Jumatatu, 29 Februari 2016

KWA NINI TUNAMSIFU MUNGU





Kusifu na kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni jukumu kuu la wakati wote katika maisha yetu binafsi na katika makanisa yetu, hii ni kwa sababu Mungu alituumba sisi kwa ajili yake mwenyewe. Anasema

“Watu wale niliojiumbia nafsi yangu ili watangaze sifa zangu”. (Isaya 43: 21)

Hii inatuthibitishia kwamba, kumbe tuliumbwa na Mungu kwa kusudi moja tu, la kumsifu na kumuabudu. Ili siku zote hisia zetu zimwelekee yeye, Mungu Baba yetu na tutangaze sifa zake Mungu muumbaji wetu. Biblia inasema, 

“Bali ninyi ni mzao mteule ukuhani wa kifalme, taifa takatifu watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:9.)


Kusifu.
Kabla ya maelezo juu ya kuabudu, ni vizuri kwanza tugusie japo kidogo juu ya kusifu ni nini? Kwa sababu ukiangalia kwa makini, kusifu na kuabudu ni vitu viwili tofauti, ingawa vinaenda pamoja.
-     Kwa kawaida unaweza kuwa na ibada ya sifa bila kuabudu, na inaweza ikawa nzuri tu.
-     Lakini siyo rahisi kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu.
Ni mara chache kutokea kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu, hii hutokea tu pale mtu anapovamiwa na mguso wa Roho Mtakatifu wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida.

Kusifu kwa vyovyote vile iwavyo, huwa ni tendo la kutangaza kwa nguvu, na kwa uwazi tena hadharani. Ukielezea na kuonyesha uhakika ulionao juu ya unachokitolea sifa.

Kwa maana hiyo, popote panapokusudiwa kuwa pawepo na sifa, kuna hekaheka na matendo, sauti na nyimbo, vyote huonekana na kusikika.

-     Kusifu ni utaratibu unaopangwa na ufahamu wako jinsi gani udhamirie kusifia, sio kulazimishwa na mtu kama tuko kwenye gwaride, kuna ule mtindo ambao viongozi wa sifa huutumia, mara bariki kushoto, bariki kulia, bariki mchungaji, bariki wanakwaya! Hayo ni mambo ya stage show katika ibada haiko hivyo. Ingawa unaweza kufanya hivyo mwanzo kabisa katika kuhamasisha, lakini baada ya hapo waachie watu wapambane wenyewe kuingia  barazani pa Mungu.

Mara nyingi nimeongea na viongozi wa sifa sehemu mbalimbali tunapokutana kwamba, sio wajibu wao kuwaambia watu hebu simameni ili tumsifu Mungu.

-     Inatakiwa mtu mwenyewe aguswe toka ndani, yaani mtu wa ndani ndio anatakiwa amuamulie mtu wa nje (mwili) kufanya vile mtu wa ndani anavyotaka.

Ukienda mahali ambako sifa zinafanyika kwa uhakika utashangaa! Utaona wengine wamelala chini, wengine wananesanesa, wengine wanarukaruka, wengine wanapiga ukuta kwa ngumi ili mradi ni hekaheka, na hakuna mtu mwenye habari za kushangaa shangaa.

Sasa kiongozi wa sifa, kwa mfano unapowaambia watu wasimame! Kwani nani alikwambia kwamba kusimama ndio tafsiri ya heshima? Ingawa ni kweli kwa jadi zetu tunaamini kwamba kusimama ni dalili ya heshima.
-     Kwa wengine kitendo cha kusimama ni dharau. Kina mama wa makabila fulani wanapotaka kukusalimia kwa heshima wanakaa chini, au wanapiga magoti.
-     Mama wa aina hiyo binti yake akisalimia watu kwa kusimama, anamuona hana heshima hiyo ni anadharau kabisa.
Makabila mengine ya kusini mwa Tanzania kama wangoni akikuheshimu au akitaka kukushukuru kwa kiwango cha juu analala chini kabisa.
-     Kwa hiyo ndio maana ninashauri kuwa ni vema viongozi wa ibada na viongozi wa sifa, kutokuwaamulia watu nini cha kufanya kulingana tafsiri zao za mila ya kwao.


Kusifu ni njia ya lango kuu la kuingilia katika kiini cha kuabudu. Hivyo kusifu ni ibada yenye umuhimu wa kipekee kwa Mungu wetu, kikundi cha sifa ni askari wa mstari wa mbele na ndio wanaotengeneza njia ya muhubiri kupitisha neno la Mungu katika mioyo ya watu ambayo tayari imeshalainishwa na sifa. Zaburi 22:3.







IBADA MAALUM






Yesu alitoa ibada maalum mbili tu kwa kanisa: 
                 ubatizo wa maji (ona Mathayo 28:19) na 
                 Meza ya Bwana (ona 1Wakor. 11:23-26). 

Tujifunze kuhusu ubatizo wa maji kwanza.

Katika agano jipya, kila aaminiye anapaswa kubatizwa mara tatu tofauti, kama ifuatavyo: ubatizo wa kuingia katika mwili wa Kristo; ubatizo wa maji, na ubatizo wa Roho Mtakatifu.


Mtu anapozaliwa mara ya pili, anabatizwa ili kuingia katika mwili wa Kristo. Yaani, anafanyika kiungo katika mwili wa Kristo ambao ni kanisa. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja (1Wakor. 12:13. Ona pia Warumi 6:3; Waefeso 1:22, 23; Wakolosai 1:18, 24).

Kubatizwa katika Roho Mtakatifu ni kitu kinachofuata wokovu, na ubatizo huu ni kwa ajili ya kila aaminiye.
Mwisho – kila mwamini anapaswa kubatizwa katika maji mara tu inapowezekana, baada ya kutubu na kumwamini Bwana Yesu. 

Ubatizo unapaswa kuwa tendo la kwanza la utii katika maisha ya mwamini mpya.


[Yesu] Akawaambia, Enendeni ulimwengu mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa (Marko 16:15, 16. Maneno mepesi kukazia).


Kanisa la kwanza lilihesabu amri ya Yesu kuhusu kubatiza kuwa ya muhimu sana. Karibu kila mara, waamini wapya walibatizwa mara moja baada ya kuokoka kwao (ona Matendo 2:37-41; 8:12-16; 36-39; 9:17-19; 10:44-48; 16:31-33; 18:5-8; 19:1-5).




Mawazo Kinyume Cha Biblia Kuhusu Ubatizo

Kuna wanaobatiza kwa kumnyunyuzia mwamini mpya matone kidogo tu ya maji. Je, ni sahihi? 

batiza katika Agano Jipya linatokana na neno la Kiyunani baptize, ambalo maana yake halisi ni “kufunika kwa maji, kuzamisha.” Basi, wale wanaobatizwa kw amaji wanatakiwa kuzamishwa ndani ya mani, si kudondoshewa matone machache tu. Maana ya ubatizo wa Kikristo ambayo tutajifunza punde tu, inaunga mkono pia wazo la kuzamishwa katika maji.

Kuna wengine wanaobatiza watoto wachanga. Hakuna mifano ya maandiko kuhusu kubatizwa kwa watoto katika Biblia. Desturi hiyo inatokana na mafundisho ya uongo kuhusu “ubatizo kuokoa” – wazo kwamba mtu huzaliwa mara ya pili anapobatizwa. 

yanafundisha wazi kabisa kwamba watu wanapaswa kumwamini Yesu kwanza kabla ya kubatizwa. Hivyo, watoto wakubwa kidogo, na wenye uwezo wa kutubu na kumfuata Yesu wanastahili kubatizwa – si watoto wachanga au hata wadogo.


Kuna wanaofundisha kwamba, ingawa mtu anaweza kumwamini Yesu, hajaokoka mpaka abatizwe. Kulingana na Maandiko, hiyo si kweli. Katika Matendo 10:44-48 na 11:17, tunasoma kwamba watu wa nyumbani mwake Kornelio waliokolewa na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu kabla hawajabatizwa katika maji. Ni kwamba haiwezekani yeyote abatizwe kwa Roho Mtakatifu kama hajaokoka kwanza (ona Yohana 14:17).


Kuna wanaofundisha kwamba kama mtu asipobatizwa kulingana na utaratibu wao, hajaokoka. Maandiko hayatoi utaratibu fulani kiibada ambao unapaswa kufuatwa, ili uwe ubatizo sahihi au halali. Kwa mfano: 

Kuna wanaosema mwamini anatakiwa kubatizwa “katika jina la Yesu” (Matendo 8:16). Wanadai kwamba mtu akibatizwa “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19) hajaokoka. 

Watu hao wanaonyesha roho ile ile ambayo iliwatawala Mafarisayo – wanachuja mbu na kumeza ngamia. Ni huzuni ilioje kwamba Wakristo wanahojiana kuhusu maneno yanayofaa kusemwa wakati wa ubatizo, huku dunia inasubiri kusikiliza Injili.


Maana Ya Ubatizo Kimaandiko

Ubatizo wa maji ni mfano wa vitu vingi ambavyo vinakuwa vimekwisha tokea katika maisha ya mwamini. Kimsingi, ni mfano kwamba tumesafishwa dhambi zetu, na sasa tunasimama mbele za Mungu tukiwa safi. Wakati Anania alipotumwa kwa Sauli (au Paulo) mara tu alipo-okoka, alimwambia hivi:


Basi sasa, unakawilia nini? Simama ubatizwe, ukaoshwe dhambi zako, ukiliitia jina lake (Matendo 22:16. Maneno mepesi kukazia).

Pili – Ubatizo wa maji ni mfano wa sisi kujitambulisha na Kristo katika kufa Kwake, kuzikwa na kufufuka. Tukiisha zaliwa mara ya pili na kuwekwa katika mwili wa Kristo, tunaanza kuhesabiwa kuwa “katika Kristo” tangu wakati huo na kuendelea. Kwa sababu Yesu alituwakilisha, Mungu anatuhesabia yote aliyofanya Yesu. 

Basi, “katika Kristo” tumekufa, tumezikwa na tumefufuliwa ili kuishi kama watu wapya kabisa.

Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti Yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima (Warumi 6:3, 4).


Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu (Wakolosai 2:12).

Kila mwamini mpya anapaswa kufundishwa kweli hizi muhimu sana wakati anapobatizwa kwa maji, naye anapaswa kubatizwa mara moja baada ya kumwamini Yesu.






Meza Ya Bwana

Meza ya Bwana asili yake ni katika Sikukuu ya Pasaka ya Agano la Kale. Usiku ule Mungu alipowakomboa Israeli kutoka utumwani Misri, aliagiza kila nyumba kuchinja mwana-kondoo wa umri wa mwaka mmoja na kuinyunyiza damu yake kwenye miimo ya milango ya nyumba zao. Wakati “malaika wa kifo” alipopita katika taifa hilo usiku ule, akiua wazaliwa wa kwanza wote katika Misri, angeiona damu kwenye nyumba za Waisraeli, na “kupita juu yake.”

Tena, Waisraeli walitakiwa kusherehekea sikukuu usiku huo kwa kumla mwanakondoo wao wa Pasaka na pia kwa kula mkate usiotiwa chachu kwa siku saba. Hili lilikuwa agizo la kudumu kwa Waisraeli, na ni kitu cha kufanyika kila mwaka wakati huo huo (ona Kutoka 12:1-28). Ni dhahiri kwamba mwana-kondoo wa Pasaka alikuwa mfano wa Kristo, anayeitwa “Pasaka wetu” katika 1Wakoirntho 5:7.

Wakati Yesu alipoanzisha Meza ya Bwana, Yeye na wanafunzi Wake walikuwa kwenye Sherehe ya Pasaka. Yesu alisulubiwa wakati wa Pasaka, na kwa njia hiyo kutimiza kikamilifu wito Wake kama “Mwanakondoo wa Mungu, azichukuaye dhambi za dunia” (Yohana 1:29).

Ule mkate tunaokula na maji ya matunda tunayokunywa ni mfano wa mwili wa Yesu, uliovunjwa kwa ajili yetu, na damu yake, iliyomwagika kwa ajili ya ondoleo la dhambi zetu.

Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake akasema, Twaeni mle, huu ndio mwili wangu. Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu (Mathayo 26:26-29).

Mtume Paulo anasimulia kisa hicho hicho kwa njia tofauti, kama ifuatavyo:

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa, Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo (1Wakor. 11:23-26).

Lini, Namna Gani? 


Maandiko hayasemi tushiriki Meza ya Bwana mara kwa mara kiasi gani, lakini ni dhahiri kwamba katika Kanisa la Kwanza ilifanyika mara kwa mara katika mikutano ya makanisa ya nyumbani, kama mlo kamili (ona 1Wakor. 11:20-34). Kuwa kuwa Meza ya Bwana asili yake ni katika Mlo wa Pasaka, ilikuwa ni mlo kamili ilipoanzishwa na Kristo, na ilikuwa sehemu ya chakula kamili katika kanisa la kwanza. Hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa hata siku hizi. 

Kwa sehemu kubwa, makanisa mengi yanafuata “mapokeo ya wanadamu.”

Tunapaswa kuikaribia Meza ya Bwana kwa kicho na heshima. Mtume Paulo alifundisha kwamba ilikuwa kosa kubwa kushiriki Meza ya Bwana kwa jinsi isivyostahili.


Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate na kukinywea kikombe.

Maana alaye na kunywa hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia (1Wakor. 11:27-32).

Tunashauriwa kujichunguza na kujihukumu wenyewe kabla ya kushiriki Meza ya Bwana, na tukigundua dhambi yoyote ile, tunahitaji kuungama na kuitubu. Vinginevyo, tunaweza kuwa “na hatia ya mwili na damu ya Bwana.”

Kwa sababu Yesu alikufa na kumwaga damu yake ili kutuweka huru kutokana na dhambi, kwa kweli hatutaki kushiriki Meza yenye vitu vinavyowakilisha mwili na damu Yake, tukiwa na dhambi yoyote ile tunayoijua, isiyotubiwa. Tukifanya hivyo, tunaweza kula na kunywa hukumu juu yetu wenyewe katika ugonjwa na hata kifo kabla ya wakati, kama ilivyokuwa kwa Wakristo Wakorintho. Njia ya kuepukana na adhabu ya Mungu ni “kujihukumu wenyewe” – yaani, kukiri na kutubu dhambi zetu.

Dhambi kuu ya Wakristo Wakorintho ilikuwa kutokuwa na upendo.
Walikuwa wanagombana wao kwa wao. Ukweli ni kwamba, kutokujaliana kwao kulijidhihirisha hata wakati wa Meza ya Bwana, wakati wengine walikula chakula na wengine wanakaa na njaa, na wengine hata walikuwa wanalewa (1Wakor. 11:20-22).

Mkate tunaokula ni mfano wa mwili wa Kristo, ambao sasa ndiyo kanisa. 



Tunashiriki mkate mmoja, ambao ni mfano wa umoja wetu kama mwili mmoja (ona 1Wakor. 10:17). Ni kosa kubwa sana kushiriki kinachowakilisha mwili mmoja wa Kristo huku tuko katika mapigano na ugomvi na kutokuwa na ushirikiano na viungo wengine wa mwili huo! Kabla hatujashiriki Meza ya Bwana, tunahitaji kuhakikisha kwamba tuko katika mahusiano yaliyo sawa na ndugu zetu na dada zetu katika Kristo.