Jumanne, 10 Mei 2016

NGUVU YA MUNGU ILIYO NDANI YETU SEHEMU YA KWANZA



NGUVU YA MUNGU ILIYO NDANI YETU
SEHEMU YA KWANZA
Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.
(Waebrania 11:3)

Biblia inatuonyesha kwamba hapo zamani Mungu alikuwepo peke yake na mahali fulani, harafu baadae aliviumba vitu vyote hivi tunavyoviona na na vile visivyoonekana.

Wakati Mungu anaiumba hii dunia hapakuwa na mahali alipokwenda kuchukua malighafi zilizotumika kuiumba  hii dunia kama vile udongo, mchanga, kokoto, mawe n.k. ili aje aiumbe hii dunia.

Siku hizi watu wanashindana kujenga majumba ya ghorofa marefu na makubwa sana yenye kutisha, lakini wakati wanajenga inabidi walete udongo, mawe, kokoto mchanga, nondo n.k. ndipo wajenge.

lakini wakati Mungu anaiumba hii dunia hapakuwa na kitu chochote ambacho Mungu angeenda kukichukua ili kimsaidie
Mungu alikuwa anasema neno lake tu na baada ya kusema kile alichosema kilitokea.

hebu anagalia Biblia mwanzo sura ya kwanza wakati wa uumbaji utaona ni namna gani Mungu aliiumba hii dunia utaona kuwa Mungu alisema neno tu, kwa mfano Biblia inasema;
Mungu akasema iwe nuru ikawa nuru” (Mwanzo 1:3)
Mungu akasema liwe anga likawa anga n.k.

Mifano ni mingi sana inayoonesha jinsi Mungu alivyoiumba hii dunia na vitu vyote vilivyomo kwa kutumia neno lake. Kilichofanyika ni kwamba Mungu alikuwa anasema neno na mara tu baada ya kusema kitu hicho kinatokea hii ni sawa na neno la Mungu katika injili ya Yohana 1.1- 4  
hapo mwanzo kulikuwako neno, naye neno alikuwa kwa Mungu, naye neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuweko kwa Mungu, vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima,nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.

hapa tunaona tena kuwa ndani ya neno kulikuwamo uzima, neno analolisema Mungu ndani yake umo uweza, ndani yake kuna nguvu ya uumbaji.

Mungu anaposema neno, ile nguvu ya uumbaji ya kiungu inatoka katika lile neno na kwenda kukitengeneza kile kitu ambacho kimetamkwa, hii ndio maana Mungu alikua anasema neno wakati anaumba, na si wakati anaumba tu bali katika utendaji wowote wa Mungu hutenda kwa kusema  neno tu

Mungu alipomtuma Yesu hapa duniani aje kufanya kazi yake
pamoja na kazi ya kuhubiri na kufundisha neno la Mungu, Yesu alikuwa anaponya wagonjwa na kuwafungua watu wenye shida mbalimbali.

Yesu alizifanya kazi hizi zote kwa kutumia neno lake peke yake,  Yesu hakutumia nguvu ya mwili au elimu ya dunia kuwaponya wagonjwa. Unajua katika elimu ya dunia wagonjwa  wengine kwa ingebidi wafanyiwe upasuaji, pengine mama ameshindwa kujifungua au pengine mtu amevunjika mifupa n.k.   


wagonjwa wengine ingebidi wachomwe sindano na wengine wanywe vidonge n.k. lakini tunaona Yesu alikuwa anasema neno lake tu wale wagonjwa wanapona  hapohapo.
Mungu alipomtuma Yesu hapa duniani aliweka nguvu yake ya uumbaji ndani yake na  ni nguvu ileile aliyoitumia wakati anaiumba dunia hii bila kupungua hata chembe moja ndio na ndio hiyohiyo aliyoiweka ndani ya Yesu.

Wachunguzi wa Biblia wanatuhabarisha kwamba Yesu kimwili alionekana kama amedhoofu sana. Hakuwa pandikizi la mtu alionekana amekonda sana katika hali ya kimwili watu wasingemtumaini kwa lolote. Na hii ni kwa sababu muda mwingi alikuwa hali chakula na ushahidi unaonekana katika matukio mengi tu.

Mfano alipofika kwa Martha na Mariamu alikataa wasishughulike na mambo ya kupika chakula alitaka wasikilize kwanza neno la Mungu, tunaweza kuona pia hata katika kisima cha Yakobo, ulikuwa ni wakati wa chakula cha mchana. Aliwaruhusu wanafunzi wake waende kula chakula yeye alibaki pale akimhubiri Yule mama wa kisamaria neno la Mungu.

Nabii Isaya anatuambia ”Yeye hana umbo wala uzuri; na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko” (Isaya 53: 2)

Pamoja na kuonekana kimwili kuwa amedhoofu, lakini lijua kuwa ndani yake kuna uweza wa Mungu ambao iwapo atasema neno ile nguvu itatoka na kwenda kufanya kile alichokisema.

Kuna sehemu tunaona akiwa na wanafunzi wake akasema tuvuke twende ng’ambo hapa walipanda kwenye jahazi lakini wakiwa katikati ya bahari upepo mkali wenye dhoruba ukaja ukataka kuwazamisha baharini.
Lakini kama unavyojua kwamba baadhi ya mitume walikuwa ni wavuvi wa samaki, kwa hiyo walikuwa wanajua sana mambo ya ubaharia na hivyo walijua mbinu ya kufanya inapotokea hali kama iliyotokea.

Lakini baada ya upepo huo mbaya kuja mitume wenye ujuzi wa mambo ya baharini walijitahidi sana kufanya kila linalowezekana lakini baadae mbinu zao zote zilishindikana, wakati wote huo Yesu alikuwa amelala wakamuamsha.

Wanafunzi wa Yesu walikuwa wameshamuona Yesu akifanya miujiza mingi sana kama vile kuponya wagonjwa, kutengeneza mikate kufufua wafu, kutoa mapepo n.k.

wanafunzi wa Yesu walikuwa hawajamuona Yesu akikemea upepo na ukatii, siku hiyo Yesu alikuwa amelala wale wanafunzi baada ya dhoruba kutokea  hawakuhitaji kumuamsha mapema kwa sababu walijua hatawasaidia kwa lolote, lakini kwamba upepo pia unaweza kumtii, wao walijua kuwa Yesu anawea kuponya na kutengeneza mikate tu.

Lakini kuhusiana na upepo hawakujua kuwa ana uwezo wa kuutuliza ndio maana hawakumuamsha mapema, unajua kwamba wavuvi wa samaki huwa ni watu wenye nguvu sana kwa sababu ile pia ni kazi ya suluba ambayo inahitaji mtu kula vizuri.

Ni mapande ya baba, ni watu wenye mazoezi ya nguvu kwa sababu moja ya shughuli zile wanazozifanya za kupiga makasia na kuvuta jerife, hivyo hao watu  wenye miraba minne na ujuzi wa baharini.


baada ya kuwa wamekwama kabisa ndipo walipoamua kumuamsha Bwana Yesu, ambaye sio bonge la mtu na ambaye hana nguvu na anaonekana amedhoofu kiasi hata hawezi kupiga makasia, ni wazi kuwa wale wanafunzi wapomwamsha hawakumwamsha kwamba wanategemea wokovu fulani kutoka kwake, bali walikuwa wanamjulisha aone jinsi wanavyoangamia

Naye mwenyewe alikuwepo katika shetri amelala juu ya mto;  wakamwamsha wakamwambia, mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia, (Marko 4.38)

Yesu alipoamka yeye hakuwa na hofu wala hakuanza kuuliza maswali na kujitetea kuwa yeye hana ujuzi wa bahari au  kujiuliza maswali ya kwa nini wale wenye miraba minne wameshindwa je yeye ataweza.

Yesu alijua alichokuwa nacho ndani yake na kwamba yeye alichotakiwa ni kusema neno tu akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari nyamaza utulie! upepo ukakoma kukawa shwari kuu. Akawaambia mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado? (Marko 4.39)

mitume waishangaa sana kuona kuwa upepo na bahari vimemtii Yesu Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana ni nani huyu, basi, hata upepo wa bahari humtii? (Marko 4:41.

Yesu alipokutana na mtu ambaye ana ulemavu wa macho (kipofu) mfano wa Bartimayo Yesu hakuhitaji kuwa na vifaa vya upasuaji ili aweze kufanya oparesheni ya jicho ,alichofanya ni kumuuliza unataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia Mwalimu wangu nataka nipate kuona tena Yesu akamwambia enenda zako imani yako imekuponya. Mara akapata tena kuona  (Marko 10: 46 – 52)
Yesu aliposema Yule mtu alipona dakika ileile. Hali kadhalika alipokutana na mama ambaye ana ulemavu wa mkono yesu hakuhitaji kufanya upasuaji wa kuinyoosha na kuipanga mifupa yake. Akamwambia Yule mama nyosha mkono wako, naye akaunyoosha mkono ukawa mzima tena (Marko 3:1-6)
yeye alichofanya ni kusema na mara moja mkono huo ulinyooka.

wakati wote huu Bwana Yesu alichokuwa anakifanya ni kwamba alikuwa anatengeneza wanafunzi, watu watakaochukua nafasi yake wakati atakapoondoka hapa duniani katika mwili, Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka  juu ya pepo  wote na kuponya maradhi.
Akawatuma watangaze ufalme wa Mungu na kupooza wagonjwa (Luka 9:1.)

kwa hiyo pamoja na mafundisho aliyokuwa akiwafundisha makutano na miujiza aliyokuwa akiifanya ilikuwa ni sehemu ya mafunzo kwa wanafunzi wake. Ukiacha wale wanafunzi 12 yesu alikuwa na wanafunzi wengine wengi na akiwa nao kuna siku moja aliwachukua wanafunzi sabini akawatuma katika vijiji mbalimbali ambavyo alikusudia yeye mwenyewe kwenda na aliwapa nguvu na mamlaka na walipokwenda na kurudi walishangaa sana jinsi ambavyo nguvu za Mungu zilivyotenda kazi ndani yao. Biblia inasema;

Basi baada ya hayo Bwana aliweka na wengine sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe …(Luka 10:1) hiki kilikuwa ni kipimo cha Yesu kujua kama wameyashika mafundisho yake? Na wanajijua kama wana nguvu na mamlaka ile ile iliyokuwa inafanya kazi ndani yake?. Biblia inaendelea kutuhabarisha kwamba;
Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema Bwana hata pepo wanatutii kwa jina lako.(Luka 10:17)

Nafikiri huu ulikuwa ni wakati wa furaha kubwa kwa wanafunzi mithili ya wanafunzi waliofaulu mtihani wao kwa kiwango cha juu, lakini kwa Bwana Yesu hicho kilikuwa ni kitu kidogo sana aliwaambia;
Lakini msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni. (Luka 10:20)                

Sasa hapa tunaweza kuona kwamba ile nguvu aliyokuwa anaitumia Mungu katika uumbaji wa ulimwengu, vilevile bila kupungua hata chembe moja ilihamia ndani ya Yesu na kumuwezesha kutenda mambo yote aliyoyatenda.

Yesu alipoondoka na kurudi alikotoka alituachia nguvu yote iliyokuwemo ndani yake bila kupungua hata chembe moja na ni nguvu ileile ambayo ilitumika kuumba ulimwengu.

Yesu aliiweka nguvu ya uumbaji iliyomo ndani yake aliiweka ndani yetu ili tuendelee kuzifanya kazi alizokuwa anazifanya. Ni lazima mtu wa Mungu ufahamu kwamba nguvu ileile iliyomo ndani ya Yesu ipo pia ndani yako wewe bila kupungua.

Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja ambaye alikuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimuweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema Tutazame sisi, akawaangalia akitarajia kupata kitu kwao. Lakini petro akasema, mimi sina fedha wala dhahabu, lakini nilichonacho ndicho nikupacho, kwa jina la Yesu kristo wa Nazareti simama uende, akamshika mkono wa kuume  akamwiua mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama akaanza kwenda. (Matendo 3:1,10)

Yesu anataka watu waitumie hiyo nguvu kufanya mambo makubwa kuliko aliyoyafanya yeye Bwana Yesu alisema;
Amin, amin, nawaambieni; yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi yeye naye atazifanya ;naam na kubwa kuliko hizi atazifanya kwa kuwa mimi nakwenda kwa Baba (Yohana 14:12.)
Kwa tafsiri nyepesi kabisa ni kwamba katika ulimwengu wa roho mtu ambaye amesimama vizuri kabisa anakuwa ni hatari kuliko hata Yesu mwenyewe.

watu wa Mungu tumezungukwa na nguvu kubwa sana ambayo shetani hataki tuijue, watu wengine waligundua kwamba hata vivuli vya watu wa Mungu vinaponya ilibidi wapange wagonjwa kwa kufuata uelekeo wa kivuli cha mtu wa Mungu na walipokea uponyaji. Biblia inasema;
Hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka  juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmoja wao. Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa. (Matendo 5:12,16)  

Hata nguo na vitambaa vya watu wa Mungu vina nguvu na watu wamevitumia na kupokea uponyaji.
MUNGU AKUPE UFAHAMU WA KUJUA SIRI HII. TUKUTANE TENA SEHEMU YA PILI YA SOMO HILI.

Furaha Amon Mob 0713 461593


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni