Jumatano, 1 Februari 2017

SOMO: ROHO MTAKATIFU NA MAMBO YAKE (3)


Mwl: Furaha Amon

Utangulizi:
Watu wengi mno ndani ya makanisa wana kiu ya kupata ujazo wa Roho Mtakatifu, lakini bado kuna tatizo kubwa sana linalohusiana na kutomwelewa vizuri Roho Mtakatifu. Kwa kuwa kiu hii ni kubwa, na tatizo la kutomwelewa Roho Mtakatifu ndani ya kanisa ni kubwa sana nimeona ni vema nitumie nafasi hii kutoa mchango kidogo wa kukusaidia kuelewa kwa kiasi habari za Roho Mtakatifu.
ROHO MTAKATIFU SIO NGUVU KAMA YA UMEME
Watu wengine wanafikiria kuwa  Roho Mtakatifu ni nguvu kama vile ilivyo nguvu ya umeme, mawazo hayo sio sahihi kabisa. Ni kweli kuwa mtu anapompokea Roho Mtakatifu hufunikwa na nguvu isiyo ya kawaida. Lakini nguvu hii sio Roho Mtakatifu. Katika kitabu cha Matendo ya mitume, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa watapokea nguvu akiisha kuwajilia Roho Mtakatifu. Lakini ukweli ni kwamba Roho Mtakatifu mwenyewe sio nguvu bali ni nafsi hai ya Mungu.

MAMBO YANAYODHIHIRISHA KUWA ROHO NI NAFSI NA NI MUNGU:
ANAWEZA KUHUZUNIKA.
“Wala msimhuzunishe Yule Roho Mtakatifu wa Mungu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi” (Efeso 4:30)
Hapa Roho Mtakatifu kama alivyo mwanadamu, anaweza kuhuzunishwa na kuhuzunika. Ukweli ni kwamba nguvu kama ilivyo ya umeme au nyingine iwayo yoyote ile haiwezi kuhuzunika, lakini roho kama nafsi hai anaweza kuhuzunishwa pale watoto wa Mungu wanapoenda kinyume na neno la Mungu.

HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKIKA:
“ kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi ipasavyo; lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum 8:26)
Huu ni udhibitisho mwingine unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi, huweza kutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Nguvu haiwezi kumwombea mwanadamu kwa Mungu kwa kuugua, bali jambo hili huweza kufanywa na nafsi iliyo hai pekee.

ANAWEZA KUAMBIWA UONGO.
“Petro akasema, Anania, kwa nini shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?” (Matendo 5:3)
Hapa tunamwona Petro akimwonya Anania kuhusiana na mali aliyoipata baada ya kuuza kiwanja chake. Alipouza kiwanja chake hakuleta fedha yote miguuni pa mitume kama walivyokuwa wamepatana katika kanisa! Anania alidhani kuwa kosa alilotenda halitatambulikana, hivyo aliamua kusema uongo mbele za mtumishi wa Mungu. Petro naye kwa njia ya ufunuo wa Roho Mtakatifu, anamwambia wazi Anania na safila mkewe kuwa hawakumwambia uongo mwanadamu bali Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu ni nafsi ndiyo maana anaweza kuambiwa uongo; nguvu haiwezi kuambiwa uongo.

ANAWEZA KUFANYIWA KUFURU:
“Kwa sababu hii nawaambia, kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kumkufuru Roho Mtakatifu hawatasamehewa” (Mathayo 12:31)
Huu nao ni uthibitisho mwingine unaoonyesha kuwa Roho Mtakatifu si nguvu bali ni nafsi iliyo hai. Kwa kuwa ni nafsi hai anaweza kutukanwa na kunenewa maneno ya kufuru na wale waliokwisha kupewa Nuru na kukionja kipawa cha mbinguni; wale waliofanywa washirika na Roho huyu na kulionja neno zuri la Mungu pamoja na kuzionja nguvu za zamani zijazo. Roho mtakatifu angelikuwa nguvu kama ilivyo nguvu ya umeme basi asingeliweza kunenewa maneno ya kufuru maana hakuna anayeweza kuikufuru nguvu.

ANAWEZA KUFANYIWA JEURI.
Pamoja na sababu hizi zinazomfanya Roho Mtakatifu kuwa nafsi halisi na hai neno linatuambia kuwa Roho Mtakatifu anaweza kufanyiwa jeuri na watoto wa Mungu. Hili hutokea pale watoto wa Mungu wanapokataa kwa kukusudia kuitii sauti ya Roho wa Mungu ndani yao na kuamua kuasi. Neno la Mungu katika waebrania 10:29 linatuambia kuwa;
“Kila afanyaye dhambi kwa kukusudia baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, anamfanyia jeuri Roho wa mema au Roho Mtakatifu”.

Kwa ujumla kuna mifano mingi ya kimaandiko inayothibitishwa kuwa Roho Mtakatifu ni nafsi hai, ila kwa hii michache nimeielezea ili ikusaidie kutafuta mingine inayofanana na hiyo.
MWISHO
Kwa leo somo letu linaishia hapa, usikose kufuatilia sehemu inayofuata ya somo hili. Kwa msaada zaidi tuwasiliane 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni