Jumamosi, 14 Januari 2017

SOMO: KUNENA KWA LUGHA SEHEMU YA KWANZA


Mwl Furaha Amon








Utangulizi;
Watu wengi wanaofuatilia masomo ninayofundisha wanaonyesha kiu kubwa ya kutaka kufahamu kwa undani kuhusu kunena kwa lugha, kunakotokana na ujazo wa Roho Mtakatifu. Inaonekana kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na jambo hili ambalo ni kubwa na muhimu sana katika maisha ya kiroho ya mtu mmoja mmoja na kanisa kama kundi. Kwa kuwa kiu hii bado ni kubwa kwa wasomaji wangu, nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kuwasaidia kuelewa kwa kiasi habari za kunena kwa lugha. Naamini kwa kupitia mafundisho haya, wale wenye kiu ya kunena kwa lugha wataweza kuanza kunena kwa lugha ili mradi kama walipokea ujazo wa Roho Mtakatifu.

AHADI YA KUJA ROHO MTAKATIFU.
Yesu baada ya kufufuka alipaa mbinguni, lakini kabla ya kufa  na kufufuka, alikuwa ameahidi kuleta msaidizi, ambaye ni Roho Mtakatifu ambaye angekuwa msaidizi wa watu watakaomwamini Yesu.
“Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine. Ili akae nanyi hata milele. Ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa maana hauwezi kumwona wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” (Yohana 14: 15-17)
Siku kumi baada ya Yesu kupaa mbinguni Roho Mtakatifu alishuka. Roho Mtakatifu alikuja duniani ili kuzisimamia kazi zote za Mungu zilizopo hapa duniani. Na kuanzia wakati huo, kazi zote za Mungu  zinamilikiwa na Roho Mtakatifu. Roho  Mtakatifu ndie mtendaji wa kazi zote za Mungu zilizopo hapa duniani. Nje ya Roho Mtakatifu hakuna kazi yoyote ya Mungu inayoweza kufanyika. Kazi zinazofanywa na Roho Mtakatifu zipo nyingi sana lakini zimeanishwa na Biblia ni kama zifuatavyo;-
·       Anatufundisha
·       Anatuonya
·       Anatuongoza
·       Anatufariji
·       anatutia moyo
·       anatuombea
·       anatenda miujiza
·       anaponya n.k
Kazi zote hizi za Roho Mtakatifu, anazifanya katika maeneo yote ya maisha ya mkristo. Hapa ni muhimu kufahamu kwamba ili Roho Mtakatifu aweze kuzifanya kazi zote hizo bila ya kusahau eneo lolote la maisha ya mkristo, Roho Mtakatifu huzifanya kazi hizo kwa mpangilio maalumu.
Hebu tujaribu kuangalia mfano wa utendaji kazi wa serikali za kidunia. Kila mtu anajua vizuri kabisa kwamba kazi ya serikali yeyote ile duniani, ni kuongoza wananchi wake katika maeneo mbalimbali ya maisha yao ya kila siku. Kwa sababu hiyo ili serikali iweze kutimiza wajibu wake huu bila kusahau eneo lolote la maisha ya watu inaowaongoza. Serikali  imegawa majukumu yake katika wizara mbalimbali ambazo hutekeleza majukumu hayo.
kwa mfano mambo yote yanayohusu afya katika nchi nzima yanashughulikiwa na wizara ya Afya. Na maswala yanayohusiana ulinzi, yanashughulikiwa na wizara ya Ulinzi. Hali kadhalika mambo yanayohusu elimu yapo chini ya wizara ya elimu. Ni hivyohivyo pia kwa wizara ya  mambo ya ndani, wizara ya mali ya asili, wizara ya kilimo, wizara ya ujenzi, wizara ya mambo ya nje n.k.
Kwa kutumia mfano huo itakusaidia kujua kuwa kwamba hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Roho Mtakatifu. Na yeye, ili aweze kufanya kila kitu kama kinavyotakiwa kufanyika kwa mkristo, anafanya kwa kutumia karama tisa ambazo ni kama wizara kwa mpangilio wa serikali za kidunia. Karama hizo ni kama zifuatazo;-
1.  karama ya neno la hekima
2.  kalama ya neno la maarifa
3.  karama ya kupambanua roho
4.  karama za kuponya
5.  karama ya miujiza
6.  karama ya imani
7.  karama ya unabii
8.  kalama ya aina za lugha
9.  kalama ya tafsiri za lugha.
Nje ya hizi kalama hakuna kazi yoyote ya Mungu inayoweza kufanyika labda ufanye ujanja ujanja na  mazingaombwe ambayo ni kazi ya shetani.
Kazi zote za Mungu zinazofanyika hapa duniani kwa sasa kila mojawapo inafanyika kupitia mojawapo ya hizi karama tisa. Huduma zote za Roho Mtakatifu kama vile Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji na Mwalimu, pia huduma hizi hufanya kazi zake kupitia Roho Mtakatifu.
KALAMA YA KUNENA KWA LUGHA
Kunena kwa lugha ni mojawapo ya karama tisa. Ni  karama iliyo katika kundi la kalama tatu za uvuvio, karama hizi ni kama ifuatavyo;
1.  Unabii
2.  Kunena kwa lugha
3.  Tafsiri za lugha.
Kalama hizi zinaitwa karama za uvuvio kwa sababu, utendaji kazi wake hujidhihirisha kwa mtu anayetumiwa kushukiwa na kufunikwa na nguvu maalumu, ambayo hudhibiti uwezo wa kuongea wa mhusika. na Roho Mtakatifu huchukua nafasi ya kutumia midomo ya muhusika kuyazungumza hayo maneno.
Maneno hayo yanaweza kuwa katika lugha yoyote atakayoamua Roho Mtakatifu. Hii ni kwa sababu Kuna lugha za mbinguni (za malaika) na kuna lugha za wanadamu. Pamoja na hayo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza kwa kutumia lugha inayoeleweka kwa muhusika.
Mtu anayehusika hujikuta anazungumza maneno ambayo hakuyapanga yeye kwa ufahamu wa akili yake. Mlolongo  wa tukio hili ndiyo ambalo huitwa kuvuviwa na Roho Mtakatifu. Mbali na karama za uvuvio kuna karama za ufunuo ambazo nazo pia ziko tatu ambazo ni;
1.          Karama ya neno la hekima,
2.          Karama ya neno la maarifa
3.          Karama ya kupambanua roho.
Kwa sababu lengo la somo hili ni kufundisha kalama moja tu ya kunena kwa lugha. Kwa maana hiyo sitagusia kwa undani utendaji kazi wa kalama hizo zingine, isipokuwa kwa faida ya msomaji nitazitaja tu bi kufafanua.
Karama zingine zinaitwa karama za nguvu, ambazo pia ziko tatu kama ifuatavyo
1.          karama ya miujiza
2.          karama ya imani na
3.          karama ya kuponya
Lakini kama nilivyotangulia kueleza awali kwamba katika somo hili hatutazungumzia habari ya karama zingine, bali nitazungumzia karama ya kunena kwa lugha peke yake
Baada ya mtu kuokoka, na kujazwa roho Roho Mtakatifu, na ishara ya kunena kwa lugha kuonekana, hiyo ni ishara kwamba karama zote tisa huwa ndani ya huyo mtu na ni Roho Mtakatifu ndiye huamua ni karama ipi ndiyo ifanye kazi ndani ya mhusika kama apendavyo yeye.
Kwa kawaida Roho Mtakatifu humgawia kila mkristo ndani ya kanisa mojawapo ya karama au humgawia karama kwa idadi kadhaa kulingana na huduma ambayo Mungu amewekeza ndani yake.
Hivyo  wakristo hujikuta huyu ana karama hii na Yule ana karama tofauti na mwingine. Mwingine anaweza kuwa na karama ya imani, mwingine karama ya unabii na mwingine karama ya neno la maarifa n.k.

Wakristo wote baada ya kujazwa Roho Mtakatifu, ishara ya kunena kwa lugha huonekana mara tu baada ya kujazwa Roho Mtakatifu. Inaweza isionekane kwa dhahiri sana kutokana na uzoefu lakini baada ya kujizoeza na ulimi kuzowea inakuwa kama lugha ya kawaida tu. Hiyo ndio inaitwa karama ya kunena kwa lugha. 
mwisho wa sehemu ya kwanza ya somo. usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya so hili na Mungu akubariki sana. kwa msaada zaidi tunaweza kuwasiliana kwa namba 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni