Alhamisi, 27 Aprili 2017

SOMO:WITO WA KARAMA ZA KUFANYA HUDUMA

                     

Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo … Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (Waefeso 4:7, 11-13).
Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha (1Wakor. 12:28).
Wito wa karama za kufanya huduma kama zinavyojulikana, ni tendo la kuitwa kwa waamini fulani na kupewa uwezo ili kusimama katika nafasi kama mtume, nabii, mwinjilisti, mchungaji au mwalimu. Hapa muhimu ni kuelewa kuwa hakuna mtu awezaye kujiweka mwenyewe katika nafasi hizo, kama ambavyo tunaona siku hizi kila mtu akijitwalia tu hizi nafasi ili kutengeneza umaarufu, na kukusanya kondoo waliokosa wachungaji. Ni lazima mtu aitwe na apewe karama hiyo na Mungu.
Inawezekana kwa mtu mmoja kushika nafasi zaidi ya moja kati ya hizo, lakini ni kwa makundi fulani fulani. Kwa mfano: Inawezekana mwamini mmoja akaitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwalimu, au nabii na mawalimu. Lakini si rahisi kwa mtu kuitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwinjilisti kwa sababu, huduma ya mchungaji inamtaka kwamba abaki mahali pamoja akihudumia kusanyiko la mahali pamoja. Hivyo, hawezi kufaa kwa wito wa uinjilisti ambao unamtaka mtu kusafiri mara kwa mara.
Japo hizo nafasi tano zote ni karama tofauti kwa makusudi tofauti, zimetolewa kwa kanisa kwa kusudi moja kubwa la jumla – kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kazi ya huduma” (Waefeso 4:12,).

Lengo la kila mtumishi linapaswa kuwa kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma. Lakini, mara nyingi, wale walio katika huduma hujifanya kana kwamba wameitwa kuwastarehesha watu wa kimwili wanaofika kanisani – si kuwawezesha watakatifu kuwa tayari kwa huduma. Kila mtu aliyeitwa katika nafasi mojawapo kati ya hizo zilizotajwa anapaswa kutathmini mara kwa mara mchango anaotoa kwa habari ya “kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma”. Kama kila mtumishi angefanya hivyo, wengi wangeondoa shughuli nyingi mbalimbali ambazo zinahesabiwa kwa sasa kwamba ni “huduma”.

somo litaendelea. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni