Jumanne, 15 Agosti 2017

HEKALU LA SULEMANI


Kama tulivyokwisha kuona tayari Mungu asingeruhusu Daudi kujenga nyumba kwa ajili ya jina lake kwa sababu alikuwa “Amemwaga damu nyingi” Badala yake mwanaye Sulemani ndiye aliyechaguliwa kulijenga hekalu kufuatana na mipango au ramani ambayo Mungu alikuwa amemwonyesha Daudi (1 Mambo ya Nyakati 28:11).
Daudi akakusanya hazina kubwa wakati wa utawala wake na kumtia moyo mwanaye katika kazi hiyo “BWANA, na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA Mungu wako kama alivyonena kwa habari zako' (1 Mambo ya Nyakati 22:11)
1 Wafalme 5-8
DAUDI ANAFANYA MAANDALIZI : 1 Mambo ya Nyakati 28:10 – 20, 29:1– 7
Maandalizi mengi kwa ajili ya hekalu yalifanywa na Daudi. Maana kwake ulikuwa ni mpango mzuri sana tena wa kusisimua naye aliweza kuona hekima ya Mungu katika kusubiri wakati wa amani kabla nyumba ya aina hiyo ya kuabudia haijajengwa. Mungu alimpa Daudi ramani ya jengo (1 Mambo ya Nyakati 28:11, 19), naye akachora mchoro kwa ajili ya Sulemani. Daudi alipowashinda maadui zake, akakusanya hazina nyingi ya dhahabu, fedha, shaba na chuma, mbao na vito vya thamani, 'ndipo' akasema, 'Kwa uweza wangu wote nimeiwekea akiba ya nyumba ya Mungu wangu' (1 Mambo ya Nyakati 29:2). Kutokana na shauku ya Daudi kwa ajili ya kazi ilisababisha wana wa Israeli na wao pia kwa hiari yao wakatoa kwa moyo, wakatoa vito vya thamani walivyokuwa navyo.
Wakuu wa mbali za mababa na maakida wa maelfu na wa mamia wakajitoa kwa hiari yao, nao wakatoa kwa hiari, dhahabu na fedha na shaba na chuma, na kila aliyekuwa na vito vya thamani na wakatoa ili viwekwe kwenye hazina ya nyumba ya BWANA. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe; kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA. Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu (1 29:6-9).
Kwa hiyo Daudi akageuza mioyo ya watu wakamwelekea Mungu katika kazi hiyo ya ujenzi wa Hekalu. Na katika maombi yake kwa Mungu Daudi akasema: 'Akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili yake jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe' (1 Mambo ya Nyakati 29:16).
 SULEMANI ANAJENGA HEKALU-1 Wafalme 5
Wakati Hiramu, mfalme wa Tiro, aliposikia habari juu ya kifo cha Daudi akapeleka ujumbe wa rambi rambi kwa mfalme Sulemani, kwani Hiramu alikuwa akimpenda sana Daudi siku zote, sasa akatamani kwamba Sulemani angeendeleza urafiki alioufurahia pamoja na baba yake.
Sulemani alikuwa tu na furaha mno kupokea wajumbe hao. Akatuma mara moja ombi la msaada kwa Hiramu katika kujenga hekalu akielewa kwamba alikuwa tayari ameshatoa mierezi kutoka misitu ya Lebanoni kwa ajili ya Daudi kujenga ikulu (nyumba yake ya ufalme ) huko Yerusalemu (2 Mambo ya Nyakati 2:3) Akamweleza Hiramu kuwa, 'nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa, kwa sababu Mungu wetu ni mkuu juu ya miungu yote'  (2 Mambo ya Nyakati 2:5). Hiramu aliweza kuona ya kwamba Mungu wa Israeli alikuwa amewabariki mno watu wake kwa kumpatia Daudi mwana mwenye hekima kutawala badala yake. “Kwa sababu BWANA awapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme juu yao”, Hiramu aliandika katika barua yake kwa Sulemani.
“Ahimidiwe BWANA,Mungu wa Israeli, aliyeumba mbingu na nchi, aliyempatia Daudi mwana wa hekima...ili amjengee BWANA nyumba (2 Mambo ya Nyakati 2:11 – 12). Hivyo Hiramu alikubali kumpelekea Sulemani mbao na akampatia watu ambao ni mafundi stadi wenye ujuzi na akili kwa kubadilishana na ngano, shayiri, mvinyo na mafuta kutoka Israeli (2 Mambo ya Nyakati 2:10).

Kila mwezi watu 10,000 walipelekwa kutokea Israeli hadi kwenye misitu ya Lebanoni kusaidia, ambapo huko Israeli maelfu walipelekwa kwenye machimbo, kukata na kuunda mawe mazuri kwa ajili ya msingi na kuta za jumba. Kazi yote ilifanyika mbali na uwanja wa hekalu, hakuna sauti iliyosikia katika Yerusalemu wafanyakazi wale watalaamu walikuwa na ufundi mkuu hivi kwamba muda ulipowadia wa kuanza ujenzi Biblia inasema,
“wala nyundo wala shoka wala chombo cha chuma chochote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba” (1 Wafalme 6:7).
Kila kitu kilikaa kikamilifu kwa usawa kabisa, kama Mungu alivyokuwa amepanga. Sulemani alianza kujenga katika mwaka wa nne wa enzi yake, nayo ikakamilika katika mwaka wa kumi na moja – miaka saba na nusu ya kazi ya uangalifu na utaalamu.
RAMANI YA HEKALU
Hekalu lilikuwa kama ile hema ya kukutania ambayo Mungu alikuwa amemweleza Musa kuijenga kule jangwani, Hema ya kukutania ilikuwa bado ikitumiwa siku za Daudi katika Israeli. Ilikuwa ni hema, iliyogawanywa katika vyumba viwili, vilivyoitwa patakatifu na patakatifu pa patakatifu. Kila wakati wana Israeli walipoondoka na kuendelea katika safari zao, hiyo hema ya kukutania ilishushwa chini kwa uangalifu na kubebwa na Walawi. Kama ilivyokuwa hekalu la Sulemani, lilikuwa mahali pa ibada, ambapo Mungu aliweka utukufu wake, nao Israeli walikuja kuabudu na kumtolea BWANA dhabihu. (Kutoka 40:17 – 38). Hata hivyo kulikuwa na tafauti moja kubwa, kwa kuwa sasa wana wa Israeli walikuwa wameshajijenga kama taifa ndani ya nchi yao, Mungu alikuwa anaibadili hema ya kukutania na kuwa hekalu la mawe, kuwa la kudumu na kuwa mahali pa utukufu zaidi kwa ibada ambalo lilisimama juu ya mlima Moria huko Yerusalemu.
Palikuwa ni makao ya Mungu katika Israeli, ambapo Makuhani na Walawi wangeweza kumtumikia Mungu kwa niaba ya watu wote. Hekalu lilikuwa pia kubwa kuliko hema ya kukutania. Lilikuwa la mawe lililonakishiwa au kurembwa na mbao na kupakwa jengo lote lilifunikwa kwa dhahabu. Kwenye sehemu za vyumba vitatu vya hekalu, vyumba vilijengwa vyenye ghorofa tatu kwenda juu kwa kutumiwa na Makuhani na kwa ajili ya hazina. Kwa upande wa mashariki mwishoni palikuwa na ukumbi wenye lango ka kuingilia, mbele ya ukumbi kuliluwa na minara (mihimili) miwili mirefu sana ya shaba .Mihimili hii ilipewa majina moja likiitwa Yakini na lingine Boazi kwenye eneo la ukumbi wa nje palikuwa tangi kubwa la maji, iliyoitwa bahari, mabeseni mengine kumi madogo zaidi ambamo dhabihu ziliwekwa, matano kwa upande wa kaskazini na matano kwa upande wa kusini. Na madhabahu kubwa sana ya shaba kwa ajili ya dhabihu za kuteketezwa ilisimama eneo la nje pia.

Kwa upande wa ndani, hekalu liligawanywa kama vile ilivyokuwa Hema ya kukutania vyumba viwili. Chumba cha kwanza kuelekee mashariki mwishoni palikuwa ndio mahali Patakatifu, humo waliingia makuhani na kuwasha vinara vile kumi vya taa na kuweka mikate ya wonyesho kwenye zile meza kumi za dhahabu, chetezo cha kufukizia uvumba kilitengenezwa kwa dhahabu ilikuwa mbele ya pazia lililotenganisha mahali patakatifu na patakatifu pa patakatifu. Kwa upande mwingine wa pazia yalikuwepo Makerebi na sanduki la Agano ambalo juu yake utukufu wa Mungu uliangazia hapo. Ni kuhani mkuu peke yake aliweza kuingia humo na ni katika siku moja kwa mwaka, wakati wa siku ya upatanisho. Vyumba hivi viwili vilitenganishwa na milango miwili (1 wafalme 6:31) na pazia ambalo lilikuwa limepambwa vizuri sana na michoro ya Makerubi.

Patakatifu pa Patakatifu palikuwa eneo lililo mraba kimuundo mikono 20 urefu, mikono 20 upana na mikono 20 urefu (ikiwa mara mbili ya ukubwa wa vipimo vya Patakatifu pa patakatifu ndani ya hema ya kukutania).

Makereubi wale wawili aliowatengenseza Sulemani kwa mti wa mzeituni uliofunikwa kwa dhahabu. Walisimama kwenda juu mikono 10 urefu na mabawa yaliyonyooka na kila kerubi moja alikuwa na bawa moja la kerubi mikono mitano urefu wake, na bawa la pili kerubi mikono mitano urefu wake;mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili.

Makerubi hawa waliwekwa ndani ya patakatifu pa patakatifu, 'na mabawa ya makerubi yakanyooshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi wa pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba' (1Wafalme6:23-27).

Wakati Sanduku la Agano lilipoletwa ndani na Makuhani liliwekwa chini ya mabawa ya Makerubi ndani ya Patakatifu pa patakatifu. Juu ya Sanduku la Agano palikuwa na Makerubi wake ambao walisimamishwa kwenye kiti cha Rehema ambacho kilifukwa kwa dhahabu. Ndani ya Sanduku mlikuwemo zile mbao mbili za mawe ambazo zilikuwa zimeandikwa zile amri kumi. (Kumbukumbu la Torati 10:3 – 4, 2 Mambo ya Nyakati 5:10). Baada ya kumalizika hekalu lote lilikuwa mahali penye utukufu mno penye uzuri wa kupendeza sana, mahali penye kufaa kuwa makao ya Mungu katikati ya watu wake.

FUNDISHO KWETU
 Hekalu la Sulemani halipo tena huko Yerusalemu karne nyingi zilizopita liliharibiwa kwa kubomolewa, kwani watu walipogeuka na kuacha kumwabudu BWANA, aliwaruhusu adui zao kuwateka kuwapeleka nchi ya mbali.

 Mungu sasa anajenga hekalu kuu kuliko lile la Sulemani. Ni hekalu lilijengwa kwa “mawe yaliyo hai” (1 Petro 2:5)-watu ambao wanamruhusu Mungu kuyarekebisha maisha yao ili kwamba wawe wenye kustahili kuwa hekalu hai la BWANA. Bwana Yesu Kristo ndiye jiwe kuu la pembeni katika jengo lile (Waefeso 2:20) na mawe mengine yote inapasa yawe kama Kristo alivyo. Maisha yetu yatakuwa yenye kumpendeza Mungu ikiwa tutafuata mfano wake, kwani alimtii Mungu katika mambo yote.

Tunafahamu kwamba atakaporudi na ufalme wa Mungu ukasimamishwa,dunia yote itajawa na utukufu wa Mungu (Hesabu 14:21), kwani watu wake wote kila mahali walisifu Jina lake. Na tujaribu kwa bidii sasa kujifunza njia za Mungu na kuwa na hekima ili tuweze kuwa sehemu ya hekalu lile ambalo Mungu atalisimamisha katika duniani.

MAELEZO YA NYONGEZA
KUWEKWA WAKFU KWA HEKALU: 1 Wafalme 8
Wakati hekalu lilipomalizika na kusimama katika utukufu wake Sulemani akatangaza sherehe maalumu kwa ajili ya kuliweka wakfu kwa Mungu. Ulikuwa ndiyo wakati wa Sanduku la Agano kuletwa na kuwekwa katika mahali patakatifu pa patakatifu.Ilikuwa shangwe ya jinsi gani kwa wana wa Israeli wote siku ile ambapo Sanduku lilipoletwa kutoka Sayuni.

Walawi wakapaza sauti zao katika kusifu na kuimba na kucheza kwa kuvipiga vyombo vyao vya nyimbo na ,'wakamsifu na kumshukru BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhari zake ni za milele’ (2 Mambo ya Nyakati 5:12–13)

Hivyo Makuhani wakaleta Sanduku na kuliweka chini ya mabawa za wale Makerubi wakuu wawili. Kwa kadiri wana wa Israeli walivyobakia kuwa watiifu kwa Mungu, hapo ndipo lingedumu kukaa hapo. Na makuhani walipotoka katika Patakatifu pa patakatifu, wingu la utukufu lilijaa hekalu lote, hata makuhani hawakuweza kubakia mle ndani ili kuendelea na shughuli zao. Hapo palikuwa na dalili ya Uwepo wa Mungu, ikiwaonyesha kwamba Mungu alikuwa ampendezwa na yote yaliyokuwa yamefanyika.

Ndipo Sulemani aliposimama kwenye jukwaa maalumu ambapo watu wote wangeweza kumwona, watu wakasimama naye mfalme akawabariki na kusema juu ya heshima kubwa ambayo Mungu alimpatia yeye katika kumruhusu kujenga nyumba kwa jina BWANA huko Yerusalemu. Kisha akapiga magoti na kunyanyua mikono yake kuelekea mbinguni na akamwomba Mungu sala yake kwa niaba ya watu wote (2 Mambo ya Nyakati 6:13) “BWANA, Mungu wa Israeli” akasema “hakuna Mungu kama wewe, mbinguni ,wala duniani chini... Lakini Mungu je!yamkini atakaa duniani? Tazama mbingu na mbingu za mbingu hazikutoshi wewe, sembuse nyumba hii niliyoijenga?” (mstari 14 ,18)

BWANA ni Mungu mwaminifu ushikaye maagano, kama BWANA,alivyofanya kwa Daudi, na kuliweka jina lake katika Yerusalemu (mstari 24,29). BWANA ndiye alikuwa Mungu wa Rehema naye angelisikia sala zao wote wamwani wanatembea mbele mbele kwa mioyo yao wote (mstari 23).

Hivyo Sulemani akamwomba Mungu ya kwamba hata matatizo ya aina yoyote kama yangetokea juu ya watu wake kwa sababu ya dhambi zao kama wangerejea na kuomba kuelekea hekalu hili na kuomba basi angewasikia maombi yao. “kama wakirejea tena kwako wakiomba na kukusihi katika nyumba hii, basi usikie huko mbinguni na ukaisamehe dhambi ya watumwa wako na watu wako Israeli” (mstari 35-36).
 Hata kama wana wa Israeli wangechukuliwa mateka kwenda nchi ya mbali, Sulemani alimwomba Mungu awasamehe na kuwarejesha katika nchi ambayo aliwapatia baba zao (1Wafalme 8:33-34).


Ndivyo Sulemani alivyoomba kwa moyo wake wote mbele za Mungu na kuwatia moyo watu kutembea mbele yake kwa mioyo yao mikamilifu (mstari 61). Na mara ghafla alipoamalizia sala yake moto ulishuka kutoka mbinguni ukaishukia dhabihu zilizokuwa kwenye madhabahu kuu ya shaba na kuziteketeza zote. Watu wote wakaogopa kwa kuona tukio hilo la muujiza nao wakasujudu kifudi fudi hata nchi sakafuni, wakaabudu, wakamshukuru BWANA, wakasema, “Kwa kuwa ni mwema kwa maana fadhili zake ni za milele” (2Mambo ya Nyakati7: 1-3). Juma lililofuata ilikuwa sikukuu ya vibanda na jinsi ilivyo sherehekewa kwa furaha katika mwaka ule, kwani watu walikuwa wenye furaha na kuchngamka mioyoni mwao kwa wema wote ambao BWANA alimfanyia Daudi, na Sulemani, na watu wake Israeli (2 Mambo ya Nyakati 7:10).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni