Jumanne, 31 Julai 2012

SAIKOLOJIA: TATIZO LA WANAUME DHAIFU KATIKA NDOA


  • Kulingana na taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), tatizo hili la wanaume dhaifu linaongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuendekeza ulevi, matumizi ya tumbaku/sigara, kutokula kwa kuzingatia mchanganyiko wa vyakula (ulaji usiofaa) na watu kutopenda mazoezi.
SHARE THIS STORY
Ni vigumu kufahamu haya, lakini ndio ukweli kuwa kuna kasi ya kuongezeka kwa wanaume dhaifu nchini na ulimwengu kwa ujumla.
Kulingana na taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), tatizo hili la wanaume dhaifu linaongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuendekeza ulevi, matumizi ya tumbaku/sigara, kutokula kwa kuzingatia mchanganyiko wa vyakula (ulaji usiofaa) na watu kutopenda mazoezi.
Hapa nchini hakuna utafiti thabiti uliofanywa lakini nafikiri tutakubaliana kuwa tatizo hili lipo tena ni kubwa, kwani kinyume na hilo kusingekuwa na watu wengi wanaojitangaza kwamba wanatibu. Marekani  wamefanya utafiti, Shirika liitwalo National Ambulatory Medical Care Survey (NAMCS) ambalo linasifika kwa kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya afya, linasema kwamba ukionana na Wamarekani 1,000 ujue kwamba 22 ni wanaume dhaifu.
NAMCS ikasema pia kwamba zaidi ya wanaume milioni 2.6 wanatumia dawa za kuongeza nguvu; ndio nasema kwamba sisi Tanzania hatujafanya utafiti rasmi uliotangazwa na Serikali, lakini wewe bila shaka utakuwa shahidi kwamba ziko dalili kwamba hali ni mbaya.
Kuna mtafiti mmoja maarufu kutoka India, Dk Srini Vasakumar, kutoka kituo cha utafiti wa tiba kiitwacho Institute of Biology and Clinical, India, ambaye amekuwa akitoa huduma za kuponya tatizo hilo la udhaifu katika maeneo mbalimbali hapa nchini, anasema hili ni tatizo linaloweza kupona, shida ya wengi ni kutochukua hatua; wengi wanalia, badala ya kuchukua hatua.
Daktari huyo mwenye Shahada ya pili ya Tiba kwa kutumia vyakula na Shahada ya uzamivu ya tiba kwa ujumla, anasema wengi wanaendelea kuwa na tatizo hili kwa  kutochukua hatua thabiti; wengi wamesoma na wanafahamu kuna aina za vyakula vinasaidia wanga, nguvu, mafuta na vitamini... lakini wanakula ili mradi tumbo lijae.
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi, Janet Bina Kahama, Aprili 10, mwaka  2007 katika kikao cha saba cha Bunge aliuliza swali namba 8 (b); je, Serikali inafahamu ni sababu gani zinasababisha kupungua kwa nguvu za kiume kunakotangazwa sana na waganga wa jadi? Aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof. David Mwakyusa alijibu kuwa tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, baadhi yao ni lishe duni hasa mboga za majani, kutokula aina mbalimbali za jamii ya karanga, matumizi yasiyofaa ya ulevi kama pombe.
Sababu nyingine ni matumizi ya sigara, dawa za kulevya, dawa zinazotibu baadhi ya magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya akili na kutopumzika kunakosababishwa na shughuli nyingi za kijamii hivyo kusababisha uchovu. 
Kwa uzoefu wangu kama mtu ambaye nimekuwa nikitoa ushauri kuhusu masuala ya ndoa ni kwamba tatizo hili lina athari kubwa katika ndoa, baadhi ya wanawake sasa hawaangalii uzuri wa mwanaume, wala utajiri  au elimu yake ama tabia, kwanza wanatamani kujua kama mume mtarajiwa ni mume dhaifu au la.
Athari za kuwa dhaifu ni kwamba baadhi ya wanawake unaweza kumpa  mamilioni ya fedha, magari nk lakini unachohonga akaenda kuhongwa mwingine. Unamnunulia gari, unaweza kushangaa  unakutana naye anatembea kwa miguu, gari kapewa kijana atanue nalo.
Ninachotaka kusema ni kwamba kila wanaume kuchukua tahadhari juu ya jambo hili ambalo linaonekana wazi kuwakwaza wanawake wengi kiasi cha baadhi kuamua kuvunja uhusiano. Hata hivyo kama mwenzi wako ana tatizo ni vizuri kuangalia namna ya kulitibu, sio kukimbiana, kwani hakupenda kuwa hivyo.

CHANZO: Mwananchi  Ijumaa,Januari 24  2014 

MAZUNGUMZO YANGU YA MWISHO NA ABEL MOTIKA (MR EBBO)




Kwa watu wanaofuatilia sanaa ya muziki wa kizazi kipya katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati pamoja na sehemu nyingine mbalimbali duniani na hasa kwa watu wanaopenda kusikiliza nyimbo za kitanzania. Jina hili la “Mr Ebbo” sio jina geni kwao,nasema hili ni jina kubwa kwa sababu nyimbo zake zimechezwa na zinaendelea kuchezwa hata na mashirika makubwa ya utangazaji kama BBC,DW,VOA n.k. lakini ukweli unabaki palepale kwamba watu wengi walimfahamu Mr Abel kupitia picha za video au katika vipindi vya TV vinavyorusha nyimbo zake. Lakini ilikuwa kumuona Abel ana kwa ana akiwa hapa Tanga sio lahisi na unaweza kukaa miaka mingi usimuone kwa macho. Hii  ni kutokana na tabia yake ya kutokukupenda kutembea ovyo mitaani kwa hiyo muda mwingi utamkuta yupo nyumbani kwake ama katika studio yake akitengeneza mashairi ya nyimbo zake ambazo ni tofauti sana na nyimbo za wasanii wengine, na muda mwingi akiwa nyumbani kwake akiangalia filamu za kitanzania ambazo yeye ni mpenzi mkubwa wa filamu hizo.

Nakumbuka ilikuwa kama saa saba mchana nikiwa na rafiki yangu wa kazini Mr Boniface Lyimo tukiwa tumetoka kwenye mapango ya Amboni kikazi nilimuomba tupitie nyumbani kwa Mr Ebbo ambaye nilikuwa nimeahidiana naye kufanya mahojiano kwa ajili ya gazeti la kazini kwetu linaloitwa SAMAWATI. Mimi binafsi nimefahamiana na Mr Ebbo mwaka 1998 wakati bado alikua hajakuwa na jina kubwa katika muziki wa kizazi kipya. Na mimi wakati huo nilikuwa naandaa filamu mojawapo ya Kiswahili inayojulikana kwa jina la KOSA KUBWA ambapo tuliomba kutumia nyumba yake kuigizia baadhi ya vipande vya filamu hiyo.
Kwa ujumla Mr Ebbo naweza kumuelezea kama alikuwa mtu mchangamfu anayeheshimu watu pamoja na kazi zao. Na kama ukienda kwake utatamani usitoke upesi kwa sababu ya uchangamfu na maneno ya utani utani mwingi wa kuchekesha.
Nilipokutana naye wakati natayarisha makala hii pamoja na kwamba tulikuwa na muda mchache sana lakini ulikuwa ni muda ambao ulikuwa wa kurahisha sana na alinipa ushirikiano wa kutosha kabisa.
HISTORIA YAKE KWA KIFUPI
Kwa kifupi nilimuomba anieleze historia yake na alinieleza kama ifuatavyo: Abel Motika alizaliwa 1974 katika Hospital ya Mount Meru Arusha na amesoma elimu ya msingi toka darasa la kwanza hadi la tatu hapo hapo Arusha na baadae akahamia Nairobi ambapo alisoma darasa la nne na la tano ndipo akahamia Tanga kwa wazazi wake, ambapo alimalizia elimu ya msingi na baadae akasoma elimu ya sekondari hapahapa jijini Tanga.

ALIANZA VIPI SHUGHULI ZA MUZIKI?
Kuhusu muziki Abel alisema kwamba alianza kuupenda muziki tangu akiwa mtoto mdogo, na anakumbuka kuwa alikuwa akisikiliza zaidi muziki na hatimaye alijiapiza kwamba ni lazima siku moja atakuja kuwa mwanamuziki. Alipomaliza darasa la saba tu tayari alikuwa amejiunga na kwaya ya kanisa la K.K.K.T usharika wa Kisosora na huko ndiko ndoto yake ilipoingia katika vitendo kwani alijifunza kwa bidii sana misingi ya muziki, pamoja na matumizi ya ala za muziki,mpangilio wa sauti ya kwanza hadi ya nne na mpaka nilipokuwa nikiongea naye aliniambia kwa wakati huo alikuwa na uwezo wa kufundisha watu kupanga sauti na kuziimba na ndivyo alivyokuwa anafanya ukienda kurekodi katika studio yake ya Motika Record Studio ambayo kwa sasa hivi inamilikiwa na mke wake Baby na ameihamishia mjini Arusha ambako ameiboresha zaidi.


Abel alikuwa kwenye kwaya kwa kipindi kirefu na yeye mwenyewe alisema huko ndiko alikojifunza mbinu za muziki,mpangilio wa vyombo sauti pamoja na vitu vingine vingi vya kinidhamu katika sanaa hii ya muziki.
Katika eneo hilo Mr Abel alipenda kuwashukuru sana walimu wake wa kwaya pamoja na watu wote waliomsaidia kujenga kipaji chake katika Muziki na hatimaye kuweza kufanya kazi inayokubalika katika jamii.


ALISEMAJE KUHUSU KUPIGA MUZIKI LIVE ?.
Nilimuuliza Abel ni kwa nini wanamuziki wa Bongo flavor hawapendi kupiga muziki wa wazi (Live) na badala yake wanatumia studio na kupiga nyimbo kwenye maholi kwa mtindo wa kukandamizia kupitia kwenye CD walizotengeneza studio? na nilimuuliza kwamba haoni hatari za kupoteza hamasa ya watu kujifunza vyombo au ala za muziki iwapo jamii itaendekeza mtindo wa kutengeneza muziki studio na kuacha kupiga muziki live?
Abel alisema inawezekana watu wengi wakaamini hivyo na hasa wanamuziki na wapenzi wa muziki wa zamani. Lakini yeye kwa maoni yake kama mwanamuziki wa kizazi kipya haoni ubaya wa kutengeneza muziki studio kwa sababu ni kazi yenye gharama nafuu na inayohitaji watu wachache kufanya kazi ya watu wengi kwa ubora  uleule au na kuzidi pia.Anasema binadamu kila siku amekuwa akiumiza kichwa na anabuni mbinu za kurahisisha maisha na ndio maendeleo yenyewe kwani maendeleo ni mabadiliko.
Alisema hata magari ya zamani yalitengenezwa na mfumo wa gia za manual,lakini wataalamu wamegundua magari ya mfumo mpya wa gia wa automatic ambayo ni rahisi zaidi kuyaendesha na sasa hivi mengi yanakuja nchini kwetu inawezekana baada ya muda tusiweze kuyaona tena magari yenye mfumo wa gia wa manual yakiingia sokoni kwani sasa hivi kuna mabasi na magari makubwa  malori yanayotumia mfumo wa gia wa Automatic. Kwa hiyo kama ilivyo kwenye magari hata na kwenye muziki ni hivyo hivyo.

Abel anaamini kwamba muziki live utaendelea kuwepo na utakuwa na wapenzi wake lakini pia na muziki wa studio utaendelea kuwepo na utakuwa na wapenzi wake na wote utaendelea kuwepo kama vile ambavyo sasa hivi kuna magari yenye mfumo wa gia wa manual na automatic yameendelea kuwepo na watu wamekuwa wakitumia kwa kadri wanavyopenda wapo wanaopendelea yenye mfumo wa manual lakini pia wapo wanaopendelea yenye mfumo wa automatic.


Abel aliamini kwamba hata kwenye muziki utakuwepo muziki live ambao utakuwa na wapenzi wake na utaendelea kuwepo lakini pia utakuwepo muziki wa kutengenezwa studio ambao pia utakuwa na wapenzi wake upo ambao ukiwapeleka kwenye muziki live hawatakuelewa. Alisema kwamba muziki kama vile muziki wa reggae na jazz ni aina ya miziki inayopendeza zaidi ikipigwa live kuliko miziki ya Pop na RnB

Abel aliamini kwamba muziki wa studio hauwezi kuua vipaji vya watu wenye nia ya kujifunza vyombo vya muziki kama watakuwepo.Kwani fursa zitaendelea kuwepo kwa watu wanye nia ya kujifunza, lakini hapendi watu walazimishwe kurudi nyuma kimaendeleo au kuogopa kutumia teknolojia mpya kwa hofu ya kuua vipaji kwa sababu hata huko kwenye teknolojia mpya pia kutahitaji vipaji ndio maana pamaja na kuwa na teknolojia mpya lakini sio kila mtu ndio sasa anaweza kufanya kazi ya muziki au kuwa mwanamuziki.
KWA NINI KUMEKUWA NA TEKNOLOJIA YA KISASA KATIKA MUZIKI.?
nilimuuliza Ebbo swali hili nay eye alinijibu kwamba Teknolojia inakuja kwa lengo na makusudi ya kupunguza ugumu wa kazi na gharama. Hivyo watu wanapotumia akili ya kuvumbua vitu ni muhimu kuvitumia ili kuheshimu mawazo yao. Kabla watu hawajavumbua magari yanayokwenda kwa injini ya mvuke wa mafuta waliwakuta wenzao wanatumia magari yanayokokotwa na wanyama. Kwa maana hiyo na sisi hatuwezi kuwalazimisha watu kutembea na punda kama zama za mawe wakati sasa hivi kuna vyombo vyenye kasi kubwa ya kurahisisha safari,tukifanya hivyo tutakuwa wapinga maendeleo na wasaliti wa utandawazi na tiknolojia.
Kwa hiyo Abel anasema kwamba sio vizuri kuwalazimisha watu wapende muziki live wakati sio kila mtu anayependa muziki uwe live wapo watu katika kizazi hiki ambao hawajawahi kwenda kwenye tamasha linalopiga muziki live na hata ukimpeleka atashangaa




NI NINI SIRI YA NYIMBO ZA MR EBBO KUKUBALIKA
Nilimuuliza Abel ni kwa nini nyimbo zake zinakubalika na zinapendwa na kada ya watu wa rika na hadhi tofauti. Abel alinijibu kwamba Tangu zamani alijiwekea misingi ya aina ya nyimbo alizotaka kuziimba. Alipenda  aimbe nyimbo ambazo hazitamkwaza mtu, Nyimbo zenye aina ya ujumbe unaowakilishwa kama ucheshi lakini ambao ndani yake kuna ujumbe utakaomfanya mtu afikiri. Alisema  kuwa kama angekuwa anapenda kuimba nyimbo za mapenzi au za kisiasa pengine kila siku angekuwa anatoa nyimbo. Lakini nyimbo anazotunga yeye ni za aina yake tofauti na za mtu mwingine kwa sababu  hazimkwazi mkubwa,mtoto,mwanamke,mwanamume kijana mzee na zinapendwa hata na watumishi wa Mungu. Aliniambia kuna   wachungaji na mashehe wanazifurahia nyimbo zake na kumueleza waziwazi kuwa wanaikubali sana kazi yake. Hii ni kwa sababu ya aina ya tungo zake alisema Mr Ebbo kuwa anatengeneza nyimbo zenye ujumbe unaoleweka, na video zake anajitahidi ziwe safi ambazo hazitasababisha wazazi wakimbiane na watoto sebuleni,hiyo ndio siri kubwa ya mafanikio yake katika sanaa hii. Anasema yeye kama hajapata wazo la kuimba anaona ni bora atulie kuliko kulazimisha kutoa nyimbo ili kuwahi soko na hili ndilo tatizo kubwa linalowapata waimbaji wengi wa muziki wa kizazi kipya.

NI MWANAMUZIKI GANI AMBAYE EBBO ALIYEMPENDA?
Nilimuuliza Mr Ebbo ni mwanamuziki gani anayempenda na ambaye angependa awe kielelezo chake katika mafanikio yake kimuziki. Alinijibu kuwa ni mwanamuziki wa zamani wa Jamaika Robert Nesta Marley (Bob Marley). huyu ni mwimbaji ambaye ndio aliyempenda na kumfanya kuwa kielelezo chake katika muziki tangu zamani. Abel alisema kwamba yeye ni mpenzi wa muziki wa reggae na alipenda sana kufanya muziki wa reggae lakini kulingana na soko la muziki kwa nchi yetu ingekuwa ni vigumu sana kwake kupata mafanikio aliyokuwa ameyapata kama angepiga muziki wa reggae. Lakini alikiri kwamba ameamua kupiga muziki anaopiga sasa ili kuwashika watu wanaomkubali lakini muda mwingi akiwa nyumbani nyimbo kwake nyimbo nyingi anazosikiliza ni za reggae


   
NI WANAMUZIKI GANI WA TANZANIA WANAOMVUTIA?
Baada ya kunijibu aina ya muziki na wanamuziki anaowapenda katika dunia nilimgeuzia kibao aniambie wanamuziki anaowapenda Katika nchi yetu ya Tanzania nay eye alinijibu kuwa  anapenda sana wanamuziki wote ambao wapo makini na wanaoheshimu muziki kama taaluma na sio sehemu ya kupotezea muda au kujifurahisha na kuwafurahisha watu tu.  Anapenda  wanamuziki wote wanaojua kwamba muziki ni kazi inayohitaji staha na kujiheshimu kama ofisa au mwakilishi wa wananchi.
Lakini bado nilijitahidi sana kumbana aniambie mwanamuziki mtanzania ambaye yupo ndani ya uvungu wa moyo wake ndipo aliponifichulia kwamba  anavutiwa sana na kazi inayofanywa na Msanii Mrisho Mpoto na Saida Kaloli. Anasema kwamba Mpoto anapenda sana muziki wake kwa sababu ni muziki wa  kufunga na sio wa kuimba mambo waziwazi alisema katika wimbo wake mpya ambao aliamini kuwa ungetoka  karibuni alitegemea kuwa utakuwa na fikra mpya. Na atajaribu kuwakumbusha Watanzania na hasa wakazi wa Tanga kwamba pamoja na kuwepo kila kitu katika Super Market lakini wasisahau walikotoka wakumbuke na masoko yao ya ngamiani mgandini na masoko mengine ya mitaani ikiwa ni pamoja na magenge. Alisema vitu kama super market sio utamaduni wetu kwa asili ni utamaduni wa Ulaya hivyo tusiuuwe utamaduni wetu na kuukumbatia utamaduni wa Ulaya.
Anasema popote uendapo katika dunia hii kitu cha kujivunia ni cha kwako. na usipende kujivunia cha mtu mwingine. Abel ambaye mpaka wakati naongea naye tayari ana Albam kadhaa. Alisema  kwamba wimbo ambao anauheshimu ni ule uliomtambulisha kwenye ramani ya muziki wa Tanzania wimbo wake wa  kwanza “mimi maasai  bwana”ambao ulikuja kubeba na nyimbo nyingine nyingi.
Abel ambaye ni baba wa watoto watatu hakutaka kabisa kuongelea suala la mgogoro wa ndoa yake na mzazi mwenzake ambayo ililipotiwa sana kwenye vyombo vya habari na hasa magazeti ya udaku yaliyotoka kila wiki. Nilimuuliza kama anaweza kutoa ufafanuzi kwa mashabiki na wapenzi wake wajue ni nini hasa kilichotokea?

Abel aliniambia kwamba anayaacha yaliyoandikwa yabaki kama yalivyo kwa sababu ni mambo ambayo yanaigusa sana nafsi yake na hawezi kusema neno baya lolote kwa sababu yule ni mzazi mwenzake na ndugu yake kwa maana wanaunganishwa na watoto kwa hiyo akimsema vibaya au akimtukana ni kama anajitukana yeye mwenyewe.
Baada ya mazungumzo haya sikuwahi kumuona tena Ebbo na wala sikusikia habari zake mpaka wakati naandaa shindano la kusaka vipaji. Nilimuweka katika orodha ya watu watakaotembelea kambi yatu ya washiriki. Lakini siku moja alfajiri sana nilipigiwa simu ya kunitaarifu kwamba Ebbo ameaga dunia. Na mtu aliyenipa taarifa hizo namheshimu sana lakini nilifikiri labda taarifa zake sio sahihi lakini baada ya muda nikanza kupata simu za watu mbalimbali ikawa ni habari mbaya sana iliyofunika jiji la Tanga nasi tukasema Jina la Bwana litukuzwe
Huyu ndio MR EBBO mwanamuziki,rafiki,shujaa wetu aliyetufurahisha wakazi wa jiji la Tanga na watanzania wote kwa ujumla.
Mke wamarehemu Ebbo akiwa na dada wa marehemu Ebbo


wazazi wa Mr Ebbo siku ya mazishi ya mtoto wao.



JIJI LA TANGA NI CHIMBUKO LA BONGO MOVIE




Waswahili wana msemo mmoja maarufu sana usemao “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Msemo huu unastahili kabisa kupewa mkoa wa Tanga kulingana na historia yake ya sanaa hii ya filamu.Kama tunavyofahamu kwamba jiji hili lenye bandari na hali inayokubalika kwa utengenezaji wa filamu kwa sababu lina hali zote zinazohitajika kwa watengenezaji wa filamu, yaani bahari  misitu milima havipo mbali pia kuna vivutio vingine vingi sana vya kitalii ambavyo ni muhimu sana kwa viwanda vya kutengeneza filamu.
Kumbuka kwamba Tanga ni moja kati ya miji ya mwanzo kabisa kupewa hadhi ya kuwa  manispaa. Hata katika hali ya kiuchumi jiji hili lilikuwa ni moja kati ya miji yenye viwanda vingi katika miji iliyokuwa inakua kwa kasi kubwa sana kiuchumi hapa nchini Tanzania. na kwa sababu hiyo ilikuwa ni moja kati ya miji iliyokuwa inawavutia sana watu wengi kutoka miji mbalimbali ya Tanzania kuja kufanya kazi katika viwanda na katika mashamba ya mkonge ambayo yalikuwa mengi sana wakati huo.
Kwa sababu hiyo na nyingine nyingi,tunaweza kukubali kwamba jiji hili lilikuwa ni moja kati ya miji ya starehe sana katika miaka hiyo na moja kati ya vivutio vya starehe hizo ilikuwa ni majumba ya kuonyeshea filamu ambayo yalikuwa yapo katikati ya jiji hili ambalo limepangika vizuri sana kwa ardhi ya tambarare pamoja na barabara zake 21 pamoja na ardhi nzuri yenye rutuba na ustawi wa maua mazuri ya kuvutia.Kwa hiyo ninaposema kwamba jiji hili ni chimbuko la filamu za kitanzania, ambazo kwa sasa zimeshika kasi kabisa katika nchi yetu,na hasa katika jiji la Dar es salaam. Ndio maana naona umuhimu wa kuwakumbusha watanzania wenzangu kwamba tunapofurahia mafanikio haya na kupongezana,tusiwasahau watu waliojitoa muhanga kuhakikisha sanaa hii inasimama. Ijapokuwa ilikuwa katika hali ngumu sana ya teknolojia duni, na hamasa hafifu ya watanzania kukubali filamu za ki- Tanzania.

Hapo ndipo inatupasa kuwakumbuka 

watu maarufu wa jiji hili kama AbdulHakem S Bayakub, Said El Siag na mzee Amri S A Bawji maarufu kama mzee SANI ambaye ni mkurugenzi wa gazeti la sani na mtunzi wa hadithi za kusisimua. Yeye kupitia gazeti lake aliandika hadithi maarufu sana iliyowavutia watu wengi sana kwa wakati huo ikijulikana kama “Love story Tanganyika na Unguja” 

Hadithi hii baadaye alikuja kuibadilisha na kuwa filamu iliyotengenezwa na Abdulhakem S Bayakub. ambayo naweza kusema kuwa ndiyo ilikuwa ni mojawapo ya filamu za kwanza kwa mtindo ule ukiacha filamu nyingine ya hapa Tanga iliyokuwa ikijulikana kama “SHAMBA KUBWA”mtindo huu sasa ndio unaotumika kwa filamu za kitanzania maarufu kama Bongo Movie. Kwa hiyo tutakapokuwa tunawatafuta mashujaa wa filamu za kitanzania tusiache kuwapa heshima yao watu hawa.

Kwa watu wasiojua sana habari zinazohusu sanaa ya maonyesho ni vizuri nikawakumbusha kwamba katika sanaa za maonyesho kuna tanzu kama maigizo(tamthilia),nyimbo kama za kwaya,taarabu na bendi,ngoma za kiasili,mashairi,ngonjera,majigambo,ada za harusi,utambaji wa hadithi,chemsha bongo,jando na unyago na mazungumzo ya ana kwa ana.Tangu zamani watanzania wamekuwa wakizitumia tanzu hizi za sanaa za maonyesho katika shughuli mbalimbali za kila siku kwa karne nyingi sana na kwa kutumia tanzu hizi jamii iliweza kukosolewa,kufundishwa,kuelekezwa,kuongozwa vyema,kutahadharishwa kurithishwa utamaduni kutiwa ujasiri n.k.

Kwa hiyo tunapoongelea filamu tunaongelea hadithi iliyotayarishwa ama kwa kuandikwa au kwa ufaraguzi(kuelekezwa na mtu) ambayo ndani yake ina matukio,migogoro,visa,mikasa na hata vitimbwi ambavyo vinaweza kuvaliwa na wahusika na kuwasirishwa kwa njia ya matendo mbele ya hadhira kwa minajiri ya kuikosoa,kuifunza,kuishawishi,kuirekebisha na hata kuitahadharisha.Mara nyingi filamu hutoa hata burudani kwa wanajamii wakati likitimiliza maudhui yake niliyoyataja hapo mwanzo.



Ingawa filamu ni aina ya simulizi,lakini inatofautiana sana na aina nyingine ya simulizi kutokana na jinsi inavyowasilishwa kwa walengwa.Kwa mfano unaposoma kitabu cha simulizi (Novel), huwa
kinaelezea habari ambayo inawahusu wahusika wakuu ambao itakubidi wewe msomaji utafute sura zao na maumbile yao kutoka kichwani mwako, na pengine kwa msaada wa kutumia maelezo machache ambayo mwandishi atakupa kulingana na wasifu wa muhusika. Novel inaelezea habari (hadithi) yake katika muunganiko wa dialogue and narrative na inakuwa tayari katika kurasa iliyochapwa. Baadhi ya filamu huwa zinafanya vizuri sana kiasi kwamba watu wengi wanaamini kwamba maandishi hayafikishi ujumbe unaofaa mpaka iigizwe mbele ya jamii.

Filamu zinakubalika sana kutokana na kuweza kumuamuru na kumsahihisha mwanadamu katika ung’amuzi wake.

Kwa mtu asiyejua kabisa habari za utengenezaji wa filamu anaweza akafikiri ni kitu chepesi sana, kinachoweza kufanywa na mtu yeyote mwenye video camera ambaye amezowea kupiga picha harusi na mikutano.Kama nilivyosema awali kwamba filamu ni mojawapo ya sanaa za maonyesho inayopendwa zaidi duniani kote,kila siku mamilioni ya watu duniani kote huangalia filamu katika kumbi mbalimbali za kuonyeshea filamu au kupitia katika televisheni au kwenye video CD na video Tape majumbani kwao.

Wakati wa kutengeneza filamu,mawazo ya mtayarishaji na kundi la watengenezaji hufafanuliwa katika hisia za ndani kabisa kiasi ambacho walengwa hujihisi kwamba wanaona vitu halisi na wala sio vya kuigiza.
Katika nchi zilizoendelea,watengenezaji wa filamu ni watu wanaotegemewa sana na serikali zao katika kutangaza sera zao au propaganda zenye nia ya kuonyesha uwezo wa mataifa yao kiuchumi,kijeshi,kisiasa n.k. Hata katika mashirika makubwa ya kijasusi yanawatumia sana wataalamu hawa katika kufichua mipango ambayo wanahisi inakusudiwa kufanywa na magaidi au maadui wa Taifa lao.


Filamu ni sanaa yenye gharama kubwa sana,kwa nchi zilizoendelea kama Amerika filamu ndefu inaweza ikatumia gharama inayopindukia dola milioni hamsini $50,000,000 na watu wengi sana hupata mikataba ya ajira na kusafiri sehemu nyingi za dunia katika kukamilisha filamu. Na inagharimu si chini ya miezi sita mpaka miaka miwili kukamilisha filamu moja ndefu.
Kiwango nafuu kabisa kwa gharama ya kutengeneza filamu katika Hollwood ni kiasi kisichopungua dola $ 250,000.
Kazi ya kutengeneza filamu katika nchi yetu inahitaji nguvu kubwa na msukumo sana kutoka kwa watu wenye uwezo kifedha na hasa serikali kupitia katika wizara inayohusika na utamaduni na michezo,sipendi ukose kufahamu kwamba, Serikali yetu kwa kushirikiana na nchi mojawapo za skandinavia’ inao mfuko wa kufadhili vitu kama hivi unaojulikana kama mfuko wa utamaduni wa Taifa. Lakini katika eneo la filamu ningependa wizara hii iende mbali zaidi ya hapo,kwa sababu ni eneo ambalo nchi inaweza kukuza uchumi kwa kupitia sanaa hii.

Katika nchi nyingine kwa mfano India,watengenezaji filamu wa “Bollywood” waliingizia serikali yao mapato makubwa sana ambayo yalisaidia sana kukuza uchumi wa nchi yao.Hii ilitokana na mauzo ya filamu zao za kihindi zilizokuwa zinashabikiwa karibu katika dunia nzima,wale watu waliozaliwa siku nyingi watakumbuka jinsi ilivyokuwa hata hapa kwetu Tanzania nyakati zile.
Hata sasa hivi tunavyoweza kuona soko la filamu kama za Nigeria lilivyoshika kasi katika nchi yetu. Ni dhahili kwamba kama wafanya biashara wetu hawafanyi ujanja ujanja wa kukopi nakala hizo, au wanigeria wakiamua kusimamia kazi zao zisiibwe na mataperi wanaozisambaza hapa nchini. Ni wazi kwamba serikali yao itanufaika na mapato yanayopatikana kutokana na kuuza kazi zao katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki.
Hata hapa kwetu Tanzania,watengenezaji wa filamu wakijiweka katika mikakati ya kuhakikisha filamu zetu zinashika kasi, na kuitangaza nchi yetu watafanikiwa sana na hasa wakitumia mtaji mkubwa wa lugha yetu mwanana ya Kiswahili ambayo ni moja kati ya lugha zinazopewa umuhimu na mataifa ya afrika mashariki na kati.
Kinachotakiwa hapa ni ushirikiano wa dhati kati ya watengenezaji wa filamu kwa upande wao,vikundi vya sanaa za uigizaji na serikali kwa maana ya kuviwezesha vikundi na kufanikisha malengo kwa nia ya kuongeza ajira na kukuza soko la filamu kwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki na kati.
Kitu ambacho hakiepukiki katika mipango hii,ni pamoja na serikali kutenga eneo la ardhi au kijiji maalumu kwa shughuli za uigizaji. Ikiwezekana kwa kila Mkoa kama vile kilivyo kijiji cha makumbusho kwa jiji la Dar es salaam. Lakini eneo linatakiwa liwe kubwa na ambalo waigizaji watapatiwa viwanja na kujenga kijiji ambacho kinatakiwa kiwe na kila kitu ili kuepusha migongano ya kijamii kwa mfano,mahospitali,mashule, vituo vya polisi,mahakama,nk

Vitu ambavyo vinaleta usumbufu sana mnapotaka kurekodi kipindi chenu katika mahospitali ya jumuiya au vituo vya polisi au mahakamani na wakati,kwanza sheria ya nchi yetu hairuhusu kufanya vitu kama hivyo au kufunga mtaa fulani kwa shughuli za kurekodi. Na kwa jinsi filamu ilivyo na kanuni zake haitakiwi kabisa kudanganya makusudi,kuwaonyesha watu chumba fulani halafu unawaambia watu hapa ndio mahakamani wakati wanaona kitu tofauti. Kwa maana hiyo unakuwa umetoa ule uhalisia wa filamu ambao ndio unaotakiwa,Kwa hiyo iwapo kutakuwa na vijiji vya wasanii kutasaidia sana kuzifanya kazi zao kwa uhuru na kuongeza ubora wa kazi zao.

Tatizo lingine ambalo lipo wazi kwa waigizaji wetu na watengenezaji wa filamu wa Tanzania,wao wanafikiri wakishaonekana kwenye vituo vya televisheni ndio kilele cha mafanikio yao. Wakati ukweli wanaishia kupata umaarufu bila kuwa na pesa. Mpaka wakati naandika makala hii naambiwa kwamba kwa jiji la Dar es salaam peke yake kuna vikundi vya uigizaji zaidi ya mia tatu 300 ambavyo vimesajiliwa lakini vyote vinasubiri kufanya kazi na vituo vya TV ambavyo havifiki saba.



Naamini watu hawa wangetegenezewa soko la ndani, na kujitahidi kutengeneza kazi zao katika kiwango kinachovutia,Wasingekuwa na ndoto za kusubiri vituo vya luninga. Watu wangetafuta masoko ya kazi zao kwenye maduka na wangeuza hata nje ya nchi.Kitu kingine ambacho naamini kwamba kitaweza kuinua kiwango cha sanaa ya uigizaji,ni mafunzo kwa waigizaji wenyewe. Kwa mfano nikiangalia filamu za Nigeria kitu cha kwanza kinachonivutia ni namna waigizaji wao walivyo makini na nidhamu kwa kile wanachotakiwa kuigiza. Kwa watu kama mimi,ambao tunapenda kuangalia makosa katika kazi za wenzetu,tunashindwa kabisa kuwakosoa wanaigiza katika uhalisia wote.
Lakini hapa kwetu inaonekana sivyo.Watu hawatumiwi kulingana na uwezo wao bali ni kwa urafiki na kujuana, matokeo yake wanapewa nafasi ambazo ukiziangalia zinaonekana kuwapwaya kabisa.

KAZI YA UPIGAJI WA PICHA ZA FILAMU
Kama nilivyoeleza mwanzo kwamba kazi ya upigaji wa picha za filamu sio kitu chepesi, katika filamu mpiga picha huchukua picha moja kutoka katika kona tofauti tofauti na anapokuwa studio huzichanganya na kutafuta kona iliyotoka vizuri na kuleta ladha nzuri kwa mtazamaji.
Makosa mengi na mafanikio tunayoyaona katika filamu zetu yanatokana na wasimamizi ingawa katika filamu sifa nyingi anapata muigizaji lakini ukweli ni kwamba kuna kundi kubwa la watu walio nyuma yake wanaomuelekeza nini cha kufanya. Na kama hawajaridhika na kipande chochote cha filamu hakiwekwi katika filamu au watarudia upigaji wa kipade hicho cha filamu mpaka kiendane na mawazo ya mtayarishaji.

WATANZANIA WANABADILIKA
Siku hizi watanzania wameanza kuwa na tabia ya kupenda na kuthamini vitu vyao kama huamini hebu angalia nidhamu inayokuwepo nyumbani wakati familia inaangalia michezo ya kuigiza katika luninga hata kama walikuwepo watoto wasumbufu wanaodeka ikifika wakati huo wote wanatulia kabisa
Ili kuleta heshima kwa filamu za Kitanzania ni muhimu sana kwa kundi la watengenezaji wa filamu ambalo linawahusisha waongozaji wa filamu, (Directors), watunzi wa hadithi (Story writers) wataalamu wa mavazi (Costume designer), wataalamu wa kubadili maumbo (make up people) watengenezaji wa mandhari (set designer) wasanii (actors), n.k. Katika ushirikiano huu lengo kubwa ni kuendeleza mawazo yaliyozalishwa na mtu mmoja kuhusiana na lengo la filamu husika.
INATAKIWA MIKUTANO YA KUTOSHA.
Wakati wa kutengeneza filamu,Mara nyingi hutumika mikutano na majadiliano ya pamoja ya mara kwa mara ili kuhakikisha kila msanii ameelewa vizuri lengo la filamu,na pia katika mikutano hii inasaidia sana urahisi wa kutafuta wafanyakazi wenye ujuzi mzuri kwa sababu wataalamu hawa wanakuwa wanajuana vizuri, hivyo watapatikana watu wenye ujuzi unaokubalika.

Wakati filamu inatoka katika hatua ya kabla ya uzalishaji,watunzi, waongozaji na watu wote wanaohusika katika hatua za mwanzo za uzalishaji wa filamu. Wataandaa  mpango wa kuelezea namna wanavyotaka kuwasilisha ujumbe wao na mfumo wa vitendo (Action) kwa kila sentensi itakayotamkwa, kwa mfano utasema neno fulani wakati ama umeshika glass, na utakapoanza kumimina utamalizia na sentensi fulani. Na mpangilio wa maandishi ya wahusika yatakavyoonekana kama wanavyopanga katika maamuzi yao.
katika hatua hii ndipo hupangwa wasanii na nafasi watakazoigiza vifaa na vitu muhimu vitakavyohitajika katika kila kipande cha filamu scene ya utengenezaji wa filamu.
MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOANDIKA HADITHI ZA FILAMU
Ninachowashauri waandishi wa hadithi za filamu za Tanzania. Ni Kutulia kwa makini sana na kuzingatia kanuni zinazotakiwa. Wasiwe wavivu katika kutafuta undani wa tatizo tunapoandika hadithi za filamu kwa sababu uzuri wa filamu unaanzia katika hadithi na hubebwa na waigizaji. Kumbuka kuwa kabla ya kuanza kutayarisha hadithi ya filamu jiulize na kujibu kwanza masuali yafuatayo;-
1.   jamii ina tatizo gani?.
2.   je tatizo hilo linajulikana kwa jamii unayoilenga?
3.   kama linajulikana walichukua hatua gani?
4.   je hatua walizochukua au wanazochukua zinasaidia kutatua au hapana?
5.   kama hazikuwasaidia je wewe unawashauri wafanye nini?
Majibu ya maswali haya yote ndio msaada mkubwa sana kwa mtayarishaji katika kutayarisha maudhui (Theme) ya filamu yake. Na ni lazima afahamu kwamba, hatimaye atatakiwa aonyeshe anataka kutoa ushauri gani juu ya jambo hilo katika hisia zake. Na anataka hatima ya jambo hilo iweje katika hisia zake,na anataka hatima ya jambo hilo iweje kwa mtazamo wake.
Katika hatua ya uzalishaji wa filamu