Jumatatu, 30 Januari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (3)


Mwl Furaha Amon


Baada ya kuweka msingi katika sehemu ya kwanza na ya pili ya somo hili, nafikiri sasa tunaweza sasa kuendelea kuangalia zaidi mambo ambayo Mungu amesema kuhusu watu kuachana kwa talaka na kuoa tena. Kwa kuwa maneno mengi yenye kuleta ukakasi kuhusu kupeana talaka, na kuoa tena ni yale ambayo Yesu aliwaambia Waisraeli, itatusiadia kwanza kuona Mungu alichosema miaka mia nyingi kabla, juu ya jambo hilo hilo kwa Waisraeli wa zamani. Tukikuta kwamba alichosema Mungu kwa njia ya Musa na alichosema Mungu kwa njia ya Yesu vinapingana, basi tutajua ya kwamba sheria ya Mungu ilibadilika au kwamba sisi ndio tumetafsiri vibaya tofauti kitu fulani kilichosemwa na Musa au na Yesu.
Basi, tuanze kwa kutazama yale ambayo Mungu alifunua hapo mwanzo kuhusu talaka na kuoa tena baada ya talaka.
Tayari nimekwisha taja Maandiko ya Mwanzo 2 ambayo kulingana na mafundisho ya Yesu, yana umuhimu kwa somo letu hili linalohusu mambo ya talaka. Hebu sasa tuyaone moja kwa moja kutoka Mwanzo kwenyewe.
Na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, ‘Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (mwanzo 2:22-24).
Basi huo ndiyo mwanzo wa ndoa. Mungu alimfanya mwanamke wa kwanza kutoka kwa mwanamume wa kwanza, na kwa ajili ya mwanamume wa kwanza, kisha Yeye Mwenyewe binafsi akamleta kwa Adamu.

Yesu anaeleza hilo hivi, “Mungu … aliwaunganisha [pamoja]” (Mathayo 19:6,). Hii ndoa ya kwanza iliyopangwa na Mungu inatoa mfano kwa ajili ya ndoa zingine zote zilizofuata. Katika maeneo yote ya maisha ya mwanadamu, Mungu yuko makini sana Mungu huumba wanawake wa kutosha wanaume, Naye huwaumba ili kila mmoja avutiwe na mwenzake. Ndio maana tunasisitiza sana kwamba kunahitajika maombi na utulivu sana katika kuchagua mwenza wa kuishi naye. Tunaweza kusema kwamba Mungu bado anapanga ndoa za watu kwa hali ya juu sana (japo siku hizi watu wanaangalia zaidi mambo ya mwili, pamoja na mali.) lakini pia kuna wanaoanza mambo ya mapenzi kabla ya kuona na hivyo kuzuwia kabisa kupata msaada wa Mungu kama wameingia mahali sahihi au wameingilia ubavu wa mtu mwingine.

Kwa hiyo mtu anapokuwa kwenye ndoa nab ado anachepuka kwa kuwa wapenzi wengi zaidi, kuliko ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa). Basi, kama Yesu alivyosema, mwanadamu yeyote asitenganishe wale ambao Mungu amewaunganisha. Halikuwa kusudi la Mungu kwamba wale wana ndoa wa kwanza waishi maisha binafsi kila mmoja, bali kwamba wapate baraka katika kuishi pamoja kwa hali ya kutegemeana. Kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu katika eneo hili ni dhambi. Basi, kutoka katika sura ya pili ya Biblia, ukweli ni kwamba talaka haikuwa kusudi la Mungu kwa ndoa yoyote ile. Nakumbuka wakati fulani mchungaji wangu alimualika muhubiri mmoja kutoka Malawi ambaye walikutana naye ufaransa. Muhubiri huyu alitoa ushuhuda ambao unaweza kusaidia katika somo letu. Alisema kwamba yeye alikuwa anafanya kazi benki na akatokea kumpenda msichana mmoja ambaye alikuwa ameokoka, kwa sheria ambazo sio rasmi, vijana waliookoka huwa hawaoani na watu wasiookoka (watu wa mataifa) kwa sababu hiyo huyu mtumishi ilibidi ajivalishe ngozi ya kondoo na kuingia kanisani na kujifanya ameokoka. Na kwa sababu ya nafasi yake katika jamii, hata kanisani alianza kupewa nafasi za uongozi na baada ya muda akamtokea yule binti na kumtamkia kwamba anataka kumuoa. Binti bila hata ya kuomba akakubali. Nafikiri aliangalia zaidi hali ya kimwili na sio kiroho. Baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria, hatimaye walifunga harusi kubwa sana. 
Yule muhubiri anasema zilichukua wiki mbili tu kuanza kuonyesha hali yake halisi, anasema kwanza alianza kurudi nyumbani akiwa amelewa. Na kuanza kumfanyia fujo mke wake na kumfukuza, baadae akaanza kuleta makreti ya bia, anakuja na marafiki zake halafu anamlazimisha mke wake ndio awe anawafungulia hizo bia kama madada wauza bar. Yule mwanamke akikataa, anakula kichapo cha haja. 
Akijaribu kukimbilia kwa wazazi wake wanamrudisha, akienda kanisani anaona kila mtu kamchoka maana kila siku kesi haziishi. Akaishi maisha ya shida sana kila siku anapigwa na kutukanwa, kisha analala nje ya nyumba yao kwenye jengo ambalo halijamalizwa kujengwa. Lakini sifa kubwa ya huyu mwanamke alikuwa anamwamini sana Mungu, na kuendelea kuomba kwa ajili ya mume wake. Yule mtumishi anasema siku moja akiwa na pikipiki kubwa. Wakati anarudi nyumbani akiwa ameonja kidogo pombe, alipata ajali mbaya ya pikipiki. Alitunyesha kichwa chake kilikuwa kama kimesukwa. Anasema kichwa kilichanikachanika, na alipoteza fahamu kwa zaidi ya mwezi. Anasema wakati hana fahamu Mungu alikuwa anamuonyesha mambo yote mabaya aliyokuwa akimfanyia mke wake. Anasema siku anapata fahamu anamuona mke wake ameinamia miguu yake akiendelea kumuombea kwa machozi, baadae akagundua kuwa pamoja na ubaya wote ule lakini mke wake alionyesha upendo wa hali ya juu sana. Na baada ya kupona aliacha na kazi, akaamua kumtumikia Mungu kwa ujumla. Kwa huyu msichana imekuwa ni bahati kwamba Mungu mwenyewe aliamua kumsaidia kutokana na uvumilivu wake.

               MWISHO WA SOMO LA TATU


Tutaendelea na sehemu ya nne ya somo hili. Kwa maoni na msaada zaidi wasiliana nami kwa mobile namba 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni