Alhamisi, 27 Aprili 2017

NAFASI YA MWINJILISTI NDANI YA KANISA (7)

Nafasi Ya Mwinjilisti
Mwinjilisti ni mtu aliyetiwa mafuta kuhubiri Injili. Jumbe zake zimepangwa kuwaongoza watu watubu na kumwamini Bwana Yesu Kristo. Zinaambatana na miujiza yenye kuvuta usikivu wa wasioamini na kuwafanya kuamini ukweli wa ujumbe wake.
Bila shaka walikuwepo wainjilisti wengi sana katika kanisa la kwanza, lakini ni mtu mmoja tu anayetajwa katika kitabu cha Matendo kama mwinjilisti. Jina lake ni Filipo. Tunasoma hivi: “…Tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake” (Matendo 21:8. Maneno.
Filipo alianza huduma yake kama mtumishi tu (au tuseme, “shemasi”) ambaye kazi yake ilikuwa kusimamia meza (ona Matendo 6:1-6). Akapandishwa kufikia nafasi ya mwinjilisti wakati wa mateso ya kanisa yaliyotokana na kuuawa kwa Stefano. Kwa mara ya kwanza alihubiri Injili huko Samaria.
Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule (Matendo 8:5-8).
Ona kwamba ujumbe wa Filipo ulikuwa mmoja tu – Kristo. Lengo lake lilikuwa kuanza kufanya watu kuwa wanafunzi, yaani, wafuasi watiifu wa Kristo. Basi, alimtangaza Kristo kama mtenda miujiza, Mwana wa Mungu, Bwana, Mwokozi na Hakimu anayerudi upesi. Akawashauri watu watubu na kumfuata Bwana wake.
Ona pia kwamba Filipo aliwezeshwa kwa ishara na maajabu, vilivyothibitisha ujumbe wake. Mtu anayesimama katika nafasi ya mwinjilisti atatiwa mafuta kwa karama za kuponya na zingine za kiroho. Kanisa la uongo lina wainjilisti wa uongo ambao wanahubiri injili ya uongo. Dunia imejaa wainjilisti wa namna hiyo, na ni dhahiri kwamba Mungu hathibitishi mahubiri yao kwa miujiza na uponyaji. Sababu ni kwamba hawahubiri Injili Yake. Hawamhubiri Kristo. Kwa kawaida, wanahubiri kuhusu mahitaji ya watu na jinsi Kristo anavyoweza kuwapa uzima tele, au wanahubiri mfumo wa wokovu ambao hautaki toba. Wanawaongoza watu katika uongofu bandia wenye kupooza hatia yao bila kuwaokoa. Matokeo ya mahubiri yao ni kwamba watu hata hawana nafasi za kuzaliwa mara ya pili, kwa sababu hawaoni haja ya kupokea kitu ambacho wanafikiri wanacho tayari. Wainjilisti aina hiyo wanamsaidia Shetani kujenga ufalme wake.
Nafasi ya mwinjilisti haiko kwenye ile orodha ya karama zingine za huduma katika 1Wakorintho 12:28, kama inavyotajwa katika Waefeso 4:11. Ila, kwa kuwa inatajwa “miujiza na karama za kuponya”, hizo zinahusika na nafasi ya mwinjilisti kwa sababu zilikuwa kawaida katika huduma ya uinjilisti ya Filipo, nazo zinatoa uthibitisho wa Mungu kwenye huduma yoyote ya mwinjilisti.
Wengi wanaotembea kutoka kanisa hadi kanisa na kujiita wainjilisti si wainjilisti kweli kwa sababu wanahubiri katika makanisa, tena kwa Wakristo. Kisha hawana ule uwezo wa karama za kuponya wala miujiza. (Kuna wanaojifanya kuwa na karama hizo, lakini wanawadanganya wajinga tu. Miujiza yao mikubwa ni kuwaangusha watu, tena kwa kuwasukuma.) Hao watumishi wanaosafiri wanaweza kuwa waalimu au wahubiri au wenye kuonya (ona Warumi 12:8), lakini hawako kwenye nafasi ya mwinjilisti. Ila, inawezekana Mungu kuanza huduma ya mtu kwa kumfanya mwonyaji au mhubiri na baadaye kumpandisha hadi nafasi ya mwinjilisti.
Kwa maelezo zaidi kuhusu nafasi ya mwinjilisti, soma Matendo 8:4 – 40, ambayo ni taarifa ya huduma ya Filipo. Ona hapo jinsi karama za huduma zinavyotegemeana na umuhimu wake (hasa mstari wa 14 hadi 25) na jinsi Filipo alivyohubiri Injili kwa watu lakini pia akaongozwa na Mungu kuwahudumia watu binafsi (ona Matendo 8:25-39).

Inaonekana kwamba wainjilisti wameagizwa kuwabatiza waongofu wao, lakini hawajapewa agizo la kutoa ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa waamini wapya. Hilo kimsingi ni jukumu la mitume au wachungaji/wazee/waangalizi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni