Jumapili, 5 Februari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU ( 7)


Mwl Furaha Amon


Hebu kwa muhtasari tuone yale ambayo tumejifunza mpaka hapa. Hata ingawa Mungu alitangaza kwamba anachukia talaka, hakuonyesha kabla au wakati wa agano la kale kwamba kuoa na kuolewa tena ni dhambi, isipokuwa katika haya mawili yafuatayo: (1) mwanamke aliyeachika mara mbili – au aliyeachika mara moja na kufiwa na mume wa pili – kuolewa na mumewe wa kwanza, na (2) mwanamke aliyeachika kuolewa na kuhani. Tena, Mungu hakuonyesha kwamba kumwoa aliyeachika ni dhambi kwa yeyote, isipokuwa makuhani.

Hayo yanaonekana kupingana na yale Yesu aliyosema juu ya watu walioachika wanao-oa tena, na wale wenye kuoa walioachika. Yesu alisema watu kama hao wanazini (ona 



Lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi ; na mtu akimwoa yule  aliyeachwa, azini.”Mathayo 5:32).
Basi, yaonekana tumemwelewa vibaya Yesu au Musa, au pengine Mungu alibadilisha sheria Yake. Mimi nadhani tunaweza kuwa tunatafsiri vibaya yale aliyofundisha Yesu, kwa sababu ni ajabu kwa Mungu kutangaza ghafula kitu kuwa dhambi kiadili, kilichokuwa kinakubalika kwa miaka elfu na mia tano katika Torati ambayo Yeye aliitoa kwa Israeli.

Kabla ya kukabiliana na hili kwa upana zaidi, hebu pia tuone kwamba ruhusa ya Mungu kwa watu kuoa tena katika agano la kale haikuwa na masharti yoyote yaliyotokanana sababu za talaka ya mtu, au kiwango cha hatia ambacho mtu alipata kwa sababu ya talaka husika. Mungu hakusema kwamba watu fulani walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa kwa sababu talaka yao haikuwa halali. Hakusema kwamba kuna watu fulani wanaoruhusiwa kuona kwa sababu ya uhalali wa talaka zao. Lakini mara nyingi wachungaji wa siku hizi wanajaribu kufanya maamuzi hivyo, kutokana na ushuhuda wa mtu mmoja. Kwa mfano: Mwanamke aliyeachika anajaribu kumshawishi mchungaji wake kwamba anastahili kuruhusiwa kuolewa kwa sababu yeye ni mwathirika wa talaka. Mume wake wa kwanza ndiye alimwacha – si yeye. Lakini, kama huyo mchungaji atapewa nafasi ya kusikiliza upande wa mume naye, anaweza kumhurumia kwa namna fulani. Pengine huyo mama alikuwa mkorofi na anastahili lawama kiasi fulani.
Tunaweza kuwadanganya watu, lakini hatuwezi kumdanganya Mungu. Kwa mfano: Mungu anamwonaje mwanamke ambaye anamnyima mumewe huduma za kitandani kila wakati, kisha anamwacha kwa sababu amekosa uaminifu kwake? Je, hahusiki na hiyo talaka kwa sehemu?
Lile jambo la mwanamke aliyeachika mara mbili katika Kumbukumbu 24 halisemi chochote kwamba talaka zake zote mbili ni halali. Mume wake wa kwanza aliona “neno ovu” kwake. Kama hilo “neno ovu” ni uasherati, angestahili kufa kulingana na Torati ya Musa (Walawi 20:10). Basi, kama uasherati tu ndiyo sababu halali ya talaka, pengine mume wake wa kwanza hakuwa na sababu nzuri ya kumwacha. Kwa upande wa pili, pengine alikuwa amezini, naye, akiwa mtu mwenye haki kama Yusufu wa Mariamu, “aliazimu kumwacha kwa siri” (Mathayo 1:19). Hapo kuna mengi yanayowezekana.
Mume wa pili anasemekana “akimchukia”. Hapa tena, hatujui wa kulaumiwa ni nani, au hata kama wote wanastahili kulaumiwa. Lakini bado haiweki tofauti. Neema ya Mungu ilitolewa kwake kwamba aolewe na yeyote ambaye angekubali kujaribu bahati yake kwa mwanamke aliyeachika mara mbili, isipokuwa mume wake wa kwanza.
               
                     MWISHO WA SEHEMU YA SITA

Tutakutana katika sehemu ya saba ya somo hili Mungu akuinue kwa kufuatilia somo hili.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni