Jumatatu, 16 Mei 2016

MAANA YA WOKOVU (1)




“Kwasababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako yakuwa Mungu alimfufua katika wafu, UTAOKOKA. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa mtu hukiri hata KUPATA WOKOVU”. (Rum 10:9-10.)
Baada ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wako, ni muhimu sana kupata mafundisho ya awali, yatakayokusaidia kujua kwa hakika, maana ya KUOKOKA au WOKOVU;Biblia inasema;-
“ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.” (Efe 4:14)

Ndio maana Yesu alisema, tukishawahubiri na kuwasaidia kuokoka, tuwafundishe yote!
“Yesu akaja kwao akasema nao, akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na mkiwafundisha kuyashika yale yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote hadi ukamilifu wa dahari”. (Math 28:18-20).
“Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara katika imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani”. (Kol 2:6-7)
Wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali” (Mdo 2:42)
“Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu, lakini kwa upole na kwa hofu” (1Pet 3:15)
Watu wengi wamechanganya sana maana halisi ya neno “kuokoka”. Unaweza kupewa tafsiri nyingi na watu, juu ya neno “kuokoka”. Wengine hudhani kuokoka ni dini au dhehebu fulani la “walokole”. Wengi hudhani wokovu ni maisha fulani ya kujinyima raha na kujitenga na jamii.

Wengine hudhani wokovu ni maisha duni na ya umasikini au kutokuwa na mali za kifahari. Ndani ya fikra za watu, kuna tafsiri nyingi tofauti juu ya “kuokoka” na hizo tafsiri nyingi si sahihi. Lakini hii hapa chini nadhani ndio tafsiri rahisi zaidi kueleweka.

NINI MAANA YA KUOKOKA?

Kuokoka ni lugha ya kawaida kabisa, yenye maana ya;
Kunusurika, kuokolewa, kusalimika, kupona, kukombolewa, kufunguliwa au kutoka katika janga au hatari fulani.

Mfano:-
Kunusurika; Paulo aliposafiri mashuani pamoja na watu wengine mia mbili na sabini na sita, alisema;
“safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia … baada ya muda mchache, ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani … na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake, wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota havikuonekana kwa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka … na baharia walipotaka kukimbia na kuiacha merikebu … Paulo akawaambia akida na askari, hawa wasipokaa ndani ya merikebu, hamtaweza kuokoka … Shauri la askari lilikuwa kuwauwa wafungwa, mtu asiogelee na kukimbia. Bali akida akitaka kumponya Paulo, akawazuia wasifanye kama walivyokusudia, akawaamuru wale wawezao kuogelea, wajitupe kwanza baharini, wafike nchi kavu … na hivyo watu wote wakapata kuifikilia nchi kavu salama. Tulipokwisha kuokoka, ndipo tulipojua ya kuwa kisiwa kile chaitwa Melita”. (Mdo 27: 1-44. 28:1)
 Hivyo tunaona neno “KUOKOKA” katika mistari hii, limetumika kama “KUNUSURIKA”.


Kupona; Wayahudi walimdhihaki Yesu , “Jiponye nafsi yako, ushuke msalabani.
( Mk 15:30)
Sisi je, tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanzaulinenwa na Bwana, kasha ukadhibitishwa kwetu na wale waliosikia. (Ebr 2:3)
KUOKOKA” katika mistari hii imetumika kama “KUPONA”.
“Na niseme nini tena? Maana wakati usingetosha kuleta habari za Gideoni, na Baraka, na Samsoni, na Yefta, na Daudi, na Samweli, na za Manabii; Ambao kwa imani, walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga.
KUOKOKA katika mistari hii, imetumika kama KUPONA, KUSALIMIKA AU KUNUSURIKA!

Kusalimika; Wakati Mungu anaangamiza dunia kwa maji ya gharika, Biblia inasema;
“Wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu mjumbe wa haki na watu
wengine saba, hapo alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa wasio mcha Mungu. Tena
akaihikumu miji ya sodoma na Ghomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya
akaifanya iwe ishara, kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya hayo.
Akamwokoa Lutu, yule mwenye haki, aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi
wa hao wahalifu. (2Pet 2:5-7)
“Hapa KUOKOKA” imetumika kama KUSALIMIKA” kutoka katika janga la gharika na moto.

- Kufunguliwa au Kukombolewa; Herode alipomtia Petro gerezani ili amuuwe, Biblia inasema;
“Panapo majira yale yale, herode mfalme akanyoosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa. Akamuuwa Yakobo ndugu yake Yohana kwa upanga. Na akiona yakuwa imewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamshika na Petro … akamweka gerezani, akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka, kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa lilikuwa likimwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule, Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, alikuwa amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi! Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua yakuwa ni kweli, yaliyofanywa na malaika. Bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, “sasa nimejua yakini yakuwa, Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi”. Na alipokuwa akifikiri hayo, akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana Marko … na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha, kijakazi jina lake Rhoda akaja kusikiliza. Alipoitambua sauti ya Petro, hakufungua mlango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani, akawaambia kwamba, Petro anasimama mbele ya lango. (Mdo 12:1-14-19)
KUOKOKA” katika mistari hii, imetumika kama “KUFUNGULIWA” au “KUKOMBOLEWA” katika kifungo.

Tuendelee kufuatilia somo hili katika sehemu ya pili

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni