Jumamosi, 19 Agosti 2017

UMUHIMU WA IBADA YA KWELI

               
UMUHIMU WA IBADA YA KWELI
Ibada ya kweli ambayo ni BORA ni pale tunapomgusa MUNGU katika ENZI YAKE kwa roho ya unyenyekevu na kupondeka kwa moyo. (Zab 100:1-4)
-     Zaburi hii inatuonyesha njia nzuri ya kumwabudu Mungu na kuhimizwa kumfanyia Bwana shangwe, sifa na shangwe ni stahili ya Mungu.

Uimbaji wa sifa – ni ufunguo Mkuu wa kuingia ndani ya nyumba ambamo Mungu yumo (ibada ni huduma, na kuabudu ni kazi) kuabudu ni utumishi angalia anavyosema
-     Mtumikieni Bwana kwa furaha Njooni mbele zake kwa kuimba
-     Huwezi kuingia ndani ya nyumba pasipo kufungua mlango lazima uwe na ufunguo.
Kama Zaburi ya 100 inavyosema Ingieni malangoni mwake kwa kusifu na kwa kushukuru.
Isaya 1:12 Naye anasema,
“Mjapo ili kuonekana mbele zangu, ni nani aliye taka neno hili mikononi mwenu, kuzikanyaga nyua zangu?”
Mungu anauliza mnapoingia nyuani mwake Kwa utaratibu upi maana huwezi kukanyaga nyua za Bwana kiholela, hapo ni Ikulu pana heshima yake na jinsi ya kuingia. Mungu kama Mfalme yumo ndani ya ikulu, nyumba yake, hekalu, yaani mahali palipowekwa wakfu kwa Ibada.

Tunapaswa kwenda hapo na ufunguo.
“Jueni Bwana ndiye Mungu, ametuumba na sisi ni watu wake na kondoo wa malisho yake”. Zab 100:1-4
-     anasema kwa msisitizo, Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru,
-     haya ni malango ya hekalu (hekalu la kale) Nyuani au barazani mwake kwa kusifu na kwa kushukuru na kuhimidi Jina lake.
-     Uimbaji ndiyo ufunguo wa malango ya Bwana kuingia barazani pake, Hodi yetu ni sifa, kuimba na kushukuru kunatupa kibali cha kuingia patakatifu pa patakatifu.
Kanisa na Mkristo asiyeimba na kusifu ni bubu, kamwe hawezi kuingia na kumwona mfalme Barazani pake. Mkristo huyo amekosa ufunguo hawezi kujieleza, hana shangwe, hana shukrani ni kama mtoto mchanga aliyezaliwa wodi ya wazazi lakini bado hajalia, ana kasoro ni kilema, ipo hatari ya kupoteza maisha.
-     Hivyo hivyo mkristo asiye na ufunguo huo atapoteza maisha ya kiroho, ibada ya kweli yenye funguo hizo ni uhai wa Mkristo.
-     Kusifu na kuabudu kunaonyesha uhai wakati tunapomwimbia nyimbo za sifa na shangwe namshnagaa mtu wa aina hiyo ambaye haabudu maana hana uhai.

INJILI ilienezwa kwa nyimbo katika karne ya 17 huko ulaya – Martin Luther, John Wesley, John Calvin, John Hus, John Wyclife walitumia nyimbo kuhubiri neno. Kwa sababu kuna nguvu yenye uhai wa Mungu katika sifa. Katika Mathayo 26:26-30 Hapa Yesu aliimba pamoja na wanafunzi wake, aliimba Zaburi 115 hadi 118. Zab 89:5-7 inasema mbingu zitayasifu maajabu yako na uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Hii inaonyesha kwamba walioko mbinguni wanaabudu.
-     Kutojali na kudharau uimbaji ni kumdharau Yesu ambaye aliimba –
-     ni kupoteza ufunguo mkuu ambao hufungua nyumba na baraza la Mungu.
-     Kumbuka Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu.
-     Baraza la watakatifu ni pale watakatifu wanapokusanyika kuabudu Mungu.
Katika 1Kor. 14:26 Paulo anasema mkutanapo pamoja kila mmoja ana Zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri, mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Hizi ndizo faida za kuwepo barazani pa watakatifu, na umuhimu wa ibada ya kweli, Vidokezo vya msaada unaopata unapoimba:
a.   Unawezeshwa kujieleza kwa undani jinsi unavyompenda na kumwabudu Mungu
b.   Uimbaji unakupa ufasaha wa kumsifu Mungu kwa furaha na uchangamfu.
c.    Utakaso na toba huambatana na kuimba bila kizuizi.
d.   Unawezeshwa kumfanyia Mungu ibada kama alivyo kuagiza na kwa wepesi.
e.   Ibada huongozwa na kuendeshwa vema kwa muziki na kumwabudu Mungu kwa utamu na kwa raha.
f.    Unawezeshwa kuonyesha upendo wako tena baada ya maungamo na ukiri wako kwa Mungu na kudhihirisha kwamba moyo wako umefunguliwa na umewekwa HURU.

Dondoo hizi ni nyenzo za muhimu kutusaidia kumwabudu Mungu ili tusipungukiwe na kukosa neema na Baraka zake zilizomo barazani mwake. Ingia na uzichote baraka kwa funguo ulizojifunza na utazipata tu kadiri unavyonyenyekea moyoni mwako.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni