Jumatano, 1 Februari 2017

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (2)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU NI NANI?                                       
“Upepo huvuma uendako, na sauti yake wasikika, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho” (Yohana 3:8)
Tunapoangalia kwa lugha ya Kiyunani, tunaweza kuona kuwa kitu ambacho ni roho hufananishwa au huelezewa kwa mfano huu uliotangulia. Hapa tunajifunza kuwa, hakuna mtu anayeweza kuukamata au kuuona upepo kwa macho ya kibinadamu, bali anachoweza kuona ni kazi au matunda yaletwayo na upepo. Hali kadhalika hatuwezi kumwona Roho Mtakatifu kwa macho ya kibinadamu wala kumkamata, bali aliyempokea anaziona kazi zake waziwazi kabisa

ROHO MTAKATIFU HAKUUMBWA.
Roho Mtakatifu hakuumbwa, bali ni mojawapo katika Nafsi takatifu za Mungu. Kwa hiyo ni sahihi kusema kwamba Roho Mtakatifu pia ni Mungu. Kumbuka kuwa tunaposema Nafsi tatu za Mungu hatumaanishi kuwa kuna Miungu watatu, bali ni Mungu mmoja katika nafsi tatu, yaani Baba Mwana na Roho Mtakatifu.
Ni vema pia tufahamu kuwa ufalme wa Mungu ni ufalme wa siri, kwa hiyo hata kumfahamu Mungu kwa ufasaha na utatu wake ni kitu kisichowezekana kwa akili za kibinadamu zilizoghoshiwa na dhambi, ni lazima tukubali kwamba ni kwa neema ya Mungu tu. Kwa kawaida ufahamu huu unapatikana kwa Yule tu aliyeokoka kwa kuzaliwa mara ya pili, na kumpokea Roho Mtakatifu aliye mwalimu wa kweli. Neno la Mungu linasema;-
“Hakuna ajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake na vivyo hivyo mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” 1 Wakorinto 2:11
Kuna sehemu nyingi sana kwenye Biblia zinazoelezea nafsi hizi za Mungu na mfano mzuri tunaupata katika injili ya Luka wakati wa kubatizwa kwa Yesu Kristo;-
“Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye Kristo amebatizwa , naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, wewe ndiwe mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe” (Luka 3: 21-22)
Kwa maelezo ya mistari hii, tunaziona nafsi zote tatu za Mungu zikijidhihirisha waziwazi kwa wakati mmoja yaani;-
1.  MWANA alikuwa majini akibatizwa
2.  ROHO MTAKATIFU akamshukia kwa mfano wa hua.
3. BABA akatoa sauti kutoka mbinguni. “Wewe ndiwe mwanangu, mpendwa; nimependezwa nawe”
Kwa kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi hai ya Mungu, hapana shaka kwamba naye pia ni Mungu na ana sifa ya kuwa Alfa na Omega kwa maana ya kwamba hana mwanzo wala mwisho na ni makosa kuamini kwamba Roho Mtakatifu ameumbwa na Mungu.

Kwa leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili. Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni