Jumatatu, 12 Novemba 2012

SURA YA NNE KUABUDU NA MAOMBI


Katika maombi ya dhati na ya kweli, mtu hujiachia akawa wazi kujieleza na kutoa siri za moyo wake akijua Mungu ndiye msaada wake na kimbillio lake. (Zab. 46:1-3),

“Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoneekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari, maji yake yajapovuma na kuumuka, ijapopepesuka milima kwa kiburi chake”.

Kwa kutambua ukuu wa Mungu na uwezo wake ndipo ibada ya kweli toka vilindi vya moyo huanza, na mtu hushuka chini sana katika ufahamu wake kumtambua Mungu ni nani na kumwabudu na kumpa sifa katika maombi.

-     Katika hali hiyo ya maombi humfanya mtu ajione si kitu bali astahiliye ni Mungu,
-     Ndipo wengine huanguka chini na kugaragara kuonyesha upendo mbele za Mungu.
“Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, walakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe”. (Mathayo 26: 39)

Hata malaika wanaabudu na kuanguka mbele za Mungu.
Yesu naye aliabudu hata akalia na kutoa machozi ya damu akiomba.
“Naye kwa vile alivyokuwa alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba, hali yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini” (Luka 22: 44)

Ayubu aliomba na kujiachia mikononi mwa Mungu akisema, najua mtetezi wangu yu hai na pasipo mwili huu nitamwona Mungu.

“Lakini mimi najua mteteaji wangu yu hai, na kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu Nami nitamwona mimi nafsi yangu Na macho yangu yatamtazama wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu” (Ayubu 19: 25 -27)


Maombi huvuka mipaka ya mazingira ya mwili wa nyama na kumleta mtu mahali alipo Mungu katika Roho kiasi kwamba muombaji anakuwa na mazungumuzo na Mungu ana kwa ana.
Kama Paulo asemavyo ABA yaani Baba aliye karibu naye kama mwana.

“Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba”. (Warumi 8: 15)

Maombi kama haya yanafanyika katika dhana ya kumtambua Mungu mwenyezi na ukuu wake, uweza wake, mamlaka na nguvu. Kisha moyo wa mtu huyu huzama ndani ya ibada kwa maombi na kumwabudu, na kumpa sifa yeye aliye juu Mungu mkuu. Ufahamu huu unamfanya mtu amheshimu Mungu na kumwabudu kwa mshangao mkuu, na kumvuta kumpenda na kuichukia dhambi, kama Isaya asemavyo,

“Mimi ni mtu mwenye midomo michafu na ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu”. (Isaya 6:1-5)

Petro naye akasema,
“Ondoka kwangu Bwana mimi ni mtu mwenye dhambi”. (Luka 5:8-9).

Heshima hii kwa Mungu huona utukufu wa Mungu ulivyo mkuu na utakatifu wake ulivyo wa ajabu, na kushindwa kustahimili mbele ya Mungu kisha kusema maneno hayo ya unyenyekevu katika maombi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni