Jumanne, 7 Februari 2017

SOMO: UFUNUO WA NENO LA MUNGU (1)


Mwl F Amon


Utangulizi;
Neno la Mungu ni mwamba, na mtu aliyejengwa kwenye mwamba hata kama majaribu makubwa yatakuja atayashinda. Neno la Mungu ambalo ni mwamba ni Rhema sio logos. Neno la Mungu ambalo linao uwezo wa kumuimarisha na kumjenga mtu ni Rhema. Rhema ndilo neno ambalo humbadilisha mtu hii ndilo neno la ufunuo. Biblia inasema;-
“Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha mafuriko yakaja, pepo zikavuma zikaipiga nyumba ile isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asifanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile ikaanguka, nalo anguko lake likawa kubwa” (Mathayo 7:24  27)
wakati mtu anasikiliza neno la Mungu likihubiriwa wakati huohuo ndani yako huwa kuna sauti ya Mungu inayolifafanua hilo neno linalohubiriwa. Ufafanuzi huu hulenga mahitaji ya muhusika. Hii hutokea hata wakati unapokuwa unasoma Neno la Mungu. Sauti hii ndio ambayo huwa inafafanua neno la Mungu ndani ya mtu. Hii ndiyo Rhema huo ndio ufunuo wa neno la Mungu
”kufafanusha maneno yake kuwatia nuru, na kumfahamisha mjinga” (Zaburi 119: .)
Wakati unasoma neno au unasikiliza mahubiri, ingawaje mhubiri atakuwa anahubiri katika somo fulani jingine, wakati huohuo Mungu anakuwa anazungumza na wewe juu ya jambo jengine tofauti moyoni mwako.
Mungu hutumia maneno yanayohubiriwa kuzungumza na wewe kwa kulipua ufunuo mwingine kupitia neno hilo linalohubiriwa. Lile linalofunuliwa kwako, hilo ndilo Mungu analolitaka kwako. Hilo ndilo neno linalobadilisha, ndilo linalokujenga na kukuimarisha. Hili ndilo unatakiwa ujengwe kwake. Hiyo ndio sauti ya Mungu kwako ikisema na wewe moja kwa moja, hilo ndilo neno unalotakiwa ulizingatie na kulishika. Hilo neno ni Roho, lina uwezo lina nguvu. Mtu anayelishika hilo neno na kulitenda huyu ndiye atakayesitawi na kuwa sawa na mbegu iliyopandwa katika udongo. Huyu ndiye ambaye amejengwa katika mwamba.

biblia haijui shida zako,wala muhubiri hazijui shida zako. Mungu pekee ndiye anayezijua. Anataka kukutana nazo,hivyo Mungu anazungumza na wewe wakati neno la Mungu linahubiriwa. Atazungumza na wewe kwa njia ya ufunuo,mkristo hujengeka kiroho kupitia ufunuo.ufunuo ni sauti ya Mungu ni neno la Mungu. Ufunuo ni Yesu Kristo mwenyewe.
wakristo wameshindwa kukua kiroho na shida zao zimeendelea kuwepo japokuwa wanahudhuria kanisani kila leo. Ni kwa sababu hawajasikiliza nini Mungu anachosema nao. Bali wamechukua kauli za viongozi wao wa dini kuwa ndilo neno la Mungu. Wamechukua mahubiri pekee wakauacha ufunuo unaolipuliwa ndani yao wakati neno linapohubiriwa. neno la mungu kwako ni ile tafsiri inayotolewa na roho mtakatifu ndani yako. Ni lile neno la Mungu unalolisikia ndani yako kupitia sauti ya Mungu wakati ukisikiliza neno linahubiriwa. Sina maana kuwa mahubiri si chochote si lolote, hapana! Mahubiri ni kibebeo cha neno la Mungu. Ndani ya mahubiri ndiko kuna neno lenyewe halisi la Mungu. mfano mpunga huwezi kuula ni mpaka ukobolewe kwanza ili utoke mchele ambao ndio hupikwa na kuliwa. Kwa maana hiyo huwezi kupika mpunga halafu ule. Hivyo hivyo kuna tofauti kati ya mahubiri na ufunuo. 
Mahubiri ni chakula ambacho hakijakobolewa, ufunuo ni chakula ambacho kipo tayari kwa kuliwa. wakristo wengi wamekuwa sio waangalifu. baada  ya unabii kutolewa na watumishi wa Mungu kuhusu eneo fulani la maisha yao, wao wameuchukua unabii huo moja kwa moja kama Mungu amesema nao. Wengi wao baadaye mambo yao hayakwenda kama unabii ulivyosema, wameathirika kiroho na kukatishwa tamaa kwa hilo.
Baada ya unabii uliotolewa kuusikia, je, wewe muhusika sauti ya Mungu ndani yako imesemaje? Hata kama baada ya kusikia kauli za viongozi wa dini au kupitia unabii uliotolewa, wewe nenda ukateketeleze uliyoyasikia kutoka kwa Mungu kupitia unabii huo au kupita kauli hizo za viongozi wadini. Pindi majaribu yakija Mungu mwenyewe atapigana na majaribu hayo, maana ni yeye ndiye aliyekuagiza kufanya.
Mungu ana kawaida ya kuyapigania aliyoyasema yeye mwenyewe. Hivyo ukiwekeza katika yale uliyoyasikia kutoka kwa Mungu utakuwa umejenga katika mwamba kwa jinsi hii ni lazima ufanikiwe.
Kuna wakristo wanaooana kwa kauli za viongozi wao wa dini, majaribu yanapokuja kwenye ndoa zao huwa wanashindwa kustahimili. Wengine wanafanya biashara kwa kauli za viongozi wao wa dini n.k. Majaribu yatakapokuja hawawezi kustahimili. Sikiliza ufunuo unaolipuliwa ndani yako kupitia hizo kauli, mahubiri na nabii, ufunuo huo ndio uufanyie kazi.
Majaribu huja ili yakutoe katika mpango wa Mungu. Kama unafanya au kama uko mahali ambapo si mpango wa Mungu, majaribu yakija yatakutoa na kukuweza. Kama unachofanya au kama pale ulipo uliagizwa na Mungu, majarbu yakija hayawezi kukutoa kwenye mpango huo. Maana huo mpango umejengwakwenye neno la Mungu ambalo ndilo mwamba.
Majaribu yanapokuja, dhoruba, misukosuko huwachanganya watu kiasi wanaanza kuona kuwa huenda Mungu hakuongea nao wafanye hilo jambo. Lakini iwapo Mungu alizungumza na wewe hata kama yakija majaribu mazito ni lazima utashinda, lakini iwapo hukusikia kutoka kwa Mungu ni lazima utashindwa na majaribu hayo, maana Mungu hatakuwa pamoja na wewe.
                                     
                     MUNGU WANGU AKUBARIKI SANA

                               Somo litaendelea. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni