Jumatatu, 17 Februari 2014

USHUHUDA MKUBWA WA MOHAMED




Mohamedi wa kabila la Fulani alianza kufuga mifugo alipokuwa na umri wa miaka sita. Alifanya hivyo kwa miaka kumi hivi mpaka alipoenda kwenye shule ya kiarabu kujifunza zaidi Kurani. Kabla ya hapo, Mohamedi alikuwa amejifunza juu ya Uislamu kutoka kwa baba yake.
Baada ya miaka kadhaa ya kjifunza hapo shuleni, alirudi nyumbani. Usiku mmoja aliota ndoto ya kuogofya sana. Aliona watu kandokando ya barabara waliokuwa wakipata shida. Aliingia ndani ya geti moja na watu walimchukua na kuanza kumpiga. Kisha akafungiwa kwenye chumba kilichokuwa na joto kali. Ilikuwa ni joto kali kiasi kwamba mwili wake ulianza kuchunika kama vile kujivua magamba. Na alipoanza kupiga kelele na kuupiga mlango teke ili uweze kufunguka, mara akaamuka toka usingizini. Hakuweza kulala tena usiku ule. Usiku uliofuata alipata ndoto nyingine. Safari hii alikuwa kwenye barabara nyingine na aliona miili iliyooza. Alienda kwenye geti lile lile, alipigwa na kuchukuliwa kwenye chumba kile kile. Ngozi yake iliyeyuka mwilini wakati mtu mmoja aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alipomtokea. Ghafla chumba kikawa na ubaridi mzuri na wale watu waliokuwa wakimpiga wakatoweka. Mtu yule alinyosha mkono wake na kuishika mikono ya Mohamedi na kusema: “Mwanangu, unafanya nini hapa? Je, unapenda nikupeleke nyumbani?” Mohamedi akasema: “Ndani ya sekunde moja nilikuwa nimesharudi nyumbani na aliniambia, ’Ninakupenda mwanangu.’”
Wiki mbili baadaye Mohamedi alipata ndoto ya tatu. Alikuwa porini na hapo palikuwa na shimo refu mbele yake na hakujua jinsi ya kulivuka. Alipoangalia ndini yake aliogopa zaidi na akafikiri kuwa pengine angetumbukia ndani yake na kufia humo. Akamwona mtu amevaa nguo nyeusi akitembea haraka. Mtu huyu alimwambia kuwa simba alikuwa akija nyuma yake Mohamedi na kwamba ili kujiokoa alitakiwa aliruke shimo lile kabla ya simba kumfikia. Mohamedi akamsikia simba akinguruma. Mara tu alipotaka kuliruka shimo lile, mtu mwingine aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alitokea mbele yake. Mtu huyu ni yule yule aliyemwona kwenye ile ndoto iliyokuwa imetangulia, akamwuliza hivi: “Mwanangu unaenda wapi?” Mtu yule mwenye vazi jeusi akawa ametoweka na ngurumo ya simba ikakoma. Mohamedi akamwambia mtu yule mwenye vazi jeupe kuwa alikuwa akienda nyumbani. Akamwuliza Mohamedi kama anahitaji msaada. Mtu yule mwenye vazi jeupe alinyosha mguu wake juu ya shimo lote. Alipofanya vile, shimo lile likafukiwa kabisa. Kisha akamwambia Mohamedi apite juu yake na aende nyumbani. Walipokuwa karibu na nyumbani kwake Mohamedi mtu yule alisema: “Ninakupenda mwanangu.”
Kwa siku sita mfululizo kila usiku, alipata ndoto zilizofanana. Kila wakati alijiona yuko katika sehemu tofauti tofauti, bila kujali mahali alipokuwa, mtu yule yule aliyekuwa amevaa nguo nyeupe alikuwa akija na kumsaidia. Katika ndoto ya mwisho ya tisa, alijiona amekaa chini ya mti akisoma vitabu ambavyo hakuweza kuvielewa. Mtu yule mwenye nguo nyeupe, yaani YESU alikuwa amekaa pembeni mwake. Alimwuliza: “Je unasoma juu ya nini?” Naye akamjibu kuwa alijaribu kuongeza ujuzi. Yesu akamwuliza Mohamedi kama alitaka msaada na kwamba angeweza kumwonesha mambo maalumu ya kusoma. Yesu alichukua kitabu kile na kusema: “Kitabu kinatoka kwa Bwana na kina ujumbe wa Mungu ndani yake. Katika kitabu hiki nitakuonesha mistari itakayokusaidia wewe.” Yesu alimsomea maandiko Mohamedi, pamoja na Yohana 14:6, kinachosema hivi: “Mimi ndimi njia, na kweli na uzima. Mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi.” Alimfafanulia na kumwambia kwamba Yeye Ndiye njia, na Mwokozi wa Ulimwengu. Pia Bwana Yesu alimwambia kuwa atapitia majaribu na mateso mengi baada ya kuwa Mkristo. Akamwambia kuwa alitaka awe Mwokozi wake na kumwelezea kwamba yeye ndiye aliyekuwa mtu yule katika ndoto zake, mtu aliyemkomboa au kumsaidia. Bwana Yesu alipomwambia kwamba alitaka ampe wokovu, na kumwuliza: ”Je unaupokea?” Mohamedi akasema “Ndiyo” na Yesu akatoweka.
Siku iliyofuata Mohamedi alimwendea Mkristo mmoja aliyefahamiana naye akamwambia juu ya ndoto hii. Huyu rafiki alimtambulisha kwa vijana wengine kutoka katika kanisa lingine na wakamwongoza Mohamedi kumpokea Yesu. Aliwaambia wazazi wake kuwa sasa yeye amekuwa Mkristo. Baada ya miezi kadhaa, Baba yake Mohamedi alimlazimisha kunywa sumu. Aliwaagiza watu wengine kutoka pale kijijini kumzunguka Mohamedi ili asiweze kukwepa ama kukimbia. Cha ajabu ni kwamba siku mbili kabla ya siku ile Yesu alikuwa amemtokea Mohamedi na kumwambia kuwa japokuwa atapitia magumu atakayokutana nayo, Yesu mwenyewe atamfanyia njia ili aweze kutoka. Hivyo Mohamedi alimwomba baba yake kama anaweza kuomba kwanza kabla ya kuinywa ile sumu. Aliomba kisha akainywa ile sumu, na akaenda kulala. Asubuhi iliyofuata, baba yake alishangaa sana alipomwona Mohamedi alikuwa hai! Hata hivyo baadaye watu wa familia yake walijaribu kumwua kwa kumlenga na mshale wenye sumu! Alilazwa wiki moja hospitalini, hata hivyo alipona vizuri!
Baada ya majaribio hayo ya kumaliza uhai wake, familia yake walipanga mikakati mingine kwa kumshawishi aache Ukristo. Baba yake alimpa ng’ombe mia moja na akamwambia kuwa angeweza kumwoza wanawake watatu kama angeachana na imani ya Kikristo! Hatimaye, Mohamedi alifanya uamuzi – lakini ilikuwa ni kuiacha familia yake hapo nyumbani. Alimshukuru baba yake kwa kundi kubwa hilo la ng’ombe, na nafasi ya wanawake hao watatu. Kisha akamwambia baba: “Bado hujafikia kile kiwango ambacho Bwana Yesu aliniahidi mimi kupata, ikiwa utaniahidi na kunipatia ahadi hizo itakuwa sawa kwangu. Je una uwezo wa kunipatia mimi uzima wa milele?” Baba yake akasema: “Hapana.” Kwa vile hataweza kumpatia uzima wa milele, hivyo kwa vyo vyote vile asingeweza kumwacha Yesu Kristo!
Miaka michache baadaye, Baba yake Mohamedi alipolala taabani karibu na kufa alimwomba msamaha Mohamedi na akasema kuwa, na yeye sasa alikuwa tayari kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wake. Mohamedi alimwongoza baba yake sala ya toba na baada ya masaa matatu alikufa. Kwa upande mwingine kifo cha baba wa Mohamedi lilikuwa ni tukio la huzuni, lakini bado katika upande mwingine, ilikuwa ni sababu ya furaha. Siyo tu kwa vile baba na mwanawe wamepatana kabla ya baba mtu kuiaga dunia, ila aliiaga dunia kwa amani, akijua kuwa katika ulimwengu ujao, atakuwa pamoja na Yesu milele yote, na – baadaye kwa siku za usoni - atakuwa na mwanawe tena mbinguni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni