Jumanne, 22 Agosti 2017

IBADA NA UIMBAJI




“Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Mwimbieni BWANA, nchi yote.” (Zaburi 96.1)
“Mwimbieni BWANA wimbo mpya, Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umetenda wokovu.” (Zaburi 98:1)

Mungu anapenda uimbaji na anapenda kuimbiwa wimbo mpya kama tuonavyoona katika zaburi hizi,
-     Kwa asili yake yeye ni mpya kila siku hajawahi kuzeeka wala kuchakaa,
-     basi kwa asili hiyo hupenda vitu vipya, ni muhimu kuwa na nyimbo mpya na pambio mpya katika ibada zetu.
-     Ibada inayofanywa katika Roho na Kweli haiwezi kuendeshwa bila ya kumwimbia Mungu nyimbo za sifa na za kumwabudu.
-     Huu ndio utaratibu na mfumo wa ibada ya kiroho, kuanzia mbinguni mbele ya kiti cha enzi na katika Agano la kale na Agano jipya mpaka leo.
Asilimia sabini na tano ya shuguli za kanisa ni kuabudu, na asilimia tisini ya kuabudu ni uimbaji yaani kuimba. Nyimbo zinazoimbwa ziimbwe katika Roho na akili pia, zikielekezwa kwa Mungu, zikikoleza maombi na sala zetu,
-     zikiibua sifa za dhati toka moyoni nakunyosha misisimiko ya nafsi, fikra, mwili isipotoke kwenda nje ya ibada ya kweli,
-     kwa hiyo nyimbo zisiimbwe kwa lengo la burudani, bali ziimbwe kwa lengo la kumsifu Mungu, kumshangilia, kumshukuru, kufariji, kutia moyo, kumkaribisha Mungu, kusaidiana, kuonyana nakujengana na kuachilia neema ya Mungu iwafunike wanaomwabudu mahali hapo.
   Matokeo ya Ibada kama hii ni makubwa,
2Nyakati 5:11-14.

“Wakamfanyia Bwana ibada kuu, Bwana akaijaza nyumba utukufu, makuhani wakashindwa kufanya kazi zao maana Bwana ameshuka katikati yao na kuwabariki”.

-     Ibada inayoendeshwa bila uimbaji ni ibada bubu na haitaleta matokeo mazuri kwa waabuduo.
-     Kwa kuwa Mungu ni mpenzi wa uimbaji ndani ya ibada zetu, hivyo ni muhimu mno kuimba kwa sauti zilizopangiliwa vizuri ili tumbariki.

UIMBAJI NDANI YA IBADA

Ni vigumu kutenganisha uimbaji na ibada, uimbaji umetawala matendo ya mwanadamu kwa asilimia kubwa, kiasi kwamba uimbaji ni lugha inayomuwezesha mtu kujieleza alivyo,
-     ni kama chakula cha lishe chenye virutubisho vya aina zote kwa afya ya mwanadamu.
Uimbaji unagusa maeneo yote ya utu wa mtu na mahitaji ya mwanadamu, kiroho na kimwili. Uimbaji ni chakula kilicho bora kabisa kukidhi matamanio ya mtu mzima.
-     Mtu akiwa na huzuni, msiba, ataimba ili afarijike na kujiliwaza au ataimba ili aomboleze,
Katika sherehe umetawala, dhifa, mikutano ya aina zote ya kiroho na ile ya kisiasa, matambiko, kazi, hata katika vita, matangazo ya biashara, vyombo vya habari, matukio yote haya hutanguliwa na uimbaji na kumaliziwa na uimbaji.
-     Uimbaji huleta uponyaji wa Roho na mwili na huondoa mkandamizo na msongo wa mawazo.
-     Hii ndiyo nguvu iliyomo katika uimbaji. Ni vema basi kila mmoja wetu akaelewa uimbaji ni nini,
-     na unafanyikaje ili aweze kutumia katika kumwabudu Mungu wakati wa ibada.
-     Si jambo jema kuimba ovyo bila mpangilio ama bila kujua nakuelewa.
NYIMBO NA AINA YA IBADA
Kila ibada ni muhimu na ina malengo yake na madhumuni, ama makusudi ya kufanya ibada hiyo. Kwa hiyo ni lazima kila ibada ipewe nafasi katika nyimbo zinazoimbwa katika ibada hiyo.
-     Iwapo nyimbo zinazoimbwa haziendani na lengo, kusudi au madhumuni ya ibada, basi ibada hiyo imevurugika na watu watashindwa kuabudu kuelekea lengo la ibada hiyo.
-     Mwisho watu watachanganyikiwa na kuwa watazamaji na kuwaondoa kabisa katika ibada inayoendelea hapo Ingawa kimwili watakuepo.
Si vema kuimba wimbo wa maombolezo katika ibada ya arusi au wimbo wa pasaka katika ibada ya krismasi ama wimbo wa uinjilisti katika ibada ya meza ya Bwana.
-     IBADA si jambo la mzaha bali ni tendo la kumuabudu MUNGU,
-     Kwa hiyo ni lazima ufanyike upangaji na uchambuzi makini wa nyimbo zipi ziimbwe katika ibada ipi ili kukidhi hitaji la ibada husika
Ufuatao ni mchakato wa aina ya ibada.
Ibada ya kuabudu ziimbwe nyimbo za kuabudu,
-     Ibada ya SIFA, Ibada ya uinjilisti, Ibada ya maombi na kujitoa, Maisha ya Kikristo kwa ujumla wake.
Imbisha nyimbo zinazoendana na ibada hizo.
Nyimbo za Matukio. Hakikisha unaimba nyimbo zinzokwenda na matukio hayo.
Meza ya Bwana, Krismas, Pasaka, Arusi, Maziko na Maomboleza, Siku kuu, Mwaka mpya, Watoto, Mwaliko wa mtu kwa Yesu, Nyimbo za taarifa au ushuhuda wa matendo makuu ya Mungu, Utakaso na Kutia moyo na IMANI, Ujasiri, Mashambulizi kwa shetani au Vita ya kiroho, Roho Mtakatifu na nyimbo zenye ujumbe maalum kwa matukio maalum kama vile, uzinduzi wa nyumba ya IBADA, au jambo lolote linalogusa kanisa au jamii.

Ni muhimu kuimba nyimbo zinazogusa ujumbe wa matukio hayo. Huu ni mwongozo wa jinsi ya kuendesha ibada na uimbaji utakaoleta Baraka na kutufikisha katika kusudi la ibada husika.
Uimbaji ni somo pana lenye kuwa na mielekeo tofauti tofauti kulingana na matumizi ya mtu anavyotaka.
-     Ingawa kanuni za muziki (uimbaji) ni zilezile kwa kila mwelekeo.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni