Jumatano, 8 Agosti 2012

SOMO : KUNYAMAZA KIMYA



MWL Furaha Amon


Utangulizi

Kuabudu ni jambo pana sana kuliko watu wengi wanavyo lifahamu. Watu wengi wanafikiri kuabudu kunaishia kwenye kitendo cha kufanya ibada au misa peke yake. Ibada au misa ni sehemu ndogo sana katika kuabudu. Kuabudu ni maisha unayoishi. Kuabudu ni maisha unayoishi. Kuabudu ni kuishi maisha fulani. Kuabudu ni mtindo fulani wa maisha ambayo Yule Mungu unayemwabudu anakutaka uyaishi. Hivyo siyo swala la kwenda  kanisani kwenye ibada au misa na ukishaondoka huko kila kitu unakiacha kanisani. Mungu unayemwabudu anakutaka uishi maisha ya aina fulani hata unapokuwa nje ya ibada, huwezi kuishi maisha ambayo hayafanani nay ale anayoyataka unayemwabudu halafu wewe ukazingatia ili mradi unahudhuria katika misa na ibada peke yake. Kuishi maisha yale anayoyataka Mungu huko ndiko kumcha Mungu. Kwa maana hiyo sehemu kubwa ya kuabudu Mungu iko nje ya nyumba za ibada zetu. Ni jinsi unavyoishi na watu huko nyumbani kwako, majirani zako, mtaani kwako, kazini pamoja na sehemu mbalimbali za maisha ya kijamii. Mungu wetu ana jinsi fulani ya anavyotaka watu wake waishi huko katika maisha ya nje na ibada. Hebu tuangalie mfano wa mambo machache tu yafuatayo;-


Biblia inasema,
Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao (Waebrania 12:14).
Mcha Mungu anatakiwa asiwe na ugomvi, chuki, kinyongo na mtu yeyote. Na kama hali kama hiyo inajitokeza ni lazima ahakikishe anatafuta kwa bidii kuwa na amani na huyo mtu hata kama mazingira yanakataa.
Biblia inasema,
Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi, nanyi mtakuwa wana wa aliye juu. Kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi iweni na huruma, kama baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa (Luka 6: 35-38
Upendo wa mcha Mungu sio wa hiari bali ni amri wala siyo ombi. Utake usitake Mungu anatulazimisha tuwapende watu wote pamoja na adui zetu.
Biblia inasema;-
Heri mtu Yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala hakusimama katika njia ya wakosaji wala hakuketi barazani pa wenye mizaha (Zaburi 1:1).
Hayo ni maisha anayotakiwa kuishi mcha Mungu. Mambo hayo niliyoyataja ni baadhi tu ya mtindo wa maisha ambayo Mungu anataka tuishi. Kuna mambo mengi ambayo Mungu anamtaka mtu anayemcha Mungu aishi kwa hayo.
Madam Vick Shedafa
Hivyo kuabudu Mungu siyo ibada peke yake bali ni aina ya maisha. Hivyo kwa kifupi ni kuwa, kuabudu siyo ibada pekee, bali hata katika maisha ya nje ya ibada. Lengo la somo hili ni kuzungumzia kumwabudu Mungu katika ibada ya maombi. Zaidi nitazungumzia kumwabudu Mungu kwa maombi baada ya mwombaji kufika kileleni katika maombi yaani Patakatifu pa patakatifu. Kabla ya kuedelea mbele kwanza nigusie kidogo kuhusu ibada. Ibada ni lazima iwe katika kiwango cha patakatifu pa patakatifu. Hii ndiyo ibada ambayo Mungu atakutana na shida za watu. Ibada inapokuwa ya mwilini au kwenye nafsi, Mungu hawezi kukutana na shida za watu. Baada ya mwombaji kufika patakatifu pa patakatifu anakuwa amefika kwenye kiti cha enzi, yuko mbele za Mungu. Mungu ametuumba ili tumwabudu. Hivyo Mungu anachokihitaji kwetu ni kumwabudu. Unapofika patakatifu pa patakatifu Biblia inasema, kabla hujaomba nalikusikia. Hivyo hakuna haja ya kuanza kueleza shida zako mara ufikapo patakatifu pa patakatifu. Mungu anataka tumwabudu siyo wakati wa kumueleza shida zako. Unapofika patakatifu pa patakatifu majaribu yote uliyonayo huyeyuka yenyewe.
Madam Lilian Kimola
Lengo la kufika patakatifu pa patakatifu ni kukutana na Mungu ili tumwabudu. Unapomwabudu Mungu, yeye naye anajua wajibu wake kwa watu wake, hivyo naye anashughulikia shida zako. Kumwabudu Mungu kwa njia ya ibada, kuomba au kuimba ni kukiri ukuu wake, kumtukuza, kumwinua, kumbariki, kumshukuru, kumtukuza kwa matendo makuu aliyokwisha kuyatenda, nk.
Unaweza kumwabudu Mungu kwa kuzungumza yaani kwa kusemelea maneno ya kumtukuza Mungu, n.k. unaweza kumwabudu Mungu kwa kuimba nyimbo za kumtukuza zenye mahadhi ya kuabudu.
Ukifika patakatifu pa patakatifu unakuwa uko mbele za Mungu. Wakristo wengi waombaji wa kiwango cha kufikia patakatifu pa patakatifu wanajua aina moja tu ya kuwa mbele za Mungu wakati mtu akiwa katika maombi, aina hiyo ni ya kusemelea maneno kwa Mungu au njia ya kuimba nyimbo za kuabudu. Pamoja na njia hiyo inayojulikana sana, kuna njia nyingine, njia hiyo ni KUKAA KIMYA  baada ya kupata mpenyo, unaweza ukasikia Roho Mtakatifu anakutaka ukae kimya mbele za Mungu. Siyo kwamba ukatishe maombi bali uendelee kuwa katika uwepo wa Mungu lakini ukiwa kimya. Usiombe, usihofu bali uwe kimya. Hapo ni kumtafakari Mungu na kusikiliza kutoka kwake.
Biblia inasema;-
Nyamazeni, ninyi wenye mwili, mbele za Bwana kwa maana ametamka, na kutoka katika maskani yake takatifu (Zakaria 2:13).
Kuna wakati Mungu hataki tuzungumze tukiwa mbele zake, hasa anapokuwa tayari ameamka kutupigania. Hivyo utakapoona tayari ameamka kutupigania, hivyo utakapoona Roho Mtakatifu anakutaka kukaa kimya, ujue uko kwenye mpenyo wa kiwango cha hali ya juu. Tendo la kumwamsha Mungu ni tendo kuu sana. Hivyo wakati Mungu ameamka, mtu mwingine hatakiwi kuzungumza. Hii inafanana hata na wakati wa wana wa Israeli Mungu alipowapigania katika bahari ya Shamu, ambapo wana wa Israeli walikuwa wamemlilia Mungu sana kufuatia jaribio la Farao na majeshi yake, kuwarudisha Misri ili wakaendelee kuwatumikia.
Biblia inasema;-
Musa akawaambia watu, msiogope simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya (Kutoka 14:13-14)
Hivyo wana wa Israeli walinyamaza kimya. Mungu alifanya maangamizi makubwa kwa adui. Maandiko yanaendelea kusema
Lakini BWANA yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake (Habakuki 2:20).
Huwezi kukaa kimya mbele za Mungu ukiwa mwilini au kwenye nafsi. Mungu yupo patakatifu pa patakatifu, wewe unatakiwa ukae kimya. Hivyo kitendo cha kukaa kimya ni kitendo au ni tukio linalofanywa na mtu ambaye yuko patakatifu pa patakatifu hivyo baada ya kupata mpenyo ndipo unaweza kukaa kimya. Hii ni kusema kuwa, unapokaa kimya wakati uko patakatifu pa patakatifu ina maana unakuwa unamwabudu Mungu.

Ukimwabudu Mungu ukiwa kimya ikiwa Roho Mtakatifu atakuongoza kufanya hivyo,kuna upako mkubwa sana ambao unashuka ndani yako sawasawa na kumwabudu Mungu kwa njia nyingine baada ya kupata mpenyo. Upako unaoshuka wakati unamwabudu Mungu kwa kukaa kimya unaweza kuwa mkubwa kuliko ule wa aina nyingine. Maana wakati huo Mungu husimama na huwa katika kukutendea au kukupigania kwa nguvu zake zote.
Hivyo using’ang’anie kumwabudu Mungu kwa kuimba nyimbo za kuabudu au kusemelea maneno tu, hivyo hata kama itatokea Roho Mtakatifu amekuongoza kukaa kimya wewe kaa kimya bado ni maombi yenye nguvu tena ya kiwango cha patakatifu pa patakatifu.
Biblia inasema,
Ukae kimya mbele za BWANA, nawe umngoje kwa saburi (Zaburi 37:7)
Kunyamaza mbele za Mungu, ni muhimu wakati mwingine ni kungoja jibu au maelekezo kutoka kwa Mungu, waombaji wengi wanataka kuwa wasemaji wakuu wanapokutana na Mungu. Wao hawataki kumpa Mungu nafasi ya kuzungumza nao, ili nao wamsikilize. Biblia inasema, njoo tusemezane. Mungu anataka tusemezane naye. Hivvyo huko ni kusema kuwa, umpe nafasi, Mungu naye aseme mbadilishane mawazo.
Biblia inasema;-
Bali wao wamgojeao BWANA watapata nguvu mpya (Isaya 40:3)

Unapokuwa kimya mbele za Mungu, unamgoja Mungu akupe nguvu mpya juu ya jaribu, shida, n.k. uliyonayo. Unapokuwa umekaa kimya unamtafakari Mungu, unamwabudu kwa kumtafakari ukuu na uweza wake.

MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUFUATILIA SOMO HILI









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni