1. Muziki ni nini?
Muziki ni sanaa inayoishi iliyo hai ambayo inadumu mpaka
ulimwengu ujao katika umilele. Huduma zingine zote zitakomea hapa duniani bali
muziki hautokoma utakuwepo milele na milele.
“Na hao waliokombolewa na BWANA
watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa
vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia”. (Isaya 35: 10)
Msitari huu unahusu watu waliokombolewa kwamba wataimba
milele!
- Furaha ya milele, ni kiashirio cha uimbaji wa watu hawa kwamba wataimba
milele.
- Muziki Ni lugha ya kiulimwengu inayozungumza na hisia za mtu yoyote,
- lugha hii hueleweka na msikilizaji, kwa kuguswa utu wake na fahamu,
kisha nafsi, moyo, akili na mwili.
- Haijalishi lugha iliyomo katika
wimbo, muziki, kwamba unajua au la,
- Mawasiliano sahihi yanakuwepo na kueleweka katika hisia za msikilizaji.
Muziki una nguvu ya kuleta amani na furaha moyoni,
burudiko na pumziko la akili kiasi cha kumshawishi mtu kukubali nakujiachia
katika mivuto yake.
Nguvu ya muziki imeujaza ulimwengu na kupenya katika
utamaduni wa kila kabila, taifa, jamii, na lugha, hii inaonyesha muziki hauna
mipaka.
Muziki umesafiri bila kizuizi kwa njia za mawasiliano ya
vyombo vya habari popote ulimwenguni. Ni vigumu kwa mtu kujizuia kuitikia mara
asikiapo muziki ukiunguruma,
- muziki ni chakula cha masikio na ubongo, muziki mtamu unapoingia
masikioni mwa msikilizaji hupenya kwenye akili zake,
- na akili zake huusukuma mwili na kuanza kutikisa kichwa, miguu, mikono
na kiwiliwili, na kucheza, kutokana na utamu wa wimbo na ujumbe wa wimbo huku
akirukaruka kufuata midundo ya muziki unaopigwa.
Katika zama zetu, muziki umekuwa ni utambulisho wa taifa
na heshima ya nchi, kila nchi duniani ina wimbo maalumu wa Taifa ambao huimbwa
kuutukuza utaifa na heshima ya Taifa.
- Kila wakati tukio la kitaifa, wimbo huo huimbwa,
- mgeni anapotembelea nchi, huimbwa
ambapo kila mtu aliye mahali hapo hutakiwa kusimama kimya huku akiimba wimbo
huo.
Hapa ni muhimu tuelewe kwamba muziki si uhuni, ama
kudhani kwamba ni kazi ya watoto, watu wasio na kazi au watu maskini, hapana
hiyo ni dhana potofu, na mtamzamo hasi dhidi ya muziki, tunapaswa kubadilika
kimtazamo na kuona utajiri uliomo katika muziki,
- Kwamba ni hazina tuliopewa na Mwenyezi Mungu kuwa urithi wetu.
- Na kumshukuru Mungu kwa vipaji na karama alizowajalia waimbaji na
wanamuziki wanaohudumia katika huduma hii ndani ya Kanisa la Kristo.
Dunia ingekosa muziki ingekuwa katika giza nene na maisha
yangekuwa butu katika nyanja zote. Muziki ni nyenzo fanikishi katika kuelimisha
jamii kwa jambo lolote kwa wepesi na kwa haraka, bila vikwazo ama vizuizi.
Biblia imejaa rejea nyingi za muziki, zaidi ya rejea 800
zinazungumzia muziki.
Huu ni ushahidi wa kutosha juu ya umuhimu
wake. Msisitizo huu wa maandiko unaonyesha wazi kwamba muziki ni huduma ya
kiroho kweli kweli, na kwamba Biblia ni kitabu cha nyimbo, pia ni kamusi ya
uimbaji wa kiroho kwa waabuduo, na kwamba kila rejea ya uimbaji itokane na
Biblia.
MUZIKI NI UHAI
Muziki ni uhai wa tamaduni, desturi, mila za jamii za
watu ulimwenguni, kila jamii ina mifumo na mitindo iliyojengeka tokea zama za
mababu zao wa kale, ambao waliachia maadili vizazi vyao vitakavyo kuwepo baada
yao.
- Historia hiyo ya maadili ilitunzwa na kuhifadhiwa katika nyimbo – muziki
umetumika kama Benki ya kutunzia maadili na tamaduni za utaifa.
- Benki hii ilifanya kazi kabla ya uvumbuzi wa kuandika vitabu kuweka
kumbukumbu za taifa na jamii husika.
- Haya tunayaona kwa Musa na wana wa Israeli Kumb. 31:29-, 32:1-44-47
Maandiko haya yanahusu Musa alipokuwa akiwaaga na kuwapa wosia Israeli kabla ya
kufa kwake.
- Akawafundisha wimbo wa wosia na
kuwaamuru wawaimbie watoto wao na watoto wao wawaimbie wimbo huo watoto wao na
kuendelea.
UFUNGUO WA KUABUDU NA KUSIFU
Zab: 100:1-4, 95:1-7
Mungu yuko mahali palipotukuka sana na kuinuliwa:
Hili linanipa wazo kwamba kuabudu na kusifu ni stahili ya
MUNGU, Biblia inasema.
“Maana yeye aliye juu aliyetukuka
akaaye milele ambaye jina lake ni Mtakatifu – anasema hivi; Nakaa mimi mahali
palipoinuka palipo patakatifu tena pamoja na yeye aliye na Roho iliyotubu na
kunyenyekea na kuifufua mioyo yao waliotubu.” (Isaya 57:15-16).
Hii ndiyo sifa na ufunguo unaotakiwa na Mungu.
Tutamkaribiaje Mungu kama huyu aliyeinuliwa na kutukuka sana?
1. Jibu linapatikana katika maandiko haya Zab 95:1-5
“Njoo tumwimbie Bwana Tuje mbele zake
kwa shukrani Kwakuwa Bwana ni Mungu Mkuu na mfalme mkuu juu ya miungu yote”.
Mikononi mwake zimo bonde za dunia , mikono yake iliumba bahari na nchi kavu
Katika mstari wa 6 mwaliko unatolewa
kwenda kumwabudu, kumsujudia kwa kumpigia magoti (kupiga magoti ni tendo la
kumkiri na kumtambua kuwa ni Mungu) Bwana aliyetuumba- Mungu wetu ambapo sisi
tu malisho yake na kondoo wa mkono wake (yeye ni Mchungaji).
Mungu hukaa na mtu aliyetubu na kunyenyekea, kamwe hawezi kukaa na
mwenye dhambi ingawa anampenda. Ibada ya mtu huyu itakubaliwa na Mungu Zab 96:9
Huu ni wito mwingine:
Mwabuduni Bwana kwa uzuri, na hofu ya utisho ndani ya moyo wa utakatifu
– tetemekeni mbele zake nchi yote. Utakatifu na hofu ni funguo za mlango wa
sifa na ibada ya kweli. Njia kuu kwa mwanadamu kumfikia Mungu katika enzi yake
ni kumpa shukrani na sifa anazostahili – tukishajitakasa kwa Toba
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni