Jumapili, 20 Agosti 2017

KWA NINI TUNAMSIFU MUNGU

































“Maana mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo, na miti yote ya kondeni itapiga makofi”.   (Isaya 55:12)

Wakati wa ibada ni wakati wa kilele cha furaha ya mwanadamu ibada na kuabudu ni kumshangaa Mungu ambaye ni Mfalme wa ajabu milele. (Yohana 4:23-24) Baba anamtafuta mtu atakayemwabudu katika roho na kweli ifahamu misingi ya sifa, ibada na kuabudu katika roho na kweli kama biblia ifundishavyo.
Mara nyingi katika makanisa yetu tunakuwa na ratiba ambayo imebana sana, kwa hiyo hutoa muda mfupi sana katika kusifu na kumuabudu Mungu katika roho na kweli hivyo kulifanya kanisa kuwa katika hatua ya kwanza yaani mwilini wakati muhubiri anapanda katika madhabahu kutoa ujumbe wa Mungu. Matokeo yake ni sawa na kupanda mbegu katika miiba au kwenye udongo usiofaa kupandwa mbegu kwa sababu ya kutoandaliwa vema na wahusika. Hivyo inahitajika weledi wa hali ya juu na mafunzo kwa kanisa zima ili kuutumia muda huo mdogo kwa faida kubwa
kulingana na somo nililofundisha la HEMA YA KUKUTANA NA MUNGU. Ambalo linafundisha hatua tatu muhimu za kumwendea Mungu, ambapo hatua ya kwanza kanisa linapoanza ibada huwa katika mwili. Baadae huenda kwenye nafsi na hatua ya mwisho hufika rohoni kabla ya mhubiri kupanda kwa ajili ya kutoa ujumbe wa Mungu. Katika kitabu hiki tunakwenda kuangalia kwa undani zaidi mambo mbalimbali yanayohusu kumsifu Mungu na kumuabudu katika Roho na kweli, maana Mungu anawatafuta watu kama hao. Mungu akubariki sana wakati unaendelea kupata siri za ufalme wa Mungu kupitia katika kitabu hiki.
Kusifu na kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni jukumu kuu la wakati wote katika maisha yetu binafsi na katika makanisa yetu, hii ni kwa sababu Mungu alituumba sisi kwa ajili yake mwenyewe. Anasema

“Watu wale niliojiumbia nafsi yangu ili watangaze sifa zangu”. (Isaya 43: 21)

Hii inatuthibitishia kwamba, kumbe tuliumbwa na Mungu kwa kusudi moja tu, la kumsifu na kumuabudu. Ili siku zote hisia zetu zimwelekee yeye, Mungu Baba yetu na tutangaze sifa zake Mungu muumbaji wetu. Biblia inasema, 

“Bali ninyi ni mzao mteule ukuhani wa kifalme, taifa takatifu watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:9.)

Kusifu.
Kabla ya maelezo juu ya kuabudu, ni vizuri kwanza tugusie japo kidogo juu ya kusifu ni nini? Kwa sababu ukiangalia kwa makini, kusifu na kuabudu ni vitu viwili tofauti, ingawa vinaenda pamoja.
-     Kwa kawaida unaweza kuwa na ibada ya sifa bila kuabudu, na inaweza ikawa nzuri tu.
Lakini siyo rahisi kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu.
Ni mara chache kutokea kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu. Hii hutokea tu pale mtu anapovamiwa na mguso wa Roho Mtakatifu wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida.

Kusifu kwa vyovyote vile iwavyo, huwa ni tendo la kutangaza kwa nguvu, na kwa uwazi tena hadharani. Ukielezea na kuonyesha uhakika ulionao juu ya unachokitolea sifa.

Kwa maana hiyo, popote panapokusudiwa kuwa pawepo na sifa, kuna hekaheka na matendo, sauti na nyimbo, vyote huonekana na kusikika.

Kusifu ni utaratibu unaopangwa na ufahamu wako jinsi gani udhamirie kusifia, sio kulazimishwa na mtu kama tuko kwenye gwaride, kuna ule mtindo ambao viongozi wa sifa huutumia, mara bariki kushoto, bariki kulia, bariki mchungaji, bariki wanakwaya! Hayo ni mambo ya stage show katika ibada haiko hivyo. Ingawa unaweza kufanya hivyo mwanzo kabisa katika kuhamasisha, lakini baada ya hapo waachie watu wapambane wenyewe kuingia  barazani pa Mungu.

Mara nyingi nimeongea na viongozi wa sifa sehemu mbalimbali tunapokutana kwamba, sio wajibu wao kuwaambia watu hebu simameni ili tumsifu Mungu.  Inatakiwa mtu mwenyewe aguswe toka ndani, yaani mtu wa ndani ndio anatakiwa amuamulie mtu wa nje (mwili) kufanya vile mtu wa ndani anavyotaka.

Ukienda mahali ambako sifa zinafanyika kwa uhakika utashangaa! Utaona wengine wamelala chini, wengine wananesanesa, wengine wanarukaruka, wengine wanapiga ukuta kwa ngumi ili mradi ni hekaheka, na hakuna mtu mwenye habari za kushangaa shangaa. Sasa kiongozi wa sifa, kwa mfano unapowaambia watu wasimame! Kwani nani alikwambia kwamba kusimama ndio tafsiri ya heshima? Ingawa ni kweli kwa jadi zetu tunaamini kwamba kusimama ni dalili ya heshima. Kwa wengine kitendo cha kusimama ni dharau. Kina mama wa makabila fulani wanapotaka kukusalimia kwa heshima wanakaa chini, au wanapiga magoti.
-     Mama wa aina hiyo binti yake akisalimia watu kwa kusimama, anamuona hana heshima hiyo ni anadharau kabisa.
Makabila mengine ya kusini mwa Tanzania kama wangoni akikuheshimu au akitaka kukushukuru kwa kiwango cha juu analala chini kabisa.
-     Kwa hiyo ndio maana ninashauri kuwa ni vema viongozi wa ibada na viongozi wa sifa, kutokuwaamulia watu nini cha kufanya kulingana tafsiri zao za mila ya kwao.


Kusifu ni njia ya lango kuu la kuingilia katika kiini cha kuabudu. Hivyo kusifu ni ibada yenye umuhimu wa kipekee kwa Mungu wetu, kikundi cha sifa ni askari wa mstari wa mbele na ndio wanaotengeneza njia ya muhubiri kupitisha neno la Mungu katika mioyo ya watu ambayo tayari imeshalainishwa na sifa. Zaburi 22:3.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni