Jumapili, 20 Agosti 2017

WAIMBAJI WANAPOKOSA MAADILI



Kabla sijawekewa mikono kuwa kiongozi wa waimbaji wa jiji la Tanga, kiongozi wangu mwenyekiti wa chama cha muziki wa injili kanda ya kaskazini, alinichukua ili kunitambulisha kwa baadhi ya maaskofu wa kipentekoste waliokuwepo Tanga. Nakumbuka askofu mmoja alitueleza sababu za kutuunga mkono ni kwamba waimbaji wanaojitegemea wengi wao wamekuwa na maadili mabou sana na wanashindwa kuwashauri kwa sababu hakuna chombo kinachoweza kuwaunganisha kati yao na viongozi wa dini, akatueleza jinsi ambavyo yeye mwenyewe alivyomdhamini mwimbaji mmoja dola 3,000$ ambazo huyo mwimbaji alitaka zitumwe kwenye akaunti yake, pesa akapokea na kwenye mkutano huo hakwenda na pesa hizo hakurudisha. Hali hii ilimtia aibu sana kwa wageni wake ambao walikuwa sio waswahili.
Huu ni mmoja kati ya mambo mengi ya aibu ambayo yanafanywa na wale wanaojiita waimbaji wakubwa. Lakini katika hotuba yangu baada ya kuapishwa, niligusia kidogo hili jambo kwa kuwaeleza wakuu wadini, kwamba hawa waimbaji wengi wao vipaji vyao huanza kuonekana kanisa, na huwa tunawakuza na kuvilea vipaji vyao toka kanisani, wanakuwa chini ya malezi ya idara za vijana baadae wanaingia kwenye kwaya ambazo zipo kanisani. Wakiwa hapo wanakuwa chini ya uangalizi wa jicho kali la mchungaji, wazee wa kanisa na walimu wa kwaya, katika ngazi hii kuna mafunzo wanayopewa katika kukuza kipaji chake na maadili ya kanisa.
Shida inakuwa ni pale anapotaka kwenda mbele zaidi yaani nje ya uwigo wa kanisa kama jengo la pahali. Mara nyingi wachungaji huwa hawakubali wakiamini kwamba ni matunda yao na ni lazima atumike kanisani hapo. Matokeo yake mwimbaji huyo huanza kufanya ukaidi na kuondoka wakati mwingine bila ya kuaga. Matokeo yake anakosa baraka na kuyumba kimwelekeo. Katika eneo hili ni wachungaji wachache sana wanaoagana na waimbaji wao kwa kuwapa mkono wa baraka. Na hii ni muhimu pia kukumbuka kwamba waimbaji wetu nao wana ndoto zao katika maisha ya uimbaji na lazima ziheshimiwe katika kupunguza migogoro na kuua vipaji ya waimbaji, hilo ni lazima wachungaji walitambue na ikiwezekana wapate nafasi ya kuongea na waimbaji mmoja mmoja, ili kujua maono yake, na ni lazima kumsaidia kwa hali na mali katika kufikia lengo lake, kama na yeye anavyojitoa katika kusukuma huduma ya kanisa, hapo ndipo litakuwa chimbuko la kuwa na waimbaji wakubwa ambao bado wana mahusiano mazuri na Mungu na wachungaji wao pia. Kanisa ni zaidi ya jengo la mahali fulani ni lazima tutengeneze uwigo mpana kuhakikisha kwamba vipaji vilivyoko kanisa vinaweza kuhudumia taifa na dunia kwa ujumla.
wakati huu tunaona waimbaji waliokuwa ni mtumishi wa Mungu kwa huduma ya uimbaji katika sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Huduma zao zilipata mpenyo mkubwa sana sehemu mbalimbali mpaka wakaota pembe,

Kutokana na umahili wao katika uimbaji walipata umaarufu ndani na nje ya Kanisa na kupelekea viongozi wa kisiasa kuwaomba wawasaidie kwenye kampeni za kisiasa za vyama vyao ili wawasaidie kushinda katika chaguzi mbalimbali za uwakilishi wa kisiasa. Nao kwa tamaa walikubaliana na ombi hilo, bila kuwaambia viongozi hao wa kisiasa kwamba wito watu ni kumwimbia Mungu tu na si vinginevyo. Ni kweli kila mtu anatamani kupata pesa lakini Yesu anauliza Itakufaa nini ukiupata ulimwengu wote?
maana sijajua kwa undani mafanikio waliyoyapata kwa kuwa waimbaji wa nyimbo za kampeni za siasa kuliko faida watakazopata kwa kumtumikia Mungu wao.
-       Mwimbaji ni chombo kitakatifu cha Bwana, Mfalme Daudi alifahamu vyema jambo hilo akachukua hatua ya kuwaweka WAIMBAJI WAKFU MADHABAHUNI pa Bwana kuonesha kwamba wametengwa rasmi kwa huduma hiyo.

Ikumbukwe kwamba Mungu hakukubaliana na mfalme Belishaza alipovitumia vyombo vitakatifu vilivyotwaliwa kutoka Hekalu la Yerusalemu na baba yake Nebukadreza.
Hebu angalia Mungu alivyochukizwa na jambo hilo.
 “Na wewe mwanawe, Ee Belishaza hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote, Bali umejiinua juu ya Bwana wa Mbingu nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako na wewe, na wakuu wako na wake zako na masuria wako mmevinywea nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba na ya chuma na mti na ya mawe wasioona wala kusikia wala kujua neno lolote, na Mungu yule ambae pumzi yako ii mkononi mwake, na njia zako zote ni zake hukumtukuza. Ndipo kile kitangaa cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake na maandiko haya yameandikwa, MENE MENE,TEKELI NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii, MENE. Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha, TEKELI, Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka, PERESI Ufalme wako umegawanyika nao wamepewa Waamedi na Waajemi. Danieli 5.22—28
-     Haya ni maonyo makali kwa mtu ambaye anakitumia chombo cha Mungu kinyume na matumizi yake, hivyo hivyo Mungu hayuko tayari kuona vipawa alivyotupa vinatumika hovyo, mbali na kusudi la huduma hii.
Maana mafuta tuliopewa sio ya kisiasa wala ya kuburudisha watu ni kwa ajili ya Mungu. Ni muhimu kuwa na unyenyekevu na heshima na kujiepusha na kitu chochote kinachokuondoa katika utumishi wako kwa Mungu. Linda sana ulicho nacho na wito wako mtu asikunyanganye.
-     Mambo yaliyompata mfalme Belishaza baada ya kuvitumia vyombo vya Bwana vibaya katika msitari wa 30 unasema, usiku huo huo akafa.

Hii ni hatari inayomkabili mtumishi yeyote anayekiuka kutumia vibaya kipawa na karama aliopewa na Bwana. Kwa hiyo kila mwimbaji wa sifa ambaye amepakwa mafuta na Mungu ni chombo cha Bwana hapaswi kutumia kipawa chake nje ya huduma ya Mungu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni