“Maana
mtatoka kwa furaha, mtaongozwa kwa amani mbele yenu milima na vilima vitatoa
nyimbo, na miti yote ya kondeni itapiga makofi”. (Isaya 55:12)
Wakati wa ibada ni wakati wa kilele
cha furaha ya mwanadamu ibada na kuabudu ni kumshangaa Mungu ambaye ni Mfalme
wa ajabu milele. (Yohana 4:23-24) Baba anamtafuta mtu atakayemwabudu katika
roho na kweli ifahamu misingi ya sifa, ibada na kuabudu katika roho na kweli
kama biblia ifundishavyo.
Mara
nyingi katika makanisa yetu tunakuwa na ratiba ambayo imebana sana, kwa hiyo
hutoa muda mfupi sana katika kusifu na kumuabudu Mungu katika roho na kweli
hivyo kulifanya kanisa kuwa katika hatua ya kwanza yaani mwilini wakati
muhubiri anapanda katika madhabahu kutoa ujumbe wa Mungu. Matokeo yake ni sawa
na kupanda mbegu katika miiba au kwenye udongo usiofaa kupandwa mbegu kwa
sababu ya kutoandaliwa vema na wahusika. Hivyo inahitajika weledi wa hali ya
juu na mafunzo kwa kanisa zima ili kuutumia muda huo mdogo kwa faida kubwa
kulingana
na somo nililofundisha la HEMA YA KUKUTANA NA MUNGU. Ambalo linafundisha hatua
tatu muhimu za kumwendea Mungu, ambapo hatua ya kwanza kanisa linapoanza ibada
huwa katika mwili. Baadae huenda kwenye nafsi na hatua ya mwisho hufika rohoni
kabla ya mhubiri kupanda kwa ajili ya kutoa ujumbe wa Mungu. Katika kitabu hiki
tunakwenda kuangalia kwa undani zaidi mambo mbalimbali yanayohusu kumsifu Mungu
na kumuabudu katika Roho na kweli, maana Mungu anawatafuta watu kama hao. Mungu
akubariki sana wakati unaendelea kupata siri za ufalme wa Mungu kupitia katika
kitabu hiki.
Kusifu
na kumwabudu Mungu katika roho na kweli ni jukumu kuu la wakati wote katika
maisha yetu binafsi na katika makanisa yetu, hii ni kwa sababu Mungu alituumba
sisi kwa ajili yake mwenyewe. Anasema
“Watu wale niliojiumbia nafsi
yangu ili watangaze sifa zangu”. (Isaya 43: 21)
Hii
inatuthibitishia kwamba, kumbe tuliumbwa na Mungu kwa kusudi moja tu, la
kumsifu na kumuabudu. Ili siku zote hisia zetu zimwelekee yeye, Mungu Baba yetu
na tutangaze sifa zake Mungu muumbaji wetu. Biblia inasema,
“Bali ninyi ni mzao mteule ukuhani wa kifalme,
taifa takatifu watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye
aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu” (1Petro 2:9.)
Kusifu.
Kabla
ya maelezo juu ya kuabudu, ni vizuri kwanza tugusie japo kidogo juu ya kusifu
ni nini? Kwa sababu ukiangalia kwa makini, kusifu na kuabudu ni vitu viwili
tofauti, ingawa vinaenda pamoja.
-
Kwa kawaida unaweza kuwa na ibada ya
sifa bila kuabudu, na inaweza ikawa nzuri tu.
Lakini
siyo rahisi kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu.
Ni
mara chache kutokea kuwa na ibada ya kuabudu bila kusifu. Hii hutokea tu pale
mtu anapovamiwa na mguso wa Roho Mtakatifu wa Mungu kwa namna isiyo ya kawaida.
Kusifu
kwa vyovyote vile iwavyo, huwa ni tendo la kutangaza kwa nguvu, na kwa uwazi
tena hadharani. Ukielezea na kuonyesha uhakika ulionao juu ya unachokitolea
sifa.
Kwa
maana hiyo, popote panapokusudiwa kuwa pawepo na sifa, kuna hekaheka na
matendo, sauti na nyimbo, vyote huonekana na kusikika.
Kusifu
ni utaratibu unaopangwa na ufahamu wako jinsi gani udhamirie kusifia, sio
kulazimishwa na mtu kama tuko kwenye gwaride, kuna ule mtindo ambao viongozi wa
sifa huutumia, mara bariki kushoto, bariki kulia, bariki mchungaji, bariki
wanakwaya! Hayo ni mambo ya stage show katika ibada haiko hivyo. Ingawa unaweza
kufanya hivyo mwanzo kabisa katika kuhamasisha, lakini baada ya hapo waachie
watu wapambane wenyewe kuingia barazani
pa Mungu.
Mara
nyingi nimeongea na viongozi wa sifa sehemu mbalimbali tunapokutana kwamba, sio
wajibu wao kuwaambia watu hebu simameni ili tumsifu Mungu. Inatakiwa mtu mwenyewe aguswe toka ndani,
yaani mtu wa ndani ndio anatakiwa amuamulie mtu wa nje (mwili) kufanya vile mtu
wa ndani anavyotaka.
Ukienda
mahali ambako sifa zinafanyika kwa uhakika utashangaa! Utaona wengine wamelala
chini, wengine wananesanesa, wengine wanarukaruka, wengine wanapiga ukuta kwa
ngumi ili mradi ni hekaheka, na hakuna mtu mwenye habari za kushangaa shangaa. Sasa
kiongozi wa sifa, kwa mfano unapowaambia watu wasimame! Kwani nani alikwambia
kwamba kusimama ndio tafsiri ya heshima? Ingawa ni kweli kwa jadi zetu
tunaamini kwamba kusimama ni dalili ya heshima. Kwa wengine kitendo cha
kusimama ni dharau. Kina mama wa makabila fulani wanapotaka kukusalimia kwa
heshima wanakaa chini, au wanapiga magoti.
-
Mama wa aina hiyo binti yake
akisalimia watu kwa kusimama, anamuona hana heshima hiyo ni anadharau kabisa.
Makabila
mengine ya kusini mwa Tanzania kama wangoni akikuheshimu au akitaka kukushukuru
kwa kiwango cha juu analala chini kabisa.
-
Kwa hiyo ndio maana ninashauri kuwa
ni vema viongozi wa ibada na viongozi wa sifa, kutokuwaamulia watu nini cha
kufanya kulingana tafsiri zao za mila ya kwao.
Kusifu
ni njia ya lango kuu la kuingilia katika kiini cha kuabudu. Hivyo kusifu ni
ibada yenye umuhimu wa kipekee kwa Mungu wetu, kikundi cha sifa ni askari wa
mstari wa mbele na ndio wanaotengeneza njia ya muhubiri kupitisha neno la Mungu
katika mioyo ya watu ambayo tayari imeshalainishwa na sifa. Zaburi 22:3.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni