Jumamosi, 11 Februari 2017

JE NI SAWA KUSIKILIZA YANAYOSEMWA NA MAPEPO? (1)


Utangulizi;-

Somo langu leo linaanza kama swali, lakini nafikiri nitalimalizia kama ushauri usio na masharti ya kukulazimisha ukubali ushauri wangu. Siku moja nimekwenda mahali fulani kwenye kanisa fulani, nikakuta mtumishi mmoja yuko na mtu ambaye amepagawa na pepo wachafu. Lakini  kilichoniogopesha ni vile kuona yule mtumishi ameshika daftari na kalamu! Halafu anamuuliza yule pepo ambaye amempagaa yule mtu! wewe ni nani? Pepo anajibu mimi maimuna! Umetumwa na nani? Nimetumwa na mama yake mdogo. Mko wangapi? n.k. baada ya majibizano hayo na yule mgonjwa kurudi kwenye fahamu zake anaanza kumsomea yale majibizano, kama alivyoelekezwa na pepo, kwamba katumwa na nani na wako wangapi n.k. Sasa mambo kama haya mimi nikiita ni ya kipumbavu na yanafanywa na mawakala wa shetani ndani ya kanisa, watu wengine wanasema nakosea. Maana mimi sioni tofauti kati ya mpiga ramli na hawa watu. Kwa nini nione haya kumfananisha mtumishi wa aina hii na mganga wa kienyeji. Na hali ndio kwa sasa imeshamiri katika makanisa ambayo tunayaita ya kiroho, kwa kweli ni janga kwa kanisa

UMUHIMU WA KUFUATA USHAURI WA MUNGU.
Mara nyingi ninapopata nafasi maalumu ya kuhubiri au kufundisha masomo ya Biblia au semina. Huwa  namuomba Mungu kwa unyenyekevu mkubwa sana juu ya hitaji la wale watu ambao ninakwenda kuwahudumia, katika ufahamu wangu ninakuwa na maelfu ya masomo ambayo ninatamani kuyafundisha. Lakini mara nyingi huwa ninamuomba Mungu anisaidie kunipa kile anachotaka yeye watu wajifunze. Ninakumbuka siku moja nilikuwa nnaongea na rafiki yangu mmoja ambaye ni Askofu kuhusu umuhimu wa tabia hii, akaniunga mkono na akanishuhudia yeye mwenyewe jinsi Mungu alivyomuepusha na mtego mbaya sana ambao shetani alikuwa ameutega katika huduma yake. 

Anasema Mungu alimwelekeza kwenye semina fulani kwamba siku ya kwanza akipanda madhabahuni asifundishe kitu chochote bali aongoze maombi tu. Alijaribu kushindana na maelekezo hayo lakini hatimaye aliamua kutii sauti ya Mungu, na ndivyo alivyofanya.
Elizabet Yohana na Rejoice George
Na baadae mwisho wa hiyo semina ndio akagundua ni kwa nini Mungu alimshauri afanye hivyo. Anasema hilo kanisa wakati huo alikuwa ameitwa kwa mara ya pili, kwa sababu alipokwenda kwa mara ya kwanza alifanya semina ambayo ilifanikiwa sana. Mungu alifanya mambo makubwa sana. Karibu wiki yote ile makanisa mengine ilibidi yafungwe kwa muda kwa sababu washirika wao walikimbilia kwenda kupata huduma katika semina hiyo ambayo Mungu alishuka kwa nguvu sana. Mpaka semina hiyo inaisha watu walitamani siku zigande, Kwa hiyo Mchungaji wa kanisa hilo akawa amejipanga kwa ajili ya semina nyingine ambayo alitaka iwe kubwa zaidi kuliko ile iliyopita. Kwa hiyo maandalizi yakafanyika na hatimaye tarehe ikapangwa na mhubiri akataarifiwa. Siku  chache baada ya matangazo ya semina na mialiko kuanza kusambazwa kikatokea kituko!, Mwanakwaya mmoja wakiwa katika mazoezi ya kujiandaa na semina akaangushwa na mapepo! Na wale wenye ujuzi wa kukemea na kuuliza maswali wakaanza kazi. Lile pepo likajibu kwamba mimi niliwekwa humu na huyo mtumishi anayekuja kufundisha!.
Rev Martin Pyuza
Aliniweka alipokuja kufundisha kwa mara ya kwanza. Habari ile ikachukuliwa kama ilivyo na viongozi wa kwaya huku ikiwa imevuviwa na roho ya pepo, ikapelekwa kwa viongozi wengine wa kanisa, na hatimaye ikafika kwa Mchungaji kiongozi ikiwa na maelekezo ya kipepo na kupelekwa kama ombi la kufuta hiyo semina. Wakataka huyo askofu kabla hajafika atumiwe ujumbe haraka sana kwamba semina imeahirishwa. Mchungaji wao alikuwa vizuri zaidi kiroho, na mtu mwenye msimamo, akasema kama mtu angetoa unabii kupitia Roho Mtakatifu, bado Biblia inaturuhusu kuupima huo unabii. Akaona haiwezekani mapepo kumuelekeza jinsi ya  kufanya kazi ya Mungu.
nabii mmoja Afrika kusini akiwa katika maombezi
Pamoja na msukumo mkubwa uliokuwepo kutoka kwa wazee na viongozi wengine wa kanisa lile, Mchungaji yule akakataa kabisa kubadilisha kitu chochote akawaambia mimi pia nina Roho Mtakatifu, sio lazima shetani anielekeze. Wakati ulipofika yule Askofu akaja. Lakini akiwa katika maombi Mungu akamwambia siku ya kwanza usifundishe kitu chochote. Tumia kipindi kizima kufanya maombi. Yeye hakuelewa kitu chochote kinachoendelea mahali pale ila alikuwa mtii kwa Mungu wake. Baada ya kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu, ndipo Mchungaji mwenyeji akapanda na hatimaye alimkaribisha Askofu kwa ajili ya kufundisha semina. Akaniambia alipopanda akaanzisha kawimbo ka kuabudu na kisha kuanza kunena kwa lugha, nguvu ya Mungu inashuka na kanisa zima linanena kwa lugha muda mrefu, akiona nguvu ya Mungu inapungua anaendeleza kale kawimbo kake nguvu ya Mungu inashuka tena kwa kasi kubwa, watu wananena kwa lugha mpaka wanaanguka wenye mapepo yanawatoka na wengine wanapokea uponyaji mubashara.
nabii mwingine akimlisha mtu nyoka kwenye maombi
Mpaka muda wake ulipoisha hakuna mtu aliyeweza kutoka nje. Kila mtu aliyefika siku ile akaamini kwamba yule aliyetenda yale ni Mungu. Siku iliyofuata ndio akaanza kufundisha masomo aliyopanga, watu walifunguliwa na kila mtu akaamini kwamba yule mwanakwaya, pengine bila kujua au kwa sababu ya kutokukaa vizuri na Mungu, alitumiwa na shetani kutaka kukwepa kipigo anachokipata. Mwisho wa semina ndio yule Mchungaji mwenyeji akamweleza kilichotokea. Na ndipo yeye akajua kwamba Mungu aliamua asifundishe ili alainishe kwanza mioyo ambayo ilitiwa sumu na shetani kupitia kwa yule mdada wa kwaya. Akaniambia angelazimisha kufundisha pengine watu wasingepokea kitu, kwa sababu walikuwa tayari wameshafunga mioyo yao, au shetani angeendelea kuwapa tafsiri tofauti ya fundisho lake, ili kuthibitisha maneno ya uwongo wa pepo wake.

KUNA WATUMISHI ITABIDI WAJE KANISANI NA TUNGULI
Iwapo kweli wewe mtumishi umeamua kukubali kutumia mapepo kwa ajili ya kuwatafutia watu wako uvumbuzi wa matatizo yao, huna tofauti na watu wanaoulizia mambo mbalimbali kutokana na mizimu.
tuko katika nyakati za hatari
Ukweli ni kwamba sasa hivi kanisa limeingiliwa sana na watu kama hao, na kwa sababu Yesu alisema kwamba tuyaache magugu yakue pamoja na ngano. Lakini si vibaya watu wa Mungu wakajua kabisa kwamba, pamoja na kwamba tumeambiwa tusiyang’oe kwa kila dalili hili ni gugu tujaribu kuliepuka. Nimeona mtu mmoja anajiita nabii. Mtu akifika kwake anaanza kumtabilia kama mganga wa kienyeji, Eti! Unakumbuka juzi ulikwenda kwa shangazi yako. Alikupa maji kwenye kikombe cha bati, uliporudi nyumbani ukasikia maumivu ya tumbo! Sasa Roho Mtakatifu huwa hafanyi vitu vya kipumbavu na kichonganishi kama hivyo.

Yeye ni Roho wa amani tena hfanyi hivyo kama hujatoa pesa anayokutajia bila kupungua. Sasa hiyo kama sio kuingiza biashara za mizimu kanisani ni nini?
Inawezekana tukawa hatuna maarifa sana ya kiroho, lakini mambo mengine hata akili ya kawaida inakataa kabisa kuamini kama ndipo kanisa lilipofikia. Siku moja mwanangu alitaka sana niongozane naye kwenda kwa nabii fulani maana amemweleza mambo mengi sana kuhusu mimi. Nilijaribu sana kumkwepa lakini siku moja nikaona busara ni kwenda naye ili nisimkatishe tamaa. Mimi najua hakika mafundisho yake hayawezi kunidhuru. Maana Biblia imenihakikishia kwamba nitakula kitu cha kufisha na hakitanidhuru. Kwa hiyo niliamua kwenda kujifunza maana huwa siamini hata kama mtu atauchambua ukoo wangu wote. Nilipofika nilianza kuona mambo ndivyo sivyo, kwanza mwanangu akaniambia kama una pesa kubwa tafuta chenji maana kila maombi yana sadaka. Na kweli ni kama wamejipanga kuhakikisha kwamba hakuna fedha inayobaki mfukoni kwa watu waliokuja. Pia nikaona kipande cha kitambaa cheupe, wenyewe wanasema kina upako wa mtumishi kwa hiyo ukikinunua unaweza kukitumia kwenye maombi mbalimbali. Mara kuna mafuta ya upako n.k.

Mambo haya ukiyaangalia kwa ujumla wake, unaona kabisa kwamba hawa jamaa wameshindwa kuwavalisha watu hirizi tu. Lakini mambo mengi ni kama waganga wa kienyeji tu. Mpaka hapo nafikiri ni juu yako wewe kuamua kama unaona busara kuwasikiliza  mapepo wakisema eti wametumwa na muhubiri fulani, halafu na wewe ukiamini ujue kwamba shetani anakuona kuwa wewe ni dhaifu sana. Shetani ni baba wa uongo, halafu wewe unategemea kuupata ukweli kutoka kwa shetani. Kama na wewe unafanya hivyo ujue hakika kuwa unamtumikia shetani, kanisa halijaanza leo kushambuliwa na watu wa aina hii. Kipindi fulani kuna kundi kubwa la vijana waliokuwa wanajifanya wametoka kuzimu au kwamba walikuwa wachawi wa kiwango cha juu, kwa hiyo wameokoka na sasa wanamtumikia Mungu. Katika kundi lile sikumbuki kama kuna aliyebaki kwenye wokovu mpaka leo! Lakini tuliwapokea na haraka sana tukawaamini tukawapa mpaka madhabahu watufundishe mambo yao ya kishirikina waliyokuwa wanayafanya kabla ya kuokoka na wengine mpaka wakaoa kanisani. Unakuta mtu anakwambia wakati mimi sijaokoka niliwahi kufanya hivi na vile. Au nilifanya mkataba huu na ule unamuuliza sasa baada ya hapo ulifanya nini ili kufuta ile mikataba uliyoichukua kuzimu. Utakuta hana jibu anabaki kujiumauma tu. Na hao ndio wapo makanisani leo wanajifanya kutabiri na kulielekeza kanisa la Mungu. Ukweli ni kwamba kanisa lipo kwenye giza nene ni lazima watu fulani wapaze sauti na kusema wazi kwamba hawa sio watumishi wa Mungu aliye hai

                         SOMO HILI LITAENDELEA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni