Ijumaa, 6 Mei 2016

LUGHA INAVYOWEZA KUTUMIKA KIROHO




LUGHA
Lugha ni kitu ambacho kinaweza kuwatambulisha watu na aina ya watu kulingana na kundi wanaloliwakilisha. Kwa maana hiyo unaweza kumtambua mtu na kundi lake kutokana na lugha anayoitumia.

Kuna lugha wanayoitumia watu wa dunia ambayo inawafanya wafanikiwe katika mambo ya dunia. Hali kadhalika tukiokoka tunapata lugha nyingine yaani ipo lugha ambayo ni tofauti na ya dunia ambayo inatufanya tufanikiwe katika mambo ya kiroho.

Ukiingia na lugha za dunia ndani ya wokovu huwezi kupata mpenyo katika mambo ya kiroho. Hii ni kwa sababu ndiyo inatambulisha watu na mfumo wao wa maisha.

Lugha inakuwezesha kutambua aina ya mtu unayeongea naye, lugha au maneno ya mtu hutengeneza taswira fulani ya maisha ambayo huumbika na hatimaye huja kutokea kweli.

Watu wengi hapa duniani wanaishi maisha ambayo waliyafikiria na kuyasema kabla hayajakuwa dhahiri. Unaposema sana juu ya jambo fulani, hatimaye jambo hilo huumbika na hatimaye hutokea hata kama hukulitaka.
Nguvu ya roho mtakatifu na roho chafu hutegemea sana mambo matatu ambayo ni;-
1.  Neno
2.  Imani
3.  Ukiri
Tukianza na neno, tunajifunza kwamba neno ni kama mwongozo wa jambo au ni kama katiba, ambayo ndani yake kuna maelekezo ya haki yako na wajibu wako kwa unayehusiana naye.

Kama vile ambavyo Mungu hutumia kitabu chake Biblia lakini pia hata shetani ana vitabu vyake anavyotumia ingawa pia shetani anaijua vizuri sana Biblia na haki za mtu aliyeokoka.
Katika matendo 19:18 – 20 tunaona habari kwamba kuna watu waliokuwa wanatumia vitabu kwa uganga wakavikusanya na kuvichoma.

IMANI.
Imani ni kuwa na uhakika wa jambo unalolitarajia, na katika mambo ya kiroho imani ni kitu cha lazima sana, hata wachawi hutumia imani ya kiwango cha juu sana katika kufanya kazi zao za kichawi. Hebu fikiria mwenyewe mtu anakaa kwenye ungo na anafanya mambo yake na hatimaye ungo unapaa na kuelekea anakotaka, jambo hili huwezi kulifanya kama una imani ya kubahatisha.

UKIRI.
Ukiri au usemi ni wa lazima sana katika mambo ya kiroho, unaweza kuwa una neno, na pia una imani ya kutosha, lakini bila kusema hakuna kinachoweza kufanyika. Maneno tunayokiri yana nguvu kubwa sana na ukiitumia vizuri ni lazima ushinde.

Wakati mfalme Daudi  anapambana na Goliathi, pamoja na Goliati kumuona Daudi kuwa ni kijana mdogo mwenye uso mzuri, lakini Goliati kuna maneno ambayo alimsemea kwamba angemuua na kuwapa ndege nyama yake.
Daudi naye wakati anamwendea Goliati naye alisema maneno ambayo yalikuwa mengi kuliko aliyoyasema Goliati, na aliahidi kukata kichwa chake na kwa upanga ijapokuwa hakuwa na upanga bali alikuwa na kombeo tu, lakini maneno yake yalitimia na akamkata kichwa Goliati kwa upanga wake mwenyewe.

Kila mara kabla ya ugomvi kutokea mara nyingi huanza na maneno, na mwenye maneno mengi mara nyingi hushinda , angalia hata kwa mabondia au wanamieleka.

Wakati wa vita vya kagera pia kulikuwa na maneno kabla ya vita kuanza. Idi Amin dada wa Rais wa Uganda wakati ule alisema atahakikisha chai anakunywa Mwanza, chakula cha mchana Dodoma na chakula cha usiku Dar es salaam. Amin hakufafanua atawezaje kufanya mambo hayo bila kutueleza ana uwezo kiasi gani.

Lakini kwa upande wa Tanzania Rais wa wakati huo mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiongea na wazee wa Dar es salaam katika ukumbi wa Karimjee alisema maneno machache kwamba sasa tunampiga Amin, uwezo wa kumpiga tunao, nia ya kumpiga tunayo, na sababu za kumpiga tunazo.  Tunataka dunia ituelewe hivyo.

Na matokeo yake idi amini alipigwa na utawala wake kuangushwa.
Kwa sababu hiyo lugha zetu na za watu wa dunia ni lazima zitofautiane ili tuweze kufanikiwa katika mambo ya Mungu.
Ni lazima tujitofautishe na watu wa dunia wanavyokiri kuhusu uchumi, maisha, biashara, nk.

Hii ni kwa sababu lugha ndiyo inayotumika kusukuma nguvu ya Mungu, ni lazima tujue Biblia inatagiza kufanya nini kwa mfano tunapokuwa katika hali ya hasira, tukiwa na majirani, kazini, nyumbani kwenye familia n.k.
Biblia natuambia katika kitabu cha Mwanzo 11: 1 – 9 kwamba nchi yote ilikuwa na lugha moja na watu hawakutaka kutawanyika.

Waliamua kujenga mnara mrefu ufike mbinguni ili wasitawanyike. Walijenga mnara huu kwa kutumia lami na matofali, na Mungu alijua kwamba watafanikiwa kwa sababu ya hamasa waliyokuwa nayo. Kwa kawaida tulitegemea kwamba Mungu angewanyanganya lami na matofali, lakini hapana Mungu aliamua kuchukua lugha yao nah ii iliwafanya wasambaratike.

Nguvu ya watu hao haikuwa katika katika lami na matofali bali ilikuwa katika lugha na katika usemi, na Mungu alijua hakika kwamba wangefanikiwa. Kwa sababu ukiri wao ulikuwa katika usemi.

Angewanyanganya lami na matofali wangeweza kushauliana cha kufanya ili ujenzi wa mnara uendelee.
Lugha ndiyo inaymtambulisha mtu ni nani na ni wa kundi gani, kwa kutumia lugha unaweza kumjua kahaba, msomi, ameokoka n.k. kwa sababu lugha ndiyo inayomtambulisha mtu na kundi lake, lugha ndiyo inayomtambulisha mtu 

kama ni wa kufa au ni wa kuishi.
Katika kitabu cha Waamuzi 12: 5 – 6 kuna habari ya vita kati ya Wagileadi na Waefraimu na kuna askari aliyejichanganya na walimgundua kutokana na usemi, alishindwa kutamka neno shibolethi akasema siboleth.
Wakati wa matatizo ya Ayubu katika kitabu cha (Ayubu 2:9-10) Ayubu alimwambia mke wake ameongea kama  wanawake wapumbavu, kumbe wanawake wapumbavu nao wana lugha zao.

Katika injili ya Mathayo 26 tunasoma habari za Petro kwamba lugha yake ilimtambulisha kwamba yuko na Yesu.
Ukitaka kumshinda shetani ni lazima kwanza ubadilishe lugha unayotumia wakati unapoongea naye, huwezi kumshinda shetani kwa kutumia lugha yake.

Mithali 6: unakamatwa na maneno yako mwenyewe, katika kitabu cha Waamuzi 15:7 Samsoni alijiapiza kwa sauti kwamba atawapiga Wafilisti halafu atakoma.
Ni vizuri kwa waliookoka wakajifunza kwamba wasikubali kuwaacha watu wanawaongelesha mambo ya ajabu na wakakaa kimya
Mzee anapomwambia mtoto mchumba anamfunika katika ulimwengu wa roho .
MUNGU AKUBARIKI KWA KUFUATILIA SOMO HILI.
Furaha Amon   - Tanga  Mob: 0713 461593


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni