Ijumaa, 10 Februari 2017

SOMO: ALICHOKIUNGANISHA MUNGU (11)



Hebu tufikiri kuhusu watu wawili. Mmoja ana ndoa, ni mtu wa dini, anayedai kumpenda Mungu kwa moyo wake wote, ambaye ameanza kumtamani mwanamke kijana anayekaa jirani. Muda si muda anamwacha mkewe na haraka anamwoa yule msichana aliyemvutia.
Yule mwingine si mtu wa dini. Yeye hajawahi kusikia hata Injili, na anaishi maisha mabaya ambayo hatimaye yanaharibu ndoa yake.
Miaka kadhaa baadaye, akiwa peke yake tu, anaisikia Injili, anatubu, na anaanza kumfuata Yesu kwa moyo wake wote. Miaka mitatu baadaye anampenda mwanamke mwenye kumpenda Mungu sana anayekutana naye kanisani. Wote wawili wanatafuta mapenzi ya Mungu na ushauri wa wengine kwa bidii, kisha wanapanga kuoana. Wanakuja kuonana, na wanakuwa waaminifu kwa Bwana na wao kwa wao mpaka kifo.
Mr & Mrs Mziray
Sasa – hebu tudhanie kwamba wote wawili wametenda dhambi kwa kuoa tena. Katika hao wawili, ni yupi mwenye dhambi kubwa zaidi? Bila shaka ni yule wa kwanza. Yeye ni sawa na mzinzi tu.
Lakini – vipi kuhusu yule mtu wa pili? Je, ni kwamba ametenda dhambi? Je, tunaweza kusema kwamba yeye hana tofauti na mzinzi – kama yule wa kwanza? Hapana. Je, tumwambie yale ambayo Yesu alisema kuhusu watu wanaoachana na kuoa tena, na kumjulisha kwamba sasa anaishi na mwanamke ambaye Mungu hakumwunganisha naye kwa sababu anamhesabu bado ana ndoa na mke wake wa kwanza? Je, tumwambie kwamba anaishi katika zinaa?
Majibu yako dhahiri kabisa. Uzinzi hutendwa na watu ambao wameoana, wanaomwona mwingine asiyekuwa mwenzi wao. Kwa hiyo, kuachana na mwenzako kwa sababu umepata mrembo zaidi ni sawa na uzinzi. Lakini, mtu ambaye hajaoa hawezi kufanya uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu, na mtu ambaye ameachika hawezi pia kutenda uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu. Tukielewa mantiki ya kihistoria na kiBiblia kuhusu maneno ya Yesu, hatuwezi kufikia maamuzi yatakayopotosha watu, na yenye kupingana na Maandiko yote.

Wanafunzi waliposikia itikio la Yesu kwa jibu la Mafarisayo, walijibu hivi, “Kama mahusiano ya mwanamume na mke wake yako hivyo, ni afadhali kutokuoa” (Mathayo 19:10). Tambua kwamba walikuwa wamekulia chini ya mafundisho na ushawishi wa Mafarisayo, na katika utamaduni uliokuwa umeathiriwa sana na Mafarisayo. Hawakuwahi kudhani kwamba ndoa ni kitu cha kudumu kiasi hicho. Ukweli ni kwamba, muda mfupi uliopita, hata wao waliamini ni halali kwa mwanamume kumwacha mkewe kwa sababu yoyote. Basi kwa haraka wakaamua kwamba ingekuwa bora kuepukana na ndoa kabisa, ili kuepuka hatari ya kuachana na kuingia kwenye uzinzi. Yesu alijibu hivi:
Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee (Mathayo 19:11-12).
Yaani – kinachoamua ni ile hamu ya kushirikiana kimwili aliyo nayo mtu, au uwezo wake wa kuitawala. Hata Paulo alisema hivi: “NI afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa” (1Wakor. 7:9). Wale waliozaliwa wakiwa matowashi au wale wanaofanywa matowashi na watu (kama ilivyokuwa zamani: watu waliwafanya wanaume wengine kuwa matowashi, ili wawape jukumu la kuwalinda wake zao) hawana hamu ya kushirikiana na mwanamke kimwili. Wale “wanaojifanya wenyewe kwa ajili ya ufalme wa mbinguni” ni wale ambao wamejaliwa na Mungu kipekee kuwa na uwezo wa kujitawala zaidi. Ndiyo maana “si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa” (Mathayo 19:11).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni