Alhamisi, 9 Agosti 2012

KWA HERI MAMA ESTER ANDREW PARK NA GRACE MEE JEE

KWA HERI MAMA ESTHER KYUNG PARK.nakumbuka ilikuwa siku ya  tarehe 11 Nov 12 asubuhi wakati najiandaa kwenda kazini nilipigiwa simu kutoka kwa mmoja wa rafiki yangu wa karibu na kwa kweli huwa hana kawaida ya kunipigia simu mapema asubuhi kiasi hicho. moyoni nilianza kuhisi kuna taarifa mbaya na ndivyo ilivyokuwa kwangu. ilikuwa ni habari ya msiba wa mama Ester Park. ilikuwa ni siku mojawapo niliyoiona nzito sana kwangu na nilijipanga vizuri kuhakikisha ninakuwa karibu na mchungaji Andrew Park na ilinibidi kufika nyumbani kwake mapema kidogo ambako nilimkuta akifanya mawasiliano na ndugu zake mbalimbali ambao wapo nje ya Tanzania. hali niliyomkuta nayo ilinitia moyo sana alionekana mtulivu sana na kama mtu aliyekubali kwamba Mungu ametwaa mojawapo ya matunda yake. sikuweza kuwa na maneno mengi zaidi ya kumshukuru Mungu.
Wachungaji wa Tanga wakishirikiana na Watumishi wa Korea Kusini wakibeba jeneza lenye mwili wa mama Ester Park kuupeleka katika mahali atakapopumzika milele nje kidogo ya jengo la kanisa hilo. msiba huu uliwakutanisha watumishi wengi kutoka ndani na nje ya mji wa Tanga.
Mwili wa Mama Park ukishushwa katika mahali palipoandaliwa kwa ajili ya kupumzika kwa amani na alipumzika katika kaburi lililochimbwa nje ya kanisa lake eneo la Kange Tanga


Rev George Nywage na Mchungaji Bright Mashauri wakimtuliza mtoto mdogo wa Marehemu ambaye aliumizwa sana na msiba huu wa kumpoteza mama yake kipenzi watoto hawa muda mfefu wameishi mbali na wazazi wao wanaishi Marekani.

Picha ya Marehemu Ester Park ikiwa juu ya Jeneza lililobeba mwili wake muda mfupi kabla ya mazishi yake. tunamshukuru Mungu kwa ajili ya huduma yake ambayo ameifanya kwa nchi yetu ya Tanzania. Tulimpenda kwa sababu alikuwa ni mtu anayependa watu. mtu muwazi na aliyependa na kuheshimu utamaduni wetu kama alivyo mchungaji Andrew Park aliyekuwa mume wake tunaamini kwamba mama yetu amepumzika kwa amani akisubiri siku ambayo parapanda litakapolia. pumzika kwa amani mama yetu Ester Park
Mchungaji Andrew Park akiwa na watoto wake wanaoishi Marekani ambao walikuwa wanasubiriwa ili waweze kumzika mama yao. Aliye katikati ni mtoto mkubwa wa  Marehemu ambaye alitoa hotuba iliyotusisimua sana watu wengi waliohudhuria ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu. kwanza kabisa alituhakikishia kwamba ana uhakika kwamba sisi tuna huzuni lakini Mungu anashangilia kumpokea mama yake katika ufalme wake. lakini pia alielezea mahusiano yao yalivyokuwa ya karibu mno na mama yao na jinsi alivyojitoa kwao. alitusimulia mkasa mmoja ambao uliwapata walipokuwa wadogo na mama yao aliwapeleka kutembea  katika eneo fulani ambalo watu wanalitumia kwa kuteleza kwenye barafu,akasema yeye na mdogo wake walikuwa hawajatulia vizuri kwa maana ya kwamba walikuwa watundu na katika utundu walijikuta wanateleza na kutumbukia kwenye shimo lakini mama yao aliwahi kuwazuwia na kuwaokoa lakini yeye mama yao alitumbukia na kuvunja mkono. haya ni maneno machache sana katika hotuba ile yaliyonisisimua sana na kujifunza kwamba watoto unapowafanyia kitu kizuri watakikumbuka daima.







Ester na Chimpae marafiki wa Grace Mee Jee
baada ya kupita muda si mrefu tulipata tena msiba ambao ulitufanya kuduwaa, ulikuwa ni msiba wa mama yetu Grace Mee Jee ambao ulitokea nyumbani kwao Korea ya Kusini na ulichomwa moto kama ilivyo kwa jadi yao na baadae kuzikwa katika jiji la Tanga kama ambavyo walikubaliana na mume wake Rev James Lee. kama wanavyonekana katika picha wakiwa pamoja na mama Grace
Mama Grace atabaki anakumbukwa daima kwangu mimi, na kwa familia yangu kwa sababu alikuwa rafiki wa kweli. Alijitahidi sana kuonyesha upendo wa waziwazi kwangu na kwa familia yangu, alinifundisha mambo mengi hasa yanayohusu maadili na tabia njema. alitumia muda mwingi kunifundisha ustaarabu wa kwao. Najua kwamba kiuchumi walikuwa vizuri kuliko mimi lakini waliniheshimu kwa sababu na mimi sikutaka kujiweka chini sana nilihakikisha kwamba na mimi nafanya kila juhudi kuwaonyesha kwamba na mimi nina uwezo japo mdogo na ninaweza kuwasaidia na kuwapa zawadi kama ambavyo wao pia wananipa. nilitaka kufuta mawazo ya watu wa nje hasa ulaya na mashariki ya mbali kwamba watu weusi ni watu wa kusaidiwa tu na kuombaomba
wakati mwingine urafiki wetu ulipita katika nyakati ngumu lakini tangu Mungu aniunganishe nao, niliazimia kwamba sitakuwa mtu wa kujipendekeza kwao na nitawashauri bila woga wala unafiki. na ninamshukuru Mungu kwamba ndivyo ilivyokuwa, sikuwahi kuyumba katika kuwashauri hata kama walikuwa hawakubaliani na mim, lakini baadae walikuja kujua kwamba, niliwashauri katika mambo ya kweli katika kila eneo la maisha yao. ilikuwa ni ngumu kwa sababu wakati fulani unawakuta wameshafanya uamuzi juu ya jambo fulani, na ninafika na kupangua kwa hoja na kuweka wazi na hatimaye wanabadilisha uamuzi au wanaamua kuendelea na uamuzi wao. na wakiendelea na maamuzi yao ni lazima wewe uonekane mbaya, lakini baada ya muda wanakuja kukutana na vikwazo ulivyowaambia.
Kapumzike kwa amani rafiki yetu. Mungu atakukumbuka kwa mema ambayo umewatendea watu mbalimbali ambao umeishi nao. najua hujafa kwa ghafla bali umeugua kwa muda mrefu. Hapana shaka ulipata nafasi ya kutengeneza njia yako mbele za Mungu. Na kumuomba msamaha katika maeneo ambayo huna uhakika kama ulifanya vizuri. Na kwa sababu hiyo Mungu atakufufua siku ya hukumu. KWA HERI RAFIKI YANGU GRACE MEE JEE
GRACE katika siku zake za mwisho wakati akiwa hospitali nchini Korea Kusini







NGUVU YA UUMBAJI


                          NGUVU YA UUMBAJI 
Biblia inasema;

"Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri".(Waebrania 11:3)

Biblia inatuonyesha kwamba hapo zamani Mungu alikuwepo peke yake na baadae aliviumba vitu vyote hivi tunavyoviona na visivyoonekana. Wakati Mungu anaiumba hii dunia hapakuwa na mahali alipokwenda kuchukua udongo,kokoto  na mawe ili aje aiumbe hii dunia. Siku hizi watu wanashindana kujenga majumba makubwa sana yenye kutisha, lakini wakati wanajenga inabidi walete udongo, mawe, kokoto mchanga nondo n.k. ndipo wajenge. lakini wakati Mungu anaiumba hii dunia hapakuwa na kitu chochote ambacho Mungu angeenda kukichukua kama vile udongo,mawe,vyuma n.k. Mungu alikuwa anasema neno lake tu na baada ya kusema kile alichosema kilitokea. hebu  anagalia Biblia mwanzo sura ya kwanza wakati wa uumbaji utaona ni namna gani Mungu aliiumba hii dunia utaona kuwa Mungu alisema neno tu, 
"Mungu akasema iwe nuru ikawa nuru" (Mwanzo 1:3
"Mungu akasema liwe anga likawa anga n.k. mifano ni mingi sana inayoonesha jinsi Mungu alivyoiumba hii dunia na vitu vyote vilivyomo kwa kutumia neno lake.
Mungu alikuwa anasema neno na baada ya kusema kitu hicho kinatokea hii ni sawa na neno la Mungu katika injili ya Yohana 1.1,4 "Hapo mwanzo kulikuwako Neno, Naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu."
hapa tunaona tena kuwa ndani ya neno kulikuwamo uzima neno analolisema Mungu ndani yake umo uweza,ndani yake kuna nguvu ya uumbaji. Mungu anaposema neno,ile nguvu ya uumbaji ya kiungu inatoka katika lile neno na kwenda kukitengeneza kile kitu ambacho kimetamkwa hii ndio maana Mungu alikua anasema neno wakati anaumba,na si wakati anaumba tu bali katika utendaji wowote wa
Mungu hutenda kwa kusema  neno tu
Mungu alimtuma Yesu hapa duniani aje kufanya kazi yake
pamoja na kazi ya kuhubiri na kufundisha neno la Mungu. Yesu alikuwa anaponya wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali. Yesu alizifanya kazi hizi zote kwa kutumi neno lake peke yake. Yesu hakutumia nguvu ya mwili au elimu ya dunia kuwaponya wagonjwa. Wagonjwa  wengine kwa elimu ya dunia ingebidi wafanyiwe upasuaji pengine mama ameshindwa kujifungua au pengine mtu amevunjika mifupa n.k.   

wagonjwa wengine ingebidi wachomwe sindano na wengine wanywe vidonge n.k. lakini tunaona Yesu alikuwa anasema neno lake tu wale wagonjwa wanapona  hapohapo. Mungu alipomtuma Yesu hapa duniani aliweka nguvu yake ya uumbaji ndani yake na  ni nguvu ileile aliyoitumia wakati anaiumba dunia hii bila kupungua hata chembe moja ndio na ndio hiyohiyo aliyoiweka ndani ya Yesu. Wachunguzi wa Biblia wanatuhabarisha kwamba Yesu kimwili alionekana kama amedhoofu sana. Hakuwa pandikizi la mtu alionekana amekonda sana katika hali ya kimwili watu wasingemtumaini kwa lolote. Na hii ni kwa sababu muda mwingi alikuwa hali chakula na ushahidi unaonekana katika maukio mengi tu. Mfano alipofika kwa 
 
Martha na Mariamu alikataa wasishughulike na mambo ya kupika chakula alitaka wasikilize kwanza neno la Mungu,tunaweza kuona pia hata katika kisima cha Yakobo,ulikuwa ni wakati wa chakula cha mchana. Aliwaruhusu wanafunzi wake waende kula chakula yeye alibaki pale akimhubiri Yule mama wa kisamaria neno la Mungu. Pamoja na kuonekana kimwili kuwa amedhoofu,lakini lijua kuwa ndani yake kuna uweza wa Mungu ambao iwapo atasema neno ile nguvu itatoka na kwenda kufanya kile alichokisema. Kuna sehemu tunaona akiwa na wanafunzi wake akasema tuvuke twende ngambo hapa walipanda kwenye jahazi lakini wakiwa katikati ya bahari upepo mkali wenye dhoruba ukaja ukataka kuwazamisha baharini. Lakini kama unavyojua kwamba baadhi ya mitume walikuwa ni wavuvi wa 

samaki,kwa hiyo walikuwa wanajua sana mambo ya ubaharia na hivyo walijua mbinu ya kufanya inapotokea hali kama iliyotokea. Lakini baada ya upepo huo mbaya kuja mitume wenye ujuzi wa mambo ya baharini wlijitahidi kufanya kila linalowezekana lakini baadae mbinu zao zote zilishindikana,wakati wote huo Yesu alikuwa amelala wakamuamsha. Wanafunzi wa Yesu walikuwa wameshamuona  Yesu akifanya miujiza mingi kma kuponya wagonjwa,kutengeneza mikate kufufua wafu,kutoa mapepo n.k. wanafunzi wa Yesu walikuwa hawajamuona Yesu akikemea upepo na ukatii,siku hiyo Yesu alikuwa amelala wale wanafunzi baada ya dhoruba kutokea  hawakuhitaji kumuamsha mapema kwa sababu walijua hatawasaidia kwa lolote, hawakujua kwamba upepo pia unaweza kumtii,wao walijua kuwa Yesu anawea kuponya na kutengeneza mikate tu.
Lakii kuhusiana na upepo hawakujua kuwa ana uwezo wa kuutuliza ndio maana hawakumuamsha mapema. Unajua kwamba wavuvi wa samaki huwa ni watu wenye nguvu,mapande ya baba,ni watu wenye mazoezi ya nguvu kwa sababu ya shughuli zile wanazozifanya za kupiga makasia na kuvuta jerife,hivyo hao watu  wenye miraba mine na ujuzi wa baharini baada ya kuwa wamekwama kabisa ndipo walipoamua kumuamsha Bwana Yesu ambaye sio bonge la mtu na ambaye hana nguvu na anaonekana amedhoofu kiasi hata hwezi kupiga makasia,wale wanafunzi wapomwamsha hawakumwamsha kwamba wanategemea wokovu 

fulani kutoka kwake bali walikwa wanamjulisha aone jinsi wanavyoangamia Biblia inasema;- "Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia Mwalimu si kitu kwako kuwa tunaangamia"? (Marko 4:38) . Yesu alipoamka yeye hakuwa na hofu wala hakuanza kuuliza maswali na kujitetea kuwa yeye hana ujuzi wa bahari au  kujiuliza maswali ya kwa nini wale wenye miraba minne wameshindwa je yeye ataweza. Yesu alijua alichokuwa nacho ndani yake na kwamba yeye alichotakiwa ni kusema neno tu Biblia inasema;- "Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu."(Marko 4.39 mitume waishangaa sana kuona kuwa upepo na bahari vimemtii Yesu "Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepona bahari humtii" (Marko 4.41) Yesu alipokutana na mtu ambaye ana ulemavu wa macho (kipofu Yesu hakuhitaji kuwa na vifaa vya upasuaji ili aweze kufanya oparesheni ya jicho,alichofanya ni kusema na aliposema Yule mtu alipona dakika ileile. Hali kadhalika alipokutana na mama ambaye ana ulemavu wa mkono yesu hakuhitaji kufanya upasuaji wa kuinyoosha na kuipanga mifupa yake. yeye alichofanya ni kusema na mara moja mkono huo ulinyooka. Wakati wote huu Bwana Yesu alikuwa anatengeneza wanafunzi watakaochukua nafasi wakati atakapoondoka,na akiwa nao kuna siku moja aliwachukua wanafunzi sabini akawatuma katika vijiji mbalimbali ambavyo alikusudia yeye mwenyewe kwenda na aliwapa mamlaka na walipokwenda na kurudi walishangaa sana jinsi ambavyo nguvu za Mungu zilivyotenda kazi ndani yao. Na Bwana Yesu aliwaambia hicho ni kitu kidogo sana. "Tazama nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."(Luka 10:19 na Luka 9:1.) Yesu alipoondoka na kurudi alikotoka altuachia nguvu yote iliyokuwemo ndani yake bila kupungua hata chembe moja na ni nguvu ileile ambayo ilitumika kuumba ulimwengu. Yesu aliiweka nguvu ya uumbaji iliyomo ndani yake aliiweka ndani yetu ili tuendelee kuzifanya kazi alizokuwa anazifanya. Ni lazima mtu wa Mungu ufahamu kwamba nguvu ileile iliyomo ndani ya Yesu ipo pia ndani yako wewe bila kupungua. Yesu anataka watu waitumie hiyo nguvu kufanya mambo makubwa kuliko aliyoyafanya yeye "Amin, amin nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba" (Yohana 14:12.) watu wa Mungu tumezungukwa na nguvu kubwa sana ambayo shetani hataki tuijue watu wengine waligundua kwamba hata vivuli vya watu wa Mungu vinaponya ilibidi wapange wagonjwa kwa kufuata uelekeo wa kivuli cha mtu wa Mungu na walipokea uponyaji. Hata nguo na vitambaa vya watu wa Mungu vina nguvu na watu wamevitumia na kupokea uponyaji. 

MUNGU AKUPE UFAHAMU WA KUJUA SIRI ZAKE.

HARUSI YA ISABELLA MWAKASEGE

Isabella na Ibrahimu wakiwa katika ibada ya ndoa
Isabella Philip Mwakasege
Wandugu jamaa na marafiki waliohudhuria harusi wakiwa pamoja na maharusi baada ya kufunga pingu za maisha huko Arusha
Isabella na mchumba wake Ibrahim wakiwa pamoja na rafiki zao katika safari ya kwenda Arusha kufunga pingu za maisha
Mimi pamoja na mke wangu Flora na mtoto wetu Stella tunawatakia maisha yenye heri na baraka kutoka Mungu muumba mbingu na nchi mdogo wetu Isabella na mpenzi wake Ibrahimu, uhusiano wao ulituonyesha kwamba kweli wanapendana na wamedhamiria kuishi maisha ya kumtegemea Mungu kwa asilimia zote. tunawakubali tunawapenda na tunaheshimu uwezo wenu wa kuamua jambo lenye heri na uwezo wa kusimamia uamuzi wenu.
hapa ni siku ile ambayo waliamua kuweka mambo yao hadharani kwa kuwatangazia ndugu jamaa na marafiki kwamba wanapendana na wameamua kwamba wataishi pamoja Ibrahim akimvalisha Isabela pete ya kufunga uchumba

Ibrahimu na Isabella baada ya kufunga ndoa wakiwa katika mapumziko mafupi hukohuko Arusha.




































TUNAYO MAMLAKA


TUNAYO MAMLAKA

Mungu ametupa mamlaka juu ya shetani na kwa kuwa tumepewa  mamlaka hayo,Mungu ametukabidhi sisi wenyewe uweza wa kumharibu na kumsambaratisha shetani na kazi zake kila tunapokutana naye. 

Kwa hiyo tumia mamlaka uliyopewa kubomoa ngome za shetani vunja vunja nguvu zake na mipango yake mfunge shetani sambaratisha shughuli zake. Yak 4.
Katika kila jaribu nyuma ya hilo jaribu kuna pepo.
·        Huyo pepo ndiye anayesababisha hilo jaribu kuwepo.
·  Kwa hiyo basi unashauriwa usipigane na  na jaribu hilo, bali pigana na Yule pepo anayesababisha hilo jaribu.
·        Hii ni sawa na ugonjwa, mtu akiwa mgonjwa  akienda hospital daktari hutafuta kile kijidudu kilichosababisha huo ugonjwa. Baada ya kukijua ni kijidudu ganikinachosumbua,daktari humpa mgonjwa huyo dawa yenye uwezo wa kukiua hicho kijidudu.
na baada ya kukiua hapo ndipo ugonjwa unaomsumbua huyo mtu hutoweka.
Kwa hiyo wewe pigana na pepo aliyesababisha jaribu usipigane na jaribu lenyewe bali pigana na ile roho ovu iliyosababisha jaribu hilo na wala usipigane na tatizo.
Watu wengi hupigana na jaribu badala ya kupigana na pepo, biashara yako inapojaribiwa  wewe pigana na hilo pepo linaloshambulia hiyo  biashara yako kwa kutumia mamlaka uliyonayo.
Mfunge shetani mtupe kuzimu, Usikubali kushindwa na shetani. neno la Mungu linatuagiza kumpinga shetani naye atatukimbia.
Unapokutana na shetani sio wakati wa kukimbilia kwa Yesu au kwa Mungu huo ni wakati wako mwenyewe kutumia mamlaka uliyopewa na Mungu.
·        Watu wamekuwa wakimwita Yesu katika kila hitaji.
·        ni kweli yapo mambo ambayo Mungu ametaka tumwite.
lakini unapokutana na shetani Mungu amekuagiza  umpinge wewe mwenyewe naye atakukimbia.
·        usipompinga shetani hataweza kukukimbia kwa maana hiyo jaribu halitaondoka.
·        litaendelea kwa maana hujamfukuza aliyesababisha hilo jaribu.
Hebu fikiria mtu akiwa amepagawa na pepo aletwe kwako umuombee lakini maombi yako unamwambia Yesu aje kumtoa huyo pepo au unamwambia Mungu aje kumtoa huyo pepo. Hilo halitawezekana Utamaliza miaka kumi ukiomba huyo pepo hatatoka.
 lakini siku ukiamua kumwamuru atoke kwa kutumia mamlaka uliyonayo kwa jina la Yesu huyo pepo atatii na kuondoka.
·        Hii ni kwa sababu Mungu ameagiza hivyo Mungu amesema tumpinge shetani naye atakimbia.
·        Mungu hajasema tumuite yeye Mungu au Bwana Yesu aje ampinge shetani.
Yesu alisema Kwa jina langu mtatoa pepo( Marko 16.17) tumia mamlaka uliyopewa kutoa mapepo kwa jina la Yesu.
·        Toa pepo wewe siyo umuite Mungu aje atoe pepo. Ni sehemu nyingi katika maandiko Mungu ametuagiza tumshinde shetani sisi wenyewe,
Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani (Waefeso 6.11). hapa ina maana kuwa kama hujavaa silaha hutaweza kumpinga shetani. Hii ni pamoja na kuishi maisha matakatifu. Ni pamoja na uombaji wa kiwango cha kupata mpenyo. YAPO MAANDIKO MENGI YENYE KUTUAGIZA KWAMBA TUTAMSHINDA SHETANI SISI WENYEWE.
Mwisho
 
ELIYA MTISHBI ALIJUA KUTUMIA MAMLAKA 1Wafalme 17.1
Katika maandiko haya tunamuona Eliya anamtambia mfalme Ahabu kwamba mvua haitanyesha mpaka aseme yeye. Eliya alifanya hayo kabla hata jina la Yesu halijaletwa. Sisi tuna mamlaka na tuna jina lenye nguvu la Yesu unachotakiwa ni kusimama tu kwenye zamu yako. Watu wamemuasi Mungu maovu mengi yanfanyika, maonevu mengi yanafanyika na wenye  wanafanya maovu hakuna wa kuwakemea hakuna wa kuwaonya  maana hakuna  watu wa Mungu wenye kuibeba mamlaka. Watu waMungu wamejichanganya kwenye dhambi na Mungu amewanyanganya mamlaka yake kama alivyomyanganya lusifeli,inatakiwa watu wamuogope Mungu wako. Watu wote wamuheshimu Mungu wako kazini kwako wafanyakazi wenzako wakubwa wako kazini hata wakuu wan chi wanatakiwa wamuogope Mungu wako pia. Watu wanahubiri injili isiyokuwa na mamlaka wala nguvu ya Mungu,waaogopa hata kukemea maovu. Injili wanaihubiri lakini watu walioko kanisani kwao bado wamefungwa na shetani,ni wagonjwa na masikini n.k.
Mtume Paulo anasema katika Rumi 1.6 huu sio uweza wako hata uone haya kuutumia . ni uweza wa Mungu,Mungu ndiye ameuweka uwezo wake ndani yako,wewe kazi yako ni kuupalilia kwa maombi na kuutunza kwa kuishi maisha matakatifu. Tena si kwamba uko kwa viongozi wa dini tu,hapana ni kwa kila aaminiye. Katika kanisa la kwanza kulikuwa hakuna cha kiongozi wala cha muumini wote walikuwa motomoto cha msingi ni kusimama kwenye zamu yako. Paulo alibarikiwa sana na uweza wa Mungu,akawaombea hata wale ambao pengine macho yao kiroho ni vipofu hawalijui hili hili kwamba wanayo mamlaka ndani yao anagalia waefeso 1.17,23 kisha angalia 1Wakorintho 12.6 kila mwamini ni kiungo katika mwili wa kristo na kristo yeye ni kichwa,kiwiliwili chake ambacho kina kina viungo vingi hicho ndicho kanisa. Ndio waamini mbalimbali wote duniani, huyu ni mkono huyu ni ukope huyuni kucha mwingine ni nywele ,utumbo,miguu n.k.
Yesu ni kichwa kiwiliwili chake  ndio watu wa Mungu,Mungu alimuweka Yesu juu sana kuliko ufalme wote,mamlaka,nguvu,usultani na kila jina litajwalo akavitia vitu vyote chini ya miguu yake kwa ajili ya kanisa. Wewe ndugu ni kiungo fulani katika mwili wa Kristo,Kristo yuko juu ya vitu vyote,aliwekwa hivyo kwa ajili yako wewe uliye kiungo katika mwili wake. Kama Yesu yuko juu,viungo vyake pia viko juu. Kuna msemo mmoja wa kishetani usemao kwamba shetani kajiinua juu ya jambo fulani,wewe mtu wa Mungu shetani yuko chini yako daima labda ukitoka ndani ya Yesu,shetani anajua nafasi yake ya kukaa chini miguu yako,hawezi kujiinua ,hana uwezo huo,bali wewe mwenyewe ambaye unao uwezo juu yake ndiye unaweza kumuiua aje juu yako. Usikubali kukiri hivyo tena kwamba shetani kajiinua. Huo ni msemo wa watu wa dini za kikristo, wakristo hao wanapookoka wanahama na msemo huu na kuingia nao katika wokovu mtume Paulo anawaombea waamni ili wafunuliwe wajue jinsi walivyo juu ya shetani. Tuko juu kuliko jina lolote litajwalo,kuna majina mengi saa ya kutisha hapa duniani,majina kama malaria ,Ukimwi ,Ebora saratani n.k. pamoja na kwamba tumewekwa juu ya kila jina litajwalo mtume Paulo alipogundua siri hii alifurahi sana ,uwezo huu ukamfanya aseme siionei haya injili ya Kristo. Hata wewe huwezi kukionea aibu kitu cha thamani namna hii. Nchi zenye bomu la nyuklia zinajigamba sana kwa sababu zinajivunia nguvu za bomu la nyuklia.lakini sisi tuna nguvu kubwa katika ulimwengu wa r oho kuliko bomu la nyuklia.
Tupo juu ya kila jina la mtu mashuhuri yeyote aliyepo na atakayekuja. Askari trafiki anasimamisha lori kubwa linaloendeshwa na jitu la miraba minne kwa kunyoosha mkono wake tu. Haijalishi hata kama ni kasichana kadogo tu,tena hana bunduki na yuko peke yake tu. Hata kama gari hilo lipo katika kasi kubwa kiasi gani dereva atahangaika mpaka atasimama. Kinachosababisha asimame ni mamlaka aliyonayo trafiki ambayo kimsingi sio yake binafsi bali ni ya serikali. Hata sisi katika ulimwengu war oho tuko na mamlaka zaidi ya trafiki. Sisi tuna mamlaka ya kifalme kila kitu kinatii,umewahi kusikia wapi kwamba mfalme anabishana na raia,na ni afadhali raia lakini shetani ndio hawezi kabisa kwetu hizi ni nyakati za shetani kupigwa kuliko wakati wowote ule aliowahi kuwepo hapa duniani,Mungu ameshusha nguvu kubwa sana ya lala salama angalia Yohana 14:12. ni afadhali shetani akutane na Yesu kuliko kukutana na mwamini anayejua kutumia mamlaka yake kikamilifu. Yesu anatutumaini sisi tufanye kazi kubwa zaidi kuliko aliyoifanya yeye.
KWA MUUMINI AMBAYE UWEZA UMO NDANI YAKO INAKUPASA KUJIHESHIMU KAMA CHOMBO KILICHOBEBA KITU CHA THAMANI.
Kwa vile nguvu hii hukaa katika kinywa chako basi unatakiwa kuchunga sana maneno unayozungumza. Maneno yako ni ya thamani sana tofauti na watu wengine wasiomwamini Yesu. Usiwe mtu mwenye kuropoka maneno yasiyo na maana,usiwe mtu wa kusogoa sogoa maneno kwenye vijiwe visivyo na maana. Unapoongea tafakari na kulipima kwanza neno unalotaka kulisema kama litampedeza litampendeza Mungu au  halitampendeza. Angalia Mathayo 12.36,37
Maneno yako yataamua uingie mbinguni au usiingie. Hii ni pamoja umeokoka na umeacha kutenda hambi zingine,lakini bado utahukumiwa kutokana na maneno yako. Lakini watu wa Mungu wengi hawalijui hili. Wanajali zaidi kuacha dhambi zingine lakini bado midomo yao ni michafu sana. Wanaitumia kulaani na kuwaangamiza watu wengine. Utakuta mchungaji anaposhindwa kuelewana na muumini wake katika eneo fulani yeye anakimbilia kulaani. Muumini ni mtoto wako,hata akikukosea ni mtoto wako tu.hata kama atahama kanisa linguine bado ni talanta yako tu utalipwa hiyo talanta. Sasa wewe umetofautiana na muumini wako kiroho unakimbilia ile fimbo yako ambayo umepewa ili upigie nyoka,unampigia muumini wako. Muumini wako ni mtoto wa Mungu ukimpiga kwa fimbo na wewe subiri kupigwa rungu la Mungu wewe mzazi baba au mama jifunze sana kubariki watoto wako 

na watu wote wa nyumbani kwako. Acha mambo ya kuwalaani kabisa,baba usimlaani mke wako wala mama usimlaani mume wako acha unaoishi nao wawe na furaha na amani bila kuogopa kulaaniwa. Kama kuna makosa wanayoyafanya yashughulikie kwa njia nyingine na wala sio ya kuwalaani angalia Yakobo (3:2-12) yaliyomo moyoni mwako ndiyo ambayo hukutoka,wewe ni mtu wa Mungu hakikisha unazungumza maneno yanayompeneza Mungu. Sio wewe mmoja uzungumze maneno yanayompendeza Mungu tena wewe huyohuyo mmoja unazungumza maneno yanayompeneza shetani.
                                           MWISHO.

Jumatano, 8 Agosti 2012

SOMO : KUNYAMAZA KIMYA



MWL Furaha Amon


Utangulizi

Kuabudu ni jambo pana sana kuliko watu wengi wanavyo lifahamu. Watu wengi wanafikiri kuabudu kunaishia kwenye kitendo cha kufanya ibada au misa peke yake. Ibada au misa ni sehemu ndogo sana katika kuabudu. Kuabudu ni maisha unayoishi. Kuabudu ni maisha unayoishi. Kuabudu ni kuishi maisha fulani. Kuabudu ni mtindo fulani wa maisha ambayo Yule Mungu unayemwabudu anakutaka uyaishi. Hivyo siyo swala la kwenda  kanisani kwenye ibada au misa na ukishaondoka huko kila kitu unakiacha kanisani. Mungu unayemwabudu anakutaka uishi maisha ya aina fulani hata unapokuwa nje ya ibada, huwezi kuishi maisha ambayo hayafanani nay ale anayoyataka unayemwabudu halafu wewe ukazingatia ili mradi unahudhuria katika misa na ibada peke yake. Kuishi maisha yale anayoyataka Mungu huko ndiko kumcha Mungu. Kwa maana hiyo sehemu kubwa ya kuabudu Mungu iko nje ya nyumba za ibada zetu. Ni jinsi unavyoishi na watu huko nyumbani kwako, majirani zako, mtaani kwako, kazini pamoja na sehemu mbalimbali za maisha ya kijamii. Mungu wetu ana jinsi fulani ya anavyotaka watu wake waishi huko katika maisha ya nje na ibada. Hebu tuangalie mfano wa mambo machache tu yafuatayo;-


Biblia inasema,
Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao (Waebrania 12:14).
Mcha Mungu anatakiwa asiwe na ugomvi, chuki, kinyongo na mtu yeyote. Na kama hali kama hiyo inajitokeza ni lazima ahakikishe anatafuta kwa bidii kuwa na amani na huyo mtu hata kama mazingira yanakataa.
Biblia inasema,
Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi, nanyi mtakuwa wana wa aliye juu. Kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi iweni na huruma, kama baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa (Luka 6: 35-38
Upendo wa mcha Mungu sio wa hiari bali ni amri wala siyo ombi. Utake usitake Mungu anatulazimisha tuwapende watu wote pamoja na adui zetu.
Biblia inasema;-
Heri mtu Yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala hakusimama katika njia ya wakosaji wala hakuketi barazani pa wenye mizaha (Zaburi 1:1).
Hayo ni maisha anayotakiwa kuishi mcha Mungu. Mambo hayo niliyoyataja ni baadhi tu ya mtindo wa maisha ambayo Mungu anataka tuishi. Kuna mambo mengi ambayo Mungu anamtaka mtu anayemcha Mungu aishi kwa hayo.
Madam Vick Shedafa
Hivyo kuabudu Mungu siyo ibada peke yake bali ni aina ya maisha. Hivyo kwa kifupi ni kuwa, kuabudu siyo ibada pekee, bali hata katika maisha ya nje ya ibada. Lengo la somo hili ni kuzungumzia kumwabudu Mungu katika ibada ya maombi. Zaidi nitazungumzia kumwabudu Mungu kwa maombi baada ya mwombaji kufika kileleni katika maombi yaani Patakatifu pa patakatifu. Kabla ya kuedelea mbele kwanza nigusie kidogo kuhusu ibada. Ibada ni lazima iwe katika kiwango cha patakatifu pa patakatifu. Hii ndiyo ibada ambayo Mungu atakutana na shida za watu. Ibada inapokuwa ya mwilini au kwenye nafsi, Mungu hawezi kukutana na shida za watu. Baada ya mwombaji kufika patakatifu pa patakatifu anakuwa amefika kwenye kiti cha enzi, yuko mbele za Mungu. Mungu ametuumba ili tumwabudu. Hivyo Mungu anachokihitaji kwetu ni kumwabudu. Unapofika patakatifu pa patakatifu Biblia inasema, kabla hujaomba nalikusikia. Hivyo hakuna haja ya kuanza kueleza shida zako mara ufikapo patakatifu pa patakatifu. Mungu anataka tumwabudu siyo wakati wa kumueleza shida zako. Unapofika patakatifu pa patakatifu majaribu yote uliyonayo huyeyuka yenyewe.
Madam Lilian Kimola
Lengo la kufika patakatifu pa patakatifu ni kukutana na Mungu ili tumwabudu. Unapomwabudu Mungu, yeye naye anajua wajibu wake kwa watu wake, hivyo naye anashughulikia shida zako. Kumwabudu Mungu kwa njia ya ibada, kuomba au kuimba ni kukiri ukuu wake, kumtukuza, kumwinua, kumbariki, kumshukuru, kumtukuza kwa matendo makuu aliyokwisha kuyatenda, nk.
Unaweza kumwabudu Mungu kwa kuzungumza yaani kwa kusemelea maneno ya kumtukuza Mungu, n.k. unaweza kumwabudu Mungu kwa kuimba nyimbo za kumtukuza zenye mahadhi ya kuabudu.
Ukifika patakatifu pa patakatifu unakuwa uko mbele za Mungu. Wakristo wengi waombaji wa kiwango cha kufikia patakatifu pa patakatifu wanajua aina moja tu ya kuwa mbele za Mungu wakati mtu akiwa katika maombi, aina hiyo ni ya kusemelea maneno kwa Mungu au njia ya kuimba nyimbo za kuabudu. Pamoja na njia hiyo inayojulikana sana, kuna njia nyingine, njia hiyo ni KUKAA KIMYA  baada ya kupata mpenyo, unaweza ukasikia Roho Mtakatifu anakutaka ukae kimya mbele za Mungu. Siyo kwamba ukatishe maombi bali uendelee kuwa katika uwepo wa Mungu lakini ukiwa kimya. Usiombe, usihofu bali uwe kimya. Hapo ni kumtafakari Mungu na kusikiliza kutoka kwake.
Biblia inasema;-
Nyamazeni, ninyi wenye mwili, mbele za Bwana kwa maana ametamka, na kutoka katika maskani yake takatifu (Zakaria 2:13).
Kuna wakati Mungu hataki tuzungumze tukiwa mbele zake, hasa anapokuwa tayari ameamka kutupigania. Hivyo utakapoona tayari ameamka kutupigania, hivyo utakapoona Roho Mtakatifu anakutaka kukaa kimya, ujue uko kwenye mpenyo wa kiwango cha hali ya juu. Tendo la kumwamsha Mungu ni tendo kuu sana. Hivyo wakati Mungu ameamka, mtu mwingine hatakiwi kuzungumza. Hii inafanana hata na wakati wa wana wa Israeli Mungu alipowapigania katika bahari ya Shamu, ambapo wana wa Israeli walikuwa wamemlilia Mungu sana kufuatia jaribio la Farao na majeshi yake, kuwarudisha Misri ili wakaendelee kuwatumikia.
Biblia inasema;-
Musa akawaambia watu, msiogope simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya (Kutoka 14:13-14)
Hivyo wana wa Israeli walinyamaza kimya. Mungu alifanya maangamizi makubwa kwa adui. Maandiko yanaendelea kusema
Lakini BWANA yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake (Habakuki 2:20).
Huwezi kukaa kimya mbele za Mungu ukiwa mwilini au kwenye nafsi. Mungu yupo patakatifu pa patakatifu, wewe unatakiwa ukae kimya. Hivyo kitendo cha kukaa kimya ni kitendo au ni tukio linalofanywa na mtu ambaye yuko patakatifu pa patakatifu hivyo baada ya kupata mpenyo ndipo unaweza kukaa kimya. Hii ni kusema kuwa, unapokaa kimya wakati uko patakatifu pa patakatifu ina maana unakuwa unamwabudu Mungu.

Ukimwabudu Mungu ukiwa kimya ikiwa Roho Mtakatifu atakuongoza kufanya hivyo,kuna upako mkubwa sana ambao unashuka ndani yako sawasawa na kumwabudu Mungu kwa njia nyingine baada ya kupata mpenyo. Upako unaoshuka wakati unamwabudu Mungu kwa kukaa kimya unaweza kuwa mkubwa kuliko ule wa aina nyingine. Maana wakati huo Mungu husimama na huwa katika kukutendea au kukupigania kwa nguvu zake zote.
Hivyo using’ang’anie kumwabudu Mungu kwa kuimba nyimbo za kuabudu au kusemelea maneno tu, hivyo hata kama itatokea Roho Mtakatifu amekuongoza kukaa kimya wewe kaa kimya bado ni maombi yenye nguvu tena ya kiwango cha patakatifu pa patakatifu.
Biblia inasema,
Ukae kimya mbele za BWANA, nawe umngoje kwa saburi (Zaburi 37:7)
Kunyamaza mbele za Mungu, ni muhimu wakati mwingine ni kungoja jibu au maelekezo kutoka kwa Mungu, waombaji wengi wanataka kuwa wasemaji wakuu wanapokutana na Mungu. Wao hawataki kumpa Mungu nafasi ya kuzungumza nao, ili nao wamsikilize. Biblia inasema, njoo tusemezane. Mungu anataka tusemezane naye. Hivvyo huko ni kusema kuwa, umpe nafasi, Mungu naye aseme mbadilishane mawazo.
Biblia inasema;-
Bali wao wamgojeao BWANA watapata nguvu mpya (Isaya 40:3)

Unapokuwa kimya mbele za Mungu, unamgoja Mungu akupe nguvu mpya juu ya jaribu, shida, n.k. uliyonayo. Unapokuwa umekaa kimya unamtafakari Mungu, unamwabudu kwa kumtafakari ukuu na uweza wake.

MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUFUATILIA SOMO HILI