa wamtumikie Bwana katika kumkumbusha Mungu na kutoa shukrani na sifa. Asafu alikuwa kiongozi mkuu wa huduma hii hekaluni

(INyak 23:30-31)
Kazi ya kwaya ilikuwa ni kutoa huduma ya sifa na shukrani katika ibada ya asubuhi na jioni kila siku hekaluni. Ratiba hii ya huduma inatakiwa idumishwe hata leo. Ni makosa kudhani kwamba kwaya ni ya siku maalum ama Jumapili tu, kwaya ipewe kuhudumu katika kila ibada.

(2Nyak 5:12-14.)
Waimbaji walibaki ndani ya hekalu wakiwa na roho moja, wakiimba sauti zao kwa mpangilio, wakimsifu na kumshukuru Mungu, na kuimba sambamba na muziki wa vyombo wakimsifu Bwana kwa wema na fadhili zake. Hekalu likajawa na utukufu wa Mungu, wingu la uwepo wa Mungu likawafunika. Huduma ya kwaya ni muhimu kama tunavyoona hapo juu, kushusha uwepo wa Mungu na kuliongoza kanisa kumsifu nakumshukuru Mungu kwa wema wake.

Hii inamaanisha kwaya ina jukumu la kutoa huduma ya sifa na shukrani, na kutunga nyimbo zenye mfumo huo bila kusahau utakatifu wa maisha yao.

Utunzi wa nyimbo uzingatie maadili ya kiroho, neno, mazingira, mahitaji ya kijamii, ubora wa mashairi, usanifu wa kitaaluma, Uongozi wa Roho Mtakatifu.

Si vema kuibuka na wimbo usiku mmoja na kuutumbukiza katika huduma. Wimbo unaweza kuutunga kwa muda mfupi ama kwa muda mrefu kutegemeana na kuridhika kwako ukizingatia hayo yaliyo tajwa hapo juu.

Ni jambo muhimu pawepo na maongozi makini katika kwaya kama Asafu alivyoongoza kwaya ya hekalu. Kwaya ni huduma haipaswi kuongozwa kwa mfumo wa kisiasa (kupiga kura) bali kwa mfumo wa huduma na malengo ya kihuduma na hasa kumtukuza Mungu ambapo kiongozi mkuu ni yule aliye na maono, na mbeba huduma ambaye ni mwalimu. Mwalimu ni kiongozi Mkuu wa kwaya kwa mujibu wa maandiko.
Uongozi wa aina hiyo pamoja na kamati zake utaendeleza huduma kama ilivyo katika neno. Mwalimu hapaswi kupigiwa kura bali anakuwa mwalimu kwa kipawa alichopewa na Mungu, hicho ndicho kinampa nafasi ya kuwa kiongozi wa kwaya.
Kila kanisa la mahali pamoja lizingatie kwa makini kulea vipawa na kuwatambua Walawi (waimbaji) waliopo kanisani na kuwasimika katika huduma hiyo kama mfalme Daudi alivyofanya (INyak 16:1-7).
Mchungaji awe karibu sana na kwaya katika utendaji wa siku kwa siku ili kudumisha mshikamano wa huduma yake na kwaya na kanisa, na kutoa msaada matatizo yanapotokea.
1.          ITEGEMEZE KWAYA
Kanisa zima liwe mdau mkuu wa kutegemeza kwaya kwa hali na mali ili iweze kusonga mbele katika fani ya uimbaji pasipo kukwama. Kumbuka asilimia sabini na tano ya shughuli za kanisa katika ibada ni kusifu (kuimba), kwa hiyo ni jambo jema wakristo wakawekeza nguvu zao katika kwaya ya kanisa. Kwaya zenye mafanikio ni zile ambazo nyuma yao iko nguvu ya kanisa kwa hali na mali, na maombezi.
Kwaya ina mvuto wa ajabu kwa watu, katika matukio mbalimbali ya kijamii. Kwa hiyo ni vema ipewe nafasi ya kutoa huduma katika matukio hayo, kama vile mikutano, semina, misiba, harusi, sherehe za kanisa na za kijamii maadamu kinachofanyika hakipingani na imani yetu na hakimdhalilishi Yesu.
Matukio ni uwanja mzuri kwa kwaya kumhubiri Yesu kupitia ujumbe wa nyimbo. Kama Kanisa litailea kwaya vizuri litavuna matunda ya baraka yasiyo na kifani.


MAFUNZO NI MUHIMU
Kanisa liimarishe na kufanya juhudi za makusudi kuwawezesha waimbaji wote kwa kuwapa mafunzo ya kusifu na kuabudu katika Roho na kweli, na kuhakikisha waimbaji wana viwango vya uimbaji vinavyokubalika.
Ibada ni kitu kitakatifu ambacho kinatakiwa kufanyika kwa utaratibu, hofu na unyenyekevu na kwa tahadhari kubwa ili kumpa Mungu heshima inayomstahili, kwa kila tendo na dhamira ya moyo iliyo safi.
Utaratibu huu ulikuwepo katika ibada ya Agano la kale na unapaswa kuendelezwa katika kanisa la leo.
(INyak 25:6-8, Zab 33:1-2)
Kila mwimbaji wa sifa na kwaya lazima ajue kwamba huduma hii iko moyoni mwa Mungu, maana yeye amezungukwa na viumbe pamoja na malaika milioni nyingi wanaomwabudu mchana na usiku

(Uf 5:7-14).
Hivyo ni vema kufanya huduma hii kwa kicho na kujitoa kwa dhati katika unyenyekevu wote, kwa bidii, na ustadi wa hali ya juu. Ni vibaya kufanya huduma hii kwa lengo binafsi, ama manufaa mengine mbali na kusudi la kumwadhimisha Mungu.
1.  ANGALIZO KWA MWANAKWAYA
Ni jambo la muhimu kwa mwanakwaya na muimbaji wa sifa aelewe kwamba, Mungu pekee ndiye anayestahili kupewa sifa na kuinuliwa katika huduma hiyo.
Muimbaji ajitambue kwamba ni chombo cha sifa kwa Bwana, kwa hiyo achunge sana kipawa hicho kisitumike kwa Bwana mwingine. Nasema hayo baada ya kuona waimbaji wengi walioinuka na kuwa juu, hawashikiki, hawaambiliki na kufunikwa na roho ya kiburi.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba, waimbaji wazuri waliotamba katika majukwaa ya injili kwa kipawa cha uimbaji, leo wako katika majukwaa ya shetani wakitumia kipawa hicho hicho kumsifu shetani.
Usisahau kwamba Mungu aliyekuita katika huduma siku moja atakutaka utoe hesabu ya utumishi wako, (2Wak 5:10.)
Simama na huduma mtu yeyote asikunyang’anye taji yako. Ukifahamu huduma hii ni huduma ya mbinguni, wewe ni mtu unayeheshimiwa sana na Bwana, maana Bwana anakaa katika SIFA. Jivunie heshima hii, jiendeleze, na kutumika bila masharti kwa utukufu wa Mungu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni