Alhamisi, 27 Aprili 2017

WITO WA KARAMA ZA KUFANYA HUDUMA (3)

Tutazame Kwa Karibu Nafasi Ya Mtume
Neno la Kiyunani linalotafsiriwa mtume ni apostolos na maana yake halisi ni “aliyetumwa”. Mtume wa kweli wa Agano Jipya ni mwamini anayetumwa na Mungu kwenda mahali fulani au maeneo fulani ili kuanzisha makanisa. Anaweka msingi wa kiroho wa “jengo” la Mungu, na anafananishwa na fundi ujenzi mkandarasi. Paulo, yeye mwenyewe akiwa mtume, aliandika hivi:
Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi kama mkuu wa wajenzi wenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake (1Wakor. 3:9-10a).
“Mkuu wa wajenzi” husimamia mpango mzima wa kujenga – yeye anaona jengo lililokamilika. Si mtaalamu kama vile fundi seremala au mwashi. Anaweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi ya fundi seremala au mwashi, lakini pengine hataifanya vizuri kama wao wenyewe. Vivyo hivyo, mtume anao uwezo wa kufanya kazi ya mwinjilisti au mchungaji, lakini kwa muda tu wakati anapoanzisha makanisa. (Mtume Paulo kwa kawaida alikuwa anakaa mahali kwa miezi sita hadi miaka mitatu.)

Mtume anafaa sana kuanzisha makanisa, kisha kuyasimamia ili kuhakikisha yanaendelea kama Mungu anavyotaka. Mtume anawajibika kuweka wazee au wachungaji au wasimamizi ili kuchunga kila kundi analoanzisha Biblia inasema "Hata nilipokwisha kuhubiri injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini". (Matendo 14:21-23) 

Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuwaweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;Tito 1:5).

somo litaendelea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni