Jumatatu, 24 Septemba 2012

WAZAZI HUCHANGIA WATOTO KUKOSA AKILI DARASANI


Wazazi huchangia watoto kukosa akili darasani

 

Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na baadhi ya mashirika yanayojihusisha na malezi ya watoto ulimwenguni akiwemo Daktari Janet Gonzalez Mena wa Marekani, umebaini kuwa wazazi ndiyo mwanzo hasa wa mafanikio ya watoto wao na kwamba wengi kati ya vijana wanaoshindwa katika maisha kushindwa kwao kunaanzia ndani ya familia zao.
Malezi ya wazazi kwa tafsiri sahihi ndiyo yanayomkuza mtoto na kumtambulisha katika jamii kwamba yeye ni nani? Tunawapata watu wa kabila la Wanyakyusa,Wanyamwezi, Wayao, Wamakua, Wamakonde kwa sababu wamezaliwa na kulelewa na wazazi wa makabila hayo.

Pamoja na yote, kuzaa peke yake bila ya kusimamia tabia ya mtoto huwa ni kazi bure. Waswahili husema: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Kwa bahati mbaya wazazi wengi wamekuwa hawaelewi kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kumtayarisha mtoto awe mwema na mwenye uwezo wa kufikiri.
Hali hii inatokana na kutokuwepo kwa elimu inayotoa somo la jinsi ya kuwalea watoto bila kuwaharibia ufahamu na kuwadumaza katika uelewa wa mambo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, wazazi ambao ndiyo wenye uchungu na watoto wametajwa kuwa chanzo cha watoto kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha pamoja na masomo.
Ukichunguza kwa makini watoto wengi wanaokuwa mbumbumbu darasani (nazungumzia wale wasiokuwa na kasoro za kibaiolojia) ni wale ambao wazazi wao hawakuzingatia mambo yafuatayo katika kuwalea tangu walipokuwa wadogo hadi kukua kwao.

 HUDUMA BORA
Wazazi wengi hasa wa dunia ya tatu wanakabiliwa na tatizo la uzazi holela, usiozingatia uwezo wa kulea na kuwapa huduma muhimu watoto wao. Mfano lishe bora, mavazi na malazi. Wanasayansi wanasema chakula bora ndicho kinachoweza kuimarisha ukuaji wa viungo vya mtoto na kuufanya ubongo uwe katika hali nzuri ya kumudu kutafsiri mambo.

Hivyo ni jukumu la mzazi anayetaka mtoto wake awe na uelewa mzuri darasani ahakikishe kuwa anampatia mwanae chakula bora kitakachomjenga afya na kumuwezesha kuwa na mwili wenye nguvu ya kukabili magonjwa ya kitoto. Lakini sambamba na hilo mzazi anatakiwa kusimamia afya ya mwanae kwa kumpeleka hospitalini mara kwa mara kutibiwa na kushauriwa.

UTAMBUZI WA KIPAJI
Jambo la pili ambalo ni muhimu kwa mzazi ni kutambua mapema kipaji cha mtoto na kumuongoza sawa na kipaji chake. Ingawa shule nyingi nchini (Tanzania) hazitoi elimu ya ngazi ya chini lakini baba na mama bado wanawajibika kujua ni elimu ya kiwango gani kutoka shule gani itamfaa mtoto wao.
Inashauriwa kwa mzazi kumtambua mwanae ana uelewa gani, ili ajue namna ya kumsaidia ili afikie kiwango bora cha uelewa.  

Kwa mfano, mtoto akiwa na uelewa wa chini anatakiwa kupelekwa kwa waalimu wazuri wenye uwezo wa kumsaidia anaposhindwa, haifai mtoto wa aina hii kupelekwa shule za ilimradi na kudhani huko atasoma na kuelewa.
Itaendelea wiki ijayo.
Masomo haya ya jinsi ya kumsaidia mwanafunzi wa ngazi yoyote kuwa wa kwanza darasani yanapatikana pia kwenye kitabu changu cha saikolojia, mbinu za kusoma na kufaulu mitihani kinachopatika Dar es Salaam pekee kwa wauza magazeti.
UBAGUZI
Kuna wazazi ambao bila kufahamu madhara ya ubaguzi, wamekuwa wakiendekeza upendeleo kwa watoto kwa kuwapenda zaidi baadhi na kuwachukia wengine. 
Hili ni kosa kubwa kwani watoto wanaobaguliwa wanapokuwa na hisia za kutopendwa hudumaa au kushuka kimasomo na pengine kuharibika kitabia kwa sababu ya kukosa kimbilio la malezi. Haifai kubagua watoto!

KUVUNJA MOYO
Watoto wengi wanaoshindwa kumudu masomo darasani ni wale ambao wamelelewa na wazazi hodari wa kuvunja moyo. Kosa dogo la mtoto humfanya mzazi kuwa kama kichaa kwa kumtusi mwanae na kumtungia majina yasiyofaa, kwa mfano: “Mbwa, mjinga, ibilisi, mbumbumbu” na mengineyo. Wanasaikolojia wanasema kauli mbaya zina uwezo wa kuharibu ufahamu wa mtoto na kumfanya ajione duni na mtu wa kushindwa.
Waingereza nao wana msemo wao, “ukitaka kumuua mbwa mpatie jina baya.” Kwa maana hiyo mzazi anapomwita mtoto wake majina mabaya hasa baada ya kushindwa au kukwama katika mtihani wake anakuwa anamuua na kamwe mtoto huyo hawezi kupata alama za juu badala yake atazidi kukinai masomo na kuamua kuacha au kujiingiza katika makudi ya kihuni.
Kauli zifuatazo zinamfaa mtoto aliyekosa kufikia lengo; “Umepata alama za chini mwanangu, lakini mtihani ujao unaweza kupata zaidi” “Juma kakupita mwezi huu lakini usijali mtihani ujao utamshinda nami nitakupa zawadi kubwa sawa?” “Uwe makini ee, umekosa 7 kati ya 10, ukijitahidi kupata zote utakuwa rubani wa ndege.” Maneno haya yanaweza kumfanya mtoto ajue kwamba amefeli lakini anayo nafasi ya kufaulu.
KUHUBIRI YASIYOWEZEKANA 
Kuna baadhi ya watu ambao midomo yao haiishi kuhubiri mambo yaliyoshindikana mbele za watoto hasa yale waliyoshindwa wao. “Mimi nilikuwa mfanyakazi lakini sikuambulia kitu chochote zaidi ya umaskini, nimesoma miaka kumi na sita, lakini nchi hii hata ukisoma hupati kitu bwana.” Maneno ya aina hii hayatakiwi kusemwa mbele ya watoto wanaotafuta elimu. Wazazi lazima wawe na kauli za INAWEZEKANA.

MIGOGORO 
Migogoro ya kifamilia hasa ya wazazi ni sumu kubwa kwa mafaniko ya mtoto, mara nyingi watoto hujikuta wakishindwa kuendelea kimasomo kwa sababu ya wazazi kutengana na kujikuta wanayumbishwa kutoka kwa mzazi mmoja kwenda kwa mwingine au kulelewa na wazazi wa kambo ambako hupewa malezi yasiyostahili.
USIMAMIZI 
Mzazi anajukumu la kusimamia masomo ya mwanae kwa kumfuatilia mwenendo wake kila siku na kubuni mbinu za kumsaidia kila anapoona hafikii malengo yake.
Wazazi wengi wamekosa kufuatilia elimu za watoto kwa kuendekeza ulevi na kutozingatia ratiba za kurudi nyumbani, jambo hili ni baya kwani linaweza kuharibu mwenendo wa mtoto ambaye anatakiwa kuongozwa kwa karibu kwa kila jambo. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni