Jumatano, 11 Mei 2016

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (8)


Mwl Furaha Amon


Pingamizi
Watu mara nyingi wamesema hivi: “Kama watu wataambiwa ni halali kwao kuoa tena baada ya kuachana kwa sababu yoyote, itawatia moyo wao kuachana kwa sababu zisizo halali.” Yawezekana ikawa kweli kiasi fulani kwa watu wa dini ambao hawajitahidi kumpendeza Mungu. Lakini, kujaribu kuwazuia watu ambao hawajajitoa kwa Mungu kabisa wasitende dhambi ni swala gumu. Ila, watu waliojitoa kwa Mungu kabisa hawatafuti njia za kutenda dhambi. Wanajaribu kumpendeza Mungu.
Na watu aina hiyo kwa kawaida wana ndoa zenye nguvu. Tena, Mungu hakusumbuka sana kwamba watu katika agano la kale wataachana kwa sababu zisizo halali kwa sababu ya kuwapa sheria nyepesi ya kuoa au kuolewa tena, maana sheria aliyotoa kwa Israeli kuhusu jambo hilo ilikuwa nyepesi kabisa.
Je, tuepuke kuwaambia watu kwamba Mungu yuko tayari kuwasamehe dhambi yoyote, wasije wakatiwa moyo kutenda dhambi kwa sababu wanajua msamaha unapatikana? Kama ndivyo, itabidi tuache kuhubiri Injili. Kila kitu kinategemea hali ya moyo ya wanadamu. Wale wanaompenda Mungu wanataka kumtii. Ninajua vizuri sana kwamba msamaha wa dhambi unapatikana kwangu nikiomba, hata kama nitatenda dhambi ya aina gani. Lakini hali hiyo haijawahi kunisukuma kufanya dhambi hata kidogo, kwa sababu nampenda Mungu na nimeokoka na ninajua Mungu anataka nimtumikie kwa uaminifu. Nimebadilishwa kwa neema ya Mungu. Ninataka kumpendeza yeye.

Mungu anajua hakuna haja ya kuongeza tokeo lingine baya kwenye matokeo mabaya mengi yasiyoepukika ya talaka, kwa matumaini ya kuwahamasisha watu wakae katika ndoa. Kuwaambia watu wenye ndoa zenye shida kwamba wasiachane kwa sababu hawataruhusiwa kuoa au kuolewa tena hakutoi hamasa kwa watu kuendelea katika ndoa. Hata kama atakuamini, uwezekano wa kuishi peke yake ukilinganisha na maisha ya mateso ya ndoa daima utasikika kama paradiso kwa mtu mwenye ndoa mbaya.
Asemavyo Paulo Kuhusu Kuoa Tena
Kabla ya kupambana na tatizo la kulinganisha maneno ya Yesu na ya Musa kuhusu kuoa tena, tunahitaji kutambua kwamba yupo mwandishi mwingine mmoja wa Biblia anayekubaliana na Musa, naye ni Paulo Mtume. Paulo aliandika waziwazi kabisa kwamba kuoa au kuolewa tena kwa walioachika si dhambi, na kukubaliana na kinachosemwa na Agano la Kale.
Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu. Basi naona hili kuwa jema kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo. Je, umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke. Lakini kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia. Lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo (1Wakor. 7:25-28).
Bila shaka Paulo alikuwa anasema na watu walioachika katika fungu hili. Anawashauri walio na ndoa, wasio na ndoa na walioachika wabaki katika hali zao kwa sababu ya mateso ambayo Wakristo walikuwa wanapitia wakati huo. Ila, Paulo alisema wazi wazi kwamba watu walioachika na wanawali hawatatenda dhambi wakiingia katika ndoa.
Ona kwamba Paulo hafafanui uhalali wa kuoa au kuolewa tena kwa walioachika. Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa kama walioachika hawana lawama yoyote katika talaka ya ndoa iliyopita. (Kwani, nani mwenye sifa za kutosha kuhukumu kitu kama hicho, zaidi ya Mungu?) Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa tu kwa wale ambao waliachana kabla ya kuokoka. Hapana! Yeye alisema tu kwamba kuoa au kuolewa tena si dhambi, kwa walioachika.
Je, Paulo Alilegeza Masharti Kuhusu Talaka?
Je, ina maana Paulo alilegeza masharti kuhusu talaka kwa kuwa aliruhusu kanuni ya neema kwa habari ya kuoa na kuolewa tena? Hapana! Paulo alikuwa anapingana na talaka kwa ujumla. Katika mistari ya mwanzoni ya sura hiyo hiyo ya barua ya kwanza kwa Wakorintho, aliweka sheria kuhusu talaka ambayo inalingana na chuki ya Mungu kwa talaka.
Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi ila Bwana; mke asiachane na mumewe. Lakini ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe. Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye, asimwache. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi, bali sasa ni watakatifu. Lakini, yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyu ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani. Kwa maana wajuaje wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo? Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungualivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote (1Wakor. 7:10-17).
Angalia kwamba Paulo anasema na waamini kwanza, ambao wana ndoa na waamini wenzao. Hawapaswi kuachana, na Paulo anasema hayo si maagizo yake, bali ya Bwana. Bila shaka hayo yanakubaliana kabisa na kila kitu tulichotazama katika Biblia mpaka hapa.

Yanayofuata yanasisimua. Paulo alikuwa mkweli wa kutosha kutambua kwamba hata waamini wanaweza kuachana, japo kwa nadra. Hayo yakitokea, Paulo anasema kwamba yule aliyemwacha mwenzake akae bila ndoa au wapatane. (Japo ushauri wa Paulo unawalenga zaidi wake, kanuni hiyo bila shaka inawahusu hata waume.)
Hapa tena – alichoandika Paulo kisitushangaze. Anatangulia kuweka sheria ya Mungu kwanza kuhusu talaka, lakini ana akili ya kutosha kutambua kwamba kutii sheria ya Mungu si kitu kinachofanyika kila wakati. Hivyo, dhambi ya kuachana inapotokea kati ya waamini wawili, anatoa maagizo zaidi. Yule aliyemwacha mwenzake abaki bila kuoa au apatane na mwenzake. Hicho ndicho kinachofaa endapo waamini wawili wataachana. Muda wote watakaobaki hawana ndoa, kuna tumaini la wao kupatana, na hilo ndiyo bora. Kama mmoja wao akioa tena, hapo ndiyo mwisho wa matumaini na uwezekano wa kupatana. (Tena, kama wametenda dhambi isiyosameheka kwa kuachana, isingekuwepo sababu ya Paulo kuwaaambia wabaki bila ndoa au wapatane.)
Unaonaje? Paulo alikuwa na akili za kutosha kujua kwamba agizo lake la pili kwa waamini walioachana halitafuatwa? Bila shaka! Labda ndiyo sababu hakutoa ushauri zaidi kwa waamini walioachana kwa sababu alitazamia kwamba waamini wa kweli wangefuata agizo lake la kwanza la kutoachana, na kwamba katika mazingira adimu sana, agizo lake la pili lingehitajika. Kwa hakika, wafuasi wa kweli wa Kristo wangefanya kila kinachowezekana ili kuhifadhi ndoa yao, kama walikuwa na matatizo ya ndoa. Na kwa hakika, mwamini ambaye, baada ya juhudi zote za kuhifadhi ndoa angejisikia kwamba hana jinsi isipokuwa kuachana, kutokana na aibu yake binafsi na shauku ya kumheshimu Kristo asingefikiri kuwa na ndoa nyingine, na bado angetumainia mapatano. Inaonekana kwamba tatizo halisi katika kanisa la kisasa kuhusu talaka ni kwamba kuna waamini bandia wengi sana – watu ambao hawajawahi kumwamini Bwana Yesu kweli, na kujitoa kwake.

Ni dhahiri basi kutokana na yale Paulo anayoandika katika 1Wakorinto 7 kwamba, Mungu ana matazamio makubwa sana kwa waamini – watu waliojazwa na Roho Mtakatifu – kuliko aliyo nayo kwa wasioamini. Kama tulivyosoma, Paulo aliandika kwamba waamini wasiwaache hata wenzao wasioamini mradi wako tayari kuishi nao. Hapo tena, agizo hili halitushangazi kwa sababu linakubaliana kabisa na kila kitu tulichosoma katika Maandiko kuhusu jambo hilo hadi sasa. Mungu anapinga talaka. Lakini Paulo anaendelea kusema kwamba, kama yule asiyeamini anataka talaka, mwamini aruhusu hiyo. Paulo anajua kwamba asiyeamini hajajitolea kwa Mungu, na hivyo hamtazamii asiyeamini kutenda kama anayeamini. Nyongeza ndogo hapo: Asiyeamini anapokubali kuishi na aaminiye, ni ushuhuda mzuri kwamba, pengine asiyeamini ana mwelekeo wa kupokea Injili, au yule anayeamini amerudi nyuma au ni Mkristo bandia.

Sasa, nani atakayesema kwamba mwamini aliyeachwa na asiyeamini hayuko huru kuoa tena? Paulo hasemi hivyo kamwe, kama alivyosema kwa habari ya waamini wawili walioachana. Itabidi kushangaa ni kwa nini Mungu apinge mwamini aliyeachwa na asiyeamini kuoa au kuolewa tena. Hilo lingetimiza kusudi gani? Lakini, ruhusa hiyo inaonekana inapingana na maelezo ya Yesu kuhusu kuoa tena, kwamba, “Yeyote amwoaye mwanamke aliyeachwa, azini” (Mathayo 5:32 ). Hapo tena, kuna mashaka kwamba pengine tumefasiri vibaya yale ambayo Yesu anasema.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni