Jumamosi, 19 Agosti 2017

IBADA KUU MBINGUNI


Ufunuo 5:6-14
Biblia inafunua ibada kuu inayoendelea mbinguni ambayo washiriki wa ibada hiyo ni wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne,
-     Wenye vinubi na vitasa vya dhahabu vyenye maombi ya watakatifu, wakiwa mbele za kiti cha enzi cha Mungu.
-     Viumbe hawa wapo hapo kufanya ibada maalum ili kumwabudu na kumpa sifa Mwanakondoo,
-      wanafanya hivyo kwa kuimba wimbo mpya wenye sifa kwa Mwanakondoo kisha malaika wengi, elfu kumi mara elfu kumi, elfu mara elfu, ambao wamekizunguka kiti cha enzi wanajiunga katika SIFA hizo. Uf 4.8-11
-     Hapa ndipo ibada hii kuu inaanzia, ambapo wenye uhai wanne wasiopumzika mchana na usiku wanamsifu Mwanakondoo wakisema Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu na kusababisha wazee ishirini na nne kuanguka chini na kumsujudia aliye Hai milele na milele,
-     huku wakivua taji zao na kuzitupa mbele ya kiti cha Enzi, wakisema, Umestahili wewe Mungu kupokea utukufu na heshima na uweza kwakuwa ndiwe uliyeviumba vitu vyote kwa sababu ya mapenzi yako vilikuweko navyo vimeumbwa.

Kisha kwa sauti ya pamoja wanasema: Anastahili kupokea uwezo, utajiri, hekima, nguvu, heshima, utukufu, na Baraka Mwanakondoo aketiye kwenye kiti cha enzi.
Maneno haya saba ni sifa kuu kwa Yesu ambaye ni Mwanakondoo wa Mungu.
Hatimaye baada ya ngurumo hizo za sauti ya sifa, kila kiumbe kilichoko mbinguni, duniani, na baharini vikamsifu Mwanakondoo,
-     na wote wakaanguka wakamsujudia Mwanakondoo. Sifa hii ikatikisa ulimwengu,
-     ulimwengu mzima ukamwabudu Mwanakondoo, Ibada hii haifanywi kwa mtume, nabii, malaika ,miungu wala kwa mwanadamu bali Ibada hii inamlenga Yesu Mwanakondoo.
-     Ibada inayofanywa kwa mtu mwingine mbali na Yesu siyo Ibada ya kweli na Mungu haisikilizi.
-     Inasikitisha kuona Ibada za mamilioni ya watu hazisikilizwi na Mungu kwa kuwa zinafanywa nje ya kumwabudu Yesu.
-     Katika Zaburi 98:1-9 na 96:1-8 Mfalme Daudi anatoa mwaliko wa kumwabudu Bwana kwa wimbo mpya kwa sababu Bwana Ametenda mambo ya ajabu,
-     Daudi anasema, “Inueni sauti, imbeni kwa furaha,
-     Nayo mito ipige makofi, na kulibariki jina lake,
-     Na kutangaza wokovu wake,
-     Kwa kuwa Bwana ni mkuu na mwenye kusifiwa sana.
Wito huu ni wito wakumwabudu BWANA peke yake.
Paulo naye anatia mkazo wa kumwabudu Mungu kwa kutoa mwongozo jinsi ya kufanya ibada katika roho ya uimbaji anasema
Neno la Kristo likae kwa wingi mioyoni mwenu (ndani yenu) katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Mkisemazana kwa zaburi na tenzi, na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Mungu mioyoni mwenu, nakumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo” (Kol 3:16-17),

Ef 5:19-20.
-     Ibada ya kweli ni ile inayomlenga Yesu na si vinginevyo.
-     Unaweza kuona jinsi mwanadamu anavyotoa muda wake, nguvu na mali katika ibada hewa kwa viumbe na sanamu, badala ya kumfanyia Mungu ibada katika Kristo Yesu,
-     wito huu ungali na nguvu ile ile kwetu kumgeukia Mungu na kujiunga na viumbe hawa wa mbinguni kumfanyia ibada sahihi Mwanakondoo.
-     Mungu ni mtakatifu na wa haki hana kigeugeu na habadiliki, ni mwadilifu.
-     Hawezi kuweka njia tofauti tofauti za kumwabudu kwa kila mtu.
-     Hiyo ingekuwa sawa na wasafiri wawili waendao mji mmoja lakini kwa njia tofauti zinazoweza kuwafikisha pale waendapo,

-     hilo haliwezekani kwa Mungu maana ni Mtakatifu, kwa utakatifu huo, Mungu ameweka njia moja ya kumwabudu ambayo ni Yesu Kristo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni