Alhamisi, 9 Agosti 2012

KWA HERI MAMA ESTER ANDREW PARK NA GRACE MEE JEE

KWA HERI MAMA ESTHER KYUNG PARK.nakumbuka ilikuwa siku ya  tarehe 11 Nov 12 asubuhi wakati najiandaa kwenda kazini nilipigiwa simu kutoka kwa mmoja wa rafiki yangu wa karibu na kwa kweli huwa hana kawaida ya kunipigia simu mapema asubuhi kiasi hicho. moyoni nilianza kuhisi kuna taarifa mbaya na ndivyo ilivyokuwa kwangu. ilikuwa ni habari ya msiba wa mama Ester Park. ilikuwa ni siku mojawapo niliyoiona nzito sana kwangu na nilijipanga vizuri kuhakikisha ninakuwa karibu na mchungaji Andrew Park na ilinibidi kufika nyumbani kwake mapema kidogo ambako nilimkuta akifanya mawasiliano na ndugu zake mbalimbali ambao wapo nje ya Tanzania. hali niliyomkuta nayo ilinitia moyo sana alionekana mtulivu sana na kama mtu aliyekubali kwamba Mungu ametwaa mojawapo ya matunda yake. sikuweza kuwa na maneno mengi zaidi ya kumshukuru Mungu.
Wachungaji wa Tanga wakishirikiana na Watumishi wa Korea Kusini wakibeba jeneza lenye mwili wa mama Ester Park kuupeleka katika mahali atakapopumzika milele nje kidogo ya jengo la kanisa hilo. msiba huu uliwakutanisha watumishi wengi kutoka ndani na nje ya mji wa Tanga.
Mwili wa Mama Park ukishushwa katika mahali palipoandaliwa kwa ajili ya kupumzika kwa amani na alipumzika katika kaburi lililochimbwa nje ya kanisa lake eneo la Kange Tanga


Rev George Nywage na Mchungaji Bright Mashauri wakimtuliza mtoto mdogo wa Marehemu ambaye aliumizwa sana na msiba huu wa kumpoteza mama yake kipenzi watoto hawa muda mfefu wameishi mbali na wazazi wao wanaishi Marekani.

Picha ya Marehemu Ester Park ikiwa juu ya Jeneza lililobeba mwili wake muda mfupi kabla ya mazishi yake. tunamshukuru Mungu kwa ajili ya huduma yake ambayo ameifanya kwa nchi yetu ya Tanzania. Tulimpenda kwa sababu alikuwa ni mtu anayependa watu. mtu muwazi na aliyependa na kuheshimu utamaduni wetu kama alivyo mchungaji Andrew Park aliyekuwa mume wake tunaamini kwamba mama yetu amepumzika kwa amani akisubiri siku ambayo parapanda litakapolia. pumzika kwa amani mama yetu Ester Park
Mchungaji Andrew Park akiwa na watoto wake wanaoishi Marekani ambao walikuwa wanasubiriwa ili waweze kumzika mama yao. Aliye katikati ni mtoto mkubwa wa  Marehemu ambaye alitoa hotuba iliyotusisimua sana watu wengi waliohudhuria ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu. kwanza kabisa alituhakikishia kwamba ana uhakika kwamba sisi tuna huzuni lakini Mungu anashangilia kumpokea mama yake katika ufalme wake. lakini pia alielezea mahusiano yao yalivyokuwa ya karibu mno na mama yao na jinsi alivyojitoa kwao. alitusimulia mkasa mmoja ambao uliwapata walipokuwa wadogo na mama yao aliwapeleka kutembea  katika eneo fulani ambalo watu wanalitumia kwa kuteleza kwenye barafu,akasema yeye na mdogo wake walikuwa hawajatulia vizuri kwa maana ya kwamba walikuwa watundu na katika utundu walijikuta wanateleza na kutumbukia kwenye shimo lakini mama yao aliwahi kuwazuwia na kuwaokoa lakini yeye mama yao alitumbukia na kuvunja mkono. haya ni maneno machache sana katika hotuba ile yaliyonisisimua sana na kujifunza kwamba watoto unapowafanyia kitu kizuri watakikumbuka daima.







Ester na Chimpae marafiki wa Grace Mee Jee
baada ya kupita muda si mrefu tulipata tena msiba ambao ulitufanya kuduwaa, ulikuwa ni msiba wa mama yetu Grace Mee Jee ambao ulitokea nyumbani kwao Korea ya Kusini na ulichomwa moto kama ilivyo kwa jadi yao na baadae kuzikwa katika jiji la Tanga kama ambavyo walikubaliana na mume wake Rev James Lee. kama wanavyonekana katika picha wakiwa pamoja na mama Grace
Mama Grace atabaki anakumbukwa daima kwangu mimi, na kwa familia yangu kwa sababu alikuwa rafiki wa kweli. Alijitahidi sana kuonyesha upendo wa waziwazi kwangu na kwa familia yangu, alinifundisha mambo mengi hasa yanayohusu maadili na tabia njema. alitumia muda mwingi kunifundisha ustaarabu wa kwao. Najua kwamba kiuchumi walikuwa vizuri kuliko mimi lakini waliniheshimu kwa sababu na mimi sikutaka kujiweka chini sana nilihakikisha kwamba na mimi nafanya kila juhudi kuwaonyesha kwamba na mimi nina uwezo japo mdogo na ninaweza kuwasaidia na kuwapa zawadi kama ambavyo wao pia wananipa. nilitaka kufuta mawazo ya watu wa nje hasa ulaya na mashariki ya mbali kwamba watu weusi ni watu wa kusaidiwa tu na kuombaomba
wakati mwingine urafiki wetu ulipita katika nyakati ngumu lakini tangu Mungu aniunganishe nao, niliazimia kwamba sitakuwa mtu wa kujipendekeza kwao na nitawashauri bila woga wala unafiki. na ninamshukuru Mungu kwamba ndivyo ilivyokuwa, sikuwahi kuyumba katika kuwashauri hata kama walikuwa hawakubaliani na mim, lakini baadae walikuja kujua kwamba, niliwashauri katika mambo ya kweli katika kila eneo la maisha yao. ilikuwa ni ngumu kwa sababu wakati fulani unawakuta wameshafanya uamuzi juu ya jambo fulani, na ninafika na kupangua kwa hoja na kuweka wazi na hatimaye wanabadilisha uamuzi au wanaamua kuendelea na uamuzi wao. na wakiendelea na maamuzi yao ni lazima wewe uonekane mbaya, lakini baada ya muda wanakuja kukutana na vikwazo ulivyowaambia.
Kapumzike kwa amani rafiki yetu. Mungu atakukumbuka kwa mema ambayo umewatendea watu mbalimbali ambao umeishi nao. najua hujafa kwa ghafla bali umeugua kwa muda mrefu. Hapana shaka ulipata nafasi ya kutengeneza njia yako mbele za Mungu. Na kumuomba msamaha katika maeneo ambayo huna uhakika kama ulifanya vizuri. Na kwa sababu hiyo Mungu atakufufua siku ya hukumu. KWA HERI RAFIKI YANGU GRACE MEE JEE
GRACE katika siku zake za mwisho wakati akiwa hospitali nchini Korea Kusini







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni