Jumapili, 5 Februari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (5)



Mwl Furaha Amon


Ndoa Katika Torati Ya Musa
Unaposoma Biblia kwa uangalifu, huwezi kuona habari za watu kupeana talaka na kuoa tena baada ya talaka, mpaka unapofikia kitabu cha tatu cha Biblia kinachoitwa Mambo ya Walawi. Katika Torati ya Musa kulikuwa na agizo la kuwakataza makuhani kuona wanawake walioachwa.
Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake (Walawi 21:7).
Hapo bila ya kupepesa tunaweza kusema wazi kwamba agizo hili linawahusu zaidi watu wenye huduma zinazotambulika na kanisa. Na hii ni kwa sababu hakuna popote katika Torati ya Musa penye katazo la namna hiyo kwa watu wengine wa Israeli ambao sio watumishi kwa ujumla. Tena, andiko hilo linabeba mambo yafuatayo:
(1)                      Walikuwepo wanawake waliokuwa wameachika katika Israeli, na
(2)                      Kusingekuwepo kosa lolote kwa wanaume Waisraeli ambao si makuhani kuoa wanawake waliokuwa wameachika.
Sheria inayotajwa katika mstari huo inawahusu makuhani tu na wanawake walioachika, wanaotaka kuolewa na makuhani. Hapakuwa na ubaya wowote katika Torati ya Musa kwa mwanamke yeyote aliyeachika kuolewa tena, mradi tu hakuolewa na kuhani.
Na hakukuwa na kosa lolote kwa mwanamume, kuoa mwanamke aliyeachika, mradi si kuhani.
Kuhani mkuu (pengine kwa sababu ni mfano wa Kristo) alitakiwa kuishi kwa viwango vya juu zaidi kuliko hata makuhani wa kawaida. Yeye hakuruhusiwa hata kuoa mjane. Mistari kadhaa baadaye tunasoma hivi katika Walawi:
Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe (Walawi 21:14).
Je, andiko hili linathibitisha kwamba ilikuwa dhambi kwa wajane wote wa Israeli kuolewa tena, au kwamba ilikuwa dhambi kwa wanaume wote wa Israeli kuoa wajane? Hapana! Mstari huu unasema – tena kwa nguvu sana – kwamba isingekuwa dhambi kwa mjane yeyote kuolewa na mwanamume yeyote, mradi si kuhani mkuu. Tena unasema mwanamume mwingine yeyote alikuwa huru kuoa mjane, mradi si kuhani mkuu. Maandiko mengine yanathibitisha uhalali wa wajane kuolewa tena (ona Warumi
“Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume amefunguliwa ile sheria ya Mume” Warumi 7:2-3;

“Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.” 1Timo. 5:14).
Mstari huo vile vile unaonyesha kwamba kusingekuwa na kosa lolote kwa mwanamume yeyote Mwisraeli kuoa mwanamke aliyeachika, au hata mwanamke ambaye hakuwa bikira – “aliyenajisika katika ukahaba” – mradi si kuhani au kuhani mkuu.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Walawi 21:7 pia “Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyechwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.”. Tena, unasema kwamba katika Torati ya Musa, hapakuwa na kosa lolote kwa mwanamke aliyeachika kuolewa tena, au mwanamke “aliyenajisika katika ukahaba” kuolewa, mradi tu asiolewe na kuhani. Kwa neema sana, Mungu aliwapa wazinzi na walioachika nafasi nyingine, japo alikuwa kinyume kabisa na uzinzi na talaka.

MWISHO WA SEHEMU YA  TANO

Tukutane katika sehemu ya sita ya somo hili; kwa msaada zaidi tunaweza kuwasiliana 0677 609056

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni