Jumapili, 20 Agosti 2017

WAIMBAJI NA WANA MUZIKI




Bila shaka Mungu anabarikiwa sana na sauti za vyombo vya muziki unaopigwa kwa ustadi na mwanamuziki aliyejaa Moyo wa Sifa. Kwa hiyo wapigaji wa vyombo wanapaswa wajitunze katika usafi wa Roho na Mwili kama watumishi walio sawa na mchungaji au mhubiri anayehubiri kwa sababu watatoa hesabu yao mbele ya Kristo siku ile ya hukumu.
-     Inawapasa kukataa aina yote ya sifa na kiburi, bali wawe wanyenyekevu na wa pole mbele ya uongozi kama kwa Bwana mwenyewe.
-     Wasiotegemea ujuzi wao bali maombi na Roho Mtakatifu apewe nafasi kubwa katika huduma yao.
-     Muziki una mvuto wa nguvu kumnasa mtu katika majaribu na kumharibu pasipo yeye mwenyewe kufahamu.
-     Hivyo ni vyema kila mwanamuziki ajiweke wakfu kwa Bwana na kutaka nguvu za Roho Mtakatifu katika huduma yake, Ili akwepe mitego na hila pamoja na tamaa za mwili ambazo mara nyingi huwa zinawashambulia sana.
Lusifa alianguka baada ya kutukuka sana katika huduma ya sifa mbele za Mungu, maana alikuwa na vinanda mwilini mwake alivyotumia kumsifu Mungu kwa ustadi wa hali ya juu sana, kiasi kwamba malaika wote walimsikiliza na kutii alichosema katika ibada yao kwa Mungu. Uovu ukapata mwanya hapo na akataka kuwa kama Mungu ili aabudiwe, mara moja akatupwa chini. Jambo hili linapaswa kuzingatiwa sana na kila mwanamuziki lisimpate. Fahamu Roho ya Lusifa inavizia kuwanasa wanamuziki na kuwangamiza.
Mwimbaji anatakiwa awe na sifa muhimu zifuatazo:-
1.          Mwimbaji awe mtu aliyeokoka Isaya 5:11-12, Zab 50:16-17
2.          Mwimbaji awe Mshirika, Mwanachama mwaminifu wa Kanisa.
3.          Mwimbaji awe na tabia njema, mwenendo mzuri kiroho
4.          Mwimbaji awe na wito na Msukumo wa Kimungu katika huduma hii na si vinginevyo
5.          Mwimbaji aifahamu sauti yake vizuri, hisia zake azielekeze sawasawa katika ujumbe wa wimbo, asikilize miundo ya sauti, asitende vitendo au kuzidisha vitendo katika wimbo isivyo kawaida.
6.          Mwimbaji ahudhurie mazoezi pasipo kukosa, mazoezi huleta ukamilifu wa huduma.
7.          Mwimbaji awe tayari kutoa huduma wakati wowote bila masharti.
8.          Mwimbaji ajitahidi kujiendeleza, kuboresha, na kuikuza sanaa ya muziki na kupandisha viwango vyake vya uimbaji.
9.          Mwimbaji awe mtu wa maombi akiombea huduma.
10.      Mwimbaji awe mtiifu, mnyenyekevu, akiheshimu viongozi wa kanisa na huduma yake.
11.      Mwimbaji awe na bidii katika upendo wa kweli na kudumisha umoja na mahusiano katika huduma.
12.      Mwimbaji aimbe kwa upako wa Roho, kamwe si kwa mazoea wala kwa ujuzi pasipo kusahau maandalizi ya mwili, usafi na muonekano usio na maswali
13.      Mwimbaji aimbe kwa lengo la kumwinua, kumsifu, na kumtukuza Mungu kwa utukufu wake. Na si kwa lengo la kupata umaarufu na fedha.
14.      Mwimbaji anatakiwa kuwa na nidhamu kubwa inayotokana na mafunzo anayopewa na walimu wake ili kujenga hali ya kujiamini anaposimama mbele ya washarika.
Mwimbaji na mtumishi asiyekuwa na sifa hizi, hawezi kuwa mtumishi katika huduma ya mwili wa Kristo ambalo ni Kanisa, ambalo lipo kwa ajili ya kumpa sifa, utukufu na enzi Mungu aliye mkuu. Sifa hizi zinatufikisha katika utumishi mwema wa huduma ya kimbinguni ya sifa na ibada ya kweli katika Roho.
Asili ya vyombo vya muziki si shetani, bali ni Mungu (Ezekiel 28:11-13)
Lusifa (shetani) aliumbwa akiwa na vinanda ndani yake ili amsifu Mungu. Uwezo huo wa kuwa na vinanda ndani yake ni wa Mungu. Katika kitabu cha ufunuo tunaona shughuli za ibada zinapewa uzito mkubwa sana, na ibada hizo zinaongozwa na malaika wenye vyombo vya hali ya juu sana na kila shughuli inakwenda sambamba na muziki

(Ufunuo 5:8-9)
Wazee 24 Wana vinubi wakiimba wimbo mpya mbele za kiti cha Enzi wakiabudu.
(Ufunuo 8:1-2)
Malaika wakapewa baragumu saba. Hizi baragumu zinapigwa sambamba na hukumu ya Mungu kwa ulimwengu wakati wa dhiki kuu
(Ufunuo 14:1-3)
Sauti ya wapiga vinubi yasikika mbinguni, Yesu akiwa na watu 144.000 wenye muhuri wa Mungu
(Ufunuo 15:2-4)
Wale walioshinda kutoka katika dhiki kuu wenye vinubi vya MUNGU wanaonekana wakifanya ibada kando ya bahari ya kioo – mbele za Mwanakodoo wakiimba.
(Ufunuo 18:22-23)
Mfumo mwovu wa shetani umebadili matumizi matakatifu ya vyombo vya muziki na kuwa silaha yake. Kwa kuvitumia katika starehe na uovu mwingi. Shetani Ni mwizi lakini tusifuatishe wala kuigiza namna ya dunia, Mungu bado hajafilisika. Tukiomba atatupa ubunifu wa miziki ya Kiroho iliyo mitakatifu na yenye vionjo vya mbinguni.
(I Thesalonike 4:16)
Malaika Mkuu atapiga parapanda ya Mungu, ndipo kwa sauti hiyo wafu walioko makaburini waliokufa katika Yesu wataisikia, maana ina uhai wa kufufua miili iliyokufa. Sauti ya parapanda ina uwezo wa kubeba mamilioni ya watu walioko duniani na kuwapandisha (kuwanyakua) mpaka hewani atakapokuwepo Yesu naye atawalaki katika mirindimo hiyo hiyo ya parapanda. Leo sauti za vinubi, vinanda, zina uwezo huo huo ndani ya Kanisa la Kristo lenye kujali ibada ya Mungu kama ilivyokuwa tangu asili. Ni lazima Kanisa limwabudu Mungu kwa vinubi, matoazi, zeze, vinanda, parapanda na matari. Hiyo haikwepeki, maana hiyo ndiyo asili ya ibada ya kiroho.

Daudi alitengeneza vyombo hivyo na kuwapa walawi wavitumie Hekaluni, akina Daudi wa leo wapo Walawi wapo waimbaji wapo, basi tumfanyie Bwana ibada tukiwa na zana za muziki.
Ulimwengu umefika mbali katika swala la muziki. Je Kanisa tuko wapi? Nani awe bora na apendeze zaidi. Ili tuwe bora kila mtu atoe mchango wake wa vyombo ili Bwana atukuzwe katika sifa.

Kanisa lijitahidi iwezekanavyo kupata vyombo vya ibada. 1Kor 14:6-8 Paulo anaelezea umuhimu wa vyombo mbalimbali katika kuboresha sauti za nyimbo zetu kila zana ina aina ya sauti yake na kuleta tofauti inayoboresha wimbo, kwa kuwa utamu wa sauti za vyombo unaleta usikivu mzuri na fahari kwa wanaosikia na utukufu kwa Mungu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni