Kuabudu ni hisia za upendo mkuu kutoka kwa
mwanadamu kwenda kwa Mungu. Kuabudu kunahusisha zaidi hisia kali zenye upendo
mkuu zinazogusa ufahamu, na kuzama katika upendo wa ndani kabisa na kuhusudu.
(Adoration).
-
Kuhusudu
ni mguso ambao unaachilia hisia za papo kwa hapo, na kusema kwa sauti ya
kusikika maneno yenye kujaa mlipuko wa upendo mkuu kutoka chini ya uvungu wa
moyo.
na kwa sauti ya upole na kusukumiza maneno
ya upendo wa ndani, pamoja na kubembeleza kwingi, ukiambatanisha na maombi
yaliyojaa unyenyekevu, heshima, adabu, na hofu na kijikita katika ibada ya
dhati mbele ya Mungu, kumsifu na kumwabudu.
Maana
ya kuabudu.
Ni tendo linalogusa akili, hisia, nafsi na
utu wa mtu na mwili pia kwa kusujudu, kuanguka kifudifudi, au uso kwa uso. “Abramu akaanguka kifudifudi,
Mungu akamwambia, akasema”, (Mwanzo. 17:3)
Tendo hili linafanywa pasipo ushawishi wa
kitu, chochote katika hisia za ndani, wala si nje ya Moyo wa kumtambua Mungu
kuwa wa thamani kuliko kitu chochote, anayestahili kupewa ibada ya pekee na
kupelekea kujitoa kwake bila unafiki wala ubinafsi.
Ni dhana zaidi ya ufahamu wetu wa kianadamu,
taratibu za dini zetu, desturi na mipango ya ibada zetu za kimazowea. Ni ibada
inayojumuisha utu wako mzima na kuwasha moto katika mawazo, fikra na hisia zako
zote, kiasi cha kuhisi unampapasa na kumwona Mungu katika Roho na kuwa halisi. “Lile
lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu,
tulilolitazama na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya neno la uzima”.
(1Yohona 1:1-2).
Na uzima huo ulidhihirika
nasi tumeona tena twashuhudia huo uzima. Uhalisi huu unampelekea mtu kumwabudu
MUNGU.
Mambo
ya kuzingatia katika kuabudu:-
Ibada ni lazima ifanywe katika roho.
Hamasiko liwe la Roho Mtakatifu na siyo misisimko ya mwili na akili tu. Ibada
ifanyike katika moyo wa dhati na wa kweli iliyofunuliwa na Yesu yaani sawasawa
na NENO lake.
Kuabudu nje ya Roho na kweli huko sio
kuabudu ni kuabudu kitu kingine kama vile sala za kutafakari, sala zenye
viwango fulani, kuwa na idadi ya sala, mpangilio wa sala kwa kuhesabu shanga,
kuchoma udi, maji maalumu ya baraka, ama kuvaa mavazi maalumu na kujiweka
katika muonekano fulani. Kumtumia mtu wa kati ili awakilishe maombi yako mbele
za Yesu na Yesu ampelekee Mungu.
Kwa vyovyote Hiyo sio maana ya kuabudu.
Kuabudu
ni ujuzi wa kipekee
Wakati wa kuabudu ni wakati muhimu mno, ni wakati
wa shughuli
ya utukufu kupita zote ambazo mwanadamu anafanya katika maisha yake. Wakati wa
kuabudu unazidi nyakati zote anazoweza mtu Kuzifurahia katika Mungu.
Tena kuabudu huacha
aina fulani ya kumbukumbu ndani ya mtu. Kumbukumbu ya kuabudu inapita vilele
vyote vya furaha hizo, maana ni wakati wa kukutana na Mungu. Je mwanadamu ni
nani hata akapewa nafasi tukufu kama hiyo? Kwa kuwa, kuabudu ni sehemu ya
maisha na ushirika na Mungu na ni jambo la rohoni, kwa maana hiyo basi, kuabudu
kunakuwa sehemu ya kila jambo analofanya mtu katika maisha yake. Kuabudu ni
ufunguo wa maisha yenye mafanikio na mwelekeo wa fikra na mawazo ya moyo, na
kuwa mtindo wa maisha ya kila siku ya mtu. Maombi ni njia kuu na bora zaidi ya
kumsifu na kumwabudu Mungu. Maombi ni wakati ambao mtu anazungumza na Mungu
mambo yake na kujimimina moyo wake mbele za Mungu.
Kuabudu na maombi
Katika maombi ya dhati na ya kweli, mtu
hujiachia akawa wazi kujieleza na kutoa siri za moyo wake akijua Mungu ndiye
msaada wake na kimbillio lake. (Zab. 46:1-3),
“Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada
utakaoneekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari, maji yake yajapovuma na kuumuka,
ijapopepesuka milima kwa kiburi chake”.
Kwa kutambua ukuu wa Mungu na uwezo wake
ndipo ibada ya kweli kutoka katika vilindi vya moyo huanza, na mtu hushuka
chini sana katika ufahamu wake kumtambua Mungu ni nani na kumwabudu na kumpa
sifa katika maombi. Katika hali hiyo ya maombi humfanya mtu ajione si kitu bali
astahiliye ni Mungu,
-
Ndipo
wengine huanguka chini na kugaragara kuonyesha upendo mbele za Mungu.
“Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli,
akaomba, akisema, Baba yangu ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, walakini si
kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe”. (Mathayo 26: 39)
Hata malaika wanaabudu na kuanguka mbele za
Mungu.
Yesu naye aliabudu hata akalia na kutoa
machozi ya damu akiomba.
“Naye kwa vile alivyokuwa alivyokuwa katika dhiki,
akazidi sana kuomba, hali yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini”
(Luka 22: 44)
Ayubu aliomba na kujiachia mikononi mwa
Mungu akisema, najua mtetezi wangu yu hai na pasipo mwili huu nitamwona Mungu.
“Lakini mimi najua mteteaji wangu yu hai, na kuwa
hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, lakini
pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu Nami nitamwona mimi nafsi yangu Na
macho yangu yatamtazama wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yangu”
(Ayubu 19: 25 -27)
Maombi huvuka mipaka ya mazingira ya mwili
wa nyama na kumleta mtu mahali alipo Mungu katika Roho kiasi kwamba muombaji
anakuwa na mazungumuzo na Mungu ana kwa ana.
Kama Paulo asemavyo ABA yaani Baba aliye
karibu naye kama mwana.
“Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo
hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani,
Baba”. (Warumi 8: 15)
Maombi kama haya yanafanyika katika dhana ya
kumtambua Mungu mwenyezi na ukuu wake, uweza wake, mamlaka na nguvu. Kisha moyo
wa mtu huyu huzama ndani ya ibada kwa maombi na kumwabudu, na kumpa sifa yeye
aliye juu Mungu mkuu. Ufahamu huu unamfanya mtu amheshimu Mungu na kumwabudu
kwa mshangao mkuu, na kumvuta kumpenda na kuichukia dhambi, kama Isaya
asemavyo,
“Mimi ni mtu mwenye midomo michafu na ninakaa kati
ya watu wenye midomo michafu”. (Isaya 6:1-5)
Petro naye akasema,
“Ondoka kwangu Bwana mimi ni mtu mwenye dhambi”. (Luka
5:8-9).
Heshima hii kwa Mungu huona utukufu wa Mungu
ulivyo mkuu na utakatifu wake ulivyo wa ajabu, na kushindwa kustahimili mbele
ya Mungu kisha kusema maneno hayo ya unyenyekevu katika maombi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni